“Kila kitabu na zama zake.” Usemi huu umejidhihirisha kufuatia kasi iliyopo kwenye muziki wa Singeli uliochukua nafasi kubwa katika masuala ya burudani nchini.
Muziki huu umekamata maeneo mengi nchini kufuatia mirindimo na maneno yanayoendana na wakati uliochagizwa kwa kiasi kikubwa na msanii, Amani Khamisi a.k.a ‘Man Fongo’.
Man Fongo anasema kutokana na kasi ya kuenea kwa Singeli humu nchini, kuna uwezekano mkubwa kwa muziki wa Bongo Fleva ukapoteza umaarufu wake baada ya muda.
Man Fongo ambaye amepachikwa jina la ‘Mfalme’ wa Singeli, anasumbua kwa vibao vingi sana kikiwemo cha ‘Hainaga Ushemeji.’
Anasema wasanii wa Bongo Fleva wana kazi kubwa kuhakikisha wanabaki kileleni kutokana na namna muziki wao ulivyopokewa vizuri na mashabiki.
“Muziki tunaouimba ni wa mtaani, ambako ndiko chimbuko la watu wa Uswahilini. Kwa sasa watu huwaambii kitu kuhusu muziki wetu. Nawaambia ukweli kabisa wasanii wa Bongo Fleva wakaze buti twende sawa au watafute kitu kingine cha kufanya,” anasema Man Fongo.
Akisisitiza umaarufu wa muziki huo wa Singeli unavyotapakaa nchini, Man Fongo anabainisha: “Ujue wenzetu wanaimba vitu vya kubuni wakati sisi tunaimba maisha halisi ya Uswahilini, kwa maskini wenzetu. Awali watu waliuita muziki wa kihuni kutokana na vijana kufanya matukio mbalimbali ulipokuwa unapigwa kwenye shughuli za mitaani nyakati za usiku maarufu ‘Vigodoro’.”
Lakini kadiri siku zinavyokwenda, muziki huo umeanza kueleweka kiasi cha baadhi ya wasanii wa Bongo Fleva kuanza kushirikiana na wasanii wa Singeli kwenye nyimbo zao.
Man Fongo anatolea mfano wa Mwana Hip Hop, Joseph Haule, maarufu Profesa Jay, ambaye ni Mbunge wa Mikumi kupitia Chadema, alipofanya kolabo ya nguvu na msanii wa Singeli, Sholomwamba.
Msanii wa muziki wa Bongo Fleva, Khery Sameer ‘Mr. Blue’, anasema hivi sasa muziki wa Singeli ndiyo unawakilisha maisha halisi ya Kitanzania. Aliyasema hayo baada ya kufanya kolabo na msanii wa muziki huo Meja Kunta, katika wimbo wa ‘Mamu Remix’.
“Singeli ndiyo muziki bora kwa sasa Tanzania, kwa kuwa unazungumzia maisha halisi ya Kitanzania, hata wasanii wake wanaishi maisha ya kawaida tofauti na wasanii wengi wa Bongo Fleva,” anasema Mr. Blue.
Safari ya muziki ya Man Fongo
Man Fongo, ambaye anasimamiwa na Makes Entertainment, anasimulia mengi kuhusiana na safari yake ya maisha na muziki kwa jumla.
Anasema alianza muziki akiwa darasa la tano mwaka 2006 wakati akifanya shughuli zake za u-DJ ambapo ilikuwa kama kurusha roho tu.
“Kipindi hicho Msaga Sumu ndiye alikuwa anajulikana zaidi na nilikuwa ninapitisha maneno kwenye baadhi ya nyimbo zake, mashabiki wakatokea kunikubali wakataka nijaribu kuimba. Licha ya kuanza muziki niliendelea na masomo yangu hadi nilipomaliza darasa la saba mwaka 2008. Sikufanikiwa kuendelea na masomo ya sekondari kutokana na kipato cha familia yangu kuwa duni,” anasema Man Fongo.
Anatamka kuwa muziki umekuwa ni maisha yake, ameanza kupata mashabiki wengi ambao wameuelewa zaidi muziki wake.
Fiesta 2016
Man Fongo anasema maonyesho makubwa ambayo alikuwa akiyafanya ni ya kuitwa kwenye shughuli za watu kama ndoa, sherehe za kuzaliwa na kadhalika, lakini anamshukuru Mungu baada ya kuitwa kwenye Fiesta ya mwaka 2016.
Man Fongo anasema hapo zamani Singeli ilionekana kama muziki wa kihuni lakini sasa watu wameuelewa muziki huo.
Malengo
Man Fongo anasema matarajio yake ni kufika mbali kimataifa, lakini hawezi kufika huko iwapo Watanzania hawatauunga mkono muziki wa Singeli.
“Kila siku ninawaza kuwaburudisha mashabiki wangu na kuupaisha muziki huu kimataifa zaidi, ni ndoto yangu kuwainua wadogo zangu ambao hawajasikika.
“Pia nimeamua kuacha tabia ya kutoa nyimbo tatu na sasa nitaanza kutoa albamu nzima, natarajia kutoa albamu yangu ya kwanza hivi karibuni,” anasema Man Fongo.