Amepata kuswekwa rumande kwa kuendesha trekta

Petro John Nyerere ni mmoja wa wajukuu wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Baba yake ni John Guido Nyerere, mtoto wa nne wa Baba wa Taifa. Petro ni mmoja wa wajukuu wachache kati ya wengi walioishi muda mrefu na babu yao pamoja na bibi yao, Mama Maria Nyerere.

Jina lake maarufu kwa babu na bibi zake ni “Mwendo”, jina analosema alipewa na babu yake kutokana na vituko na utukutu wakati akiwa mdogo.

 

“Nilizaliwa katika Kijiji cha Komuge (Kwa sasa ni Wilaya ya Rorya). Nililelewa na bibi na babu yangu kijijini hapo kwa miezi zaidi ya mitatu. Hii yote naamini ilikuwa ni baraka ya babu kumtaka bibi aniangalie,” anasema.

Simulizi zinasema Petro alikuwa mtundu mno. Hata yeye mwenyewe anakiri; “Nikiwa mdogo nilikuwa mtundu sana, nakumbuka nikiwa naendesha baiskeli na kukimbia katika vibaraza vya Ikulu, siku zote wakati tuko Msasani babu akiwa anarudi kutoka ofisini ama safari nilikuwa nampigia saluti na kumfungulia mlango wa gari alimopanda.

“Wakati huo mpambe wake Mzee Makwaia (marehemu Luteni Kanali mstaafu Adam Makwaia) na hata wengine aliokuwa nao hadi kifo chake, alikaa pembeni kuniachia kufanya kazi hiyo ya kufungua mlango…Ilikuwa kama ndiyo kazi yangu kila akifika pale nyumbani Msasani.

“Nikiwa mdogo, wakati wa kula jioni alihakikisha anaongea na mimi hadi nimalize chakula, maana alijua kabisa kwamba nikikaa kimya nitasinzia au kulala kwa sababu ya uchovu wa mchana kutwa kutokana na utundu wangu wa kupenda kucheza.

“Tukiwa Butiama tulianza mashindano ya nani atakuwa wa kwanza kufika shambani. Mara nyingi alinishinda, kwani ilibidi nisubiri lifti yake. Akawa akinitania kwa kuniambia sina ujanja hadi nimsubiri. Enzi hizo tulikuwa na farasi pale nyumbani. Kwa msaada wa mtunza farasi aliyeiwa John (alijulikana zaidi kama John Farasi), akanifundisha kuendesha farasi, na kwa muda mfupi nilikuwa nimeweza kujua. Siku moja nikaamka mapema na kupanda farasi na kwenda shambani kabla babu hajaondoka.

“Alipofika shambani alinikuta nikiwa nimewahi, lakini nikiwa nimeshindwa kutelemka kutoka kwenye farasi. Siku hiyo hiyo jioni ndugu yetu aitwaye Mjoma wa Chifu Wanzagi alikuwa akipiga ng’ombe katika zizi dogo lililokuwa Mwitongo. Kitendo hicho kilimuudhi sana babu. Akamtia makwenzi. Baadaye akaniuliza nimefikaje pale mapema kabla yake? Nikamjibu kuwa yeye alikuwa anazunguka na barabara, mimi nimeruka kwenye mawe. Kuanzia siku hiyo akanipa jina la ‘Mwendo wa Kuruka’.

“Babu alipenda sana wajukuu zake. Alihakikisha kila Desemba tunakwenda Butiama. Sisi wajukuu tuliokuwa wadogo tulisafiri naye kwa ndege ya CCM. Huko tulikutana ukoo wa Burito. Mara nyingine kulikuwa na sherehe za ukoo, kitu kilichosaidia kujuana na kuwa pamoja. Hadi leo hii nakumbuka na kufaidi utaratibu huo wa kutukutanisha wanafamilia. Wengi tumetambuana, hasa ikizingatiwa kuwa ukoo wa Chifu Nyerere Burito ni mkubwa sana,” amasema.

Petro anakumbuka kuwa likizo za mwezi wa sita mara nyingi Mwalimu alipenda yeye na wajukuu wengine wamfuate Butiama. Anasema pamoja na mambo mengine mengi, babu yake alihakikisha familia yake inadumu katika imani ya kumuabudu Mungu.

“Babu alikuwa nguzo kubwa katika familia hasa katika imani, sikumbuki siku ambayo akiwa Dar es Salaam tulikosa kwenda kanisani kwanza kabla ya shule. Wakati mwingine Mwalimu Ndosi (wa Shule ya Msingi Muhimbili) alikuwa anatuadhibu kwa sababu ya kuchelewa.

“Mimi na dada yangu, Wade, tulilelewa na babu na bibi. Ilikuwa mwiko kumwita mfanyakazi/mtumishi kwa jina au kazi yake. Mfano kumwita mtu ‘dereva’. Tulitakiwa tumwite ‘uncle’ au ‘auntie’. Tabia hii tumeendelea nayo hadi leo. Mafunzo ya dini na heshima kutoka kwa babu na bibi yanatupa faraja hadi leo. Namkumbuka babu sana. Leo hii kwa heshima aliyotuachia tunaweza kutembea kifua mbele na kujiona huru,” anasema.

Petro anasema mbali ya kujengwa kiimani, pia amejengwa kuipenda kazi.

“Tulipokuwa Butiama, Mwalimu alihakikisha tunapenda kilimo na tunashiriki kwa vitendo…alitupeleka shambani saa 4 asubuhi na kurejea kwa chakula cha mchana na kurudi tena shambani saa 9 alasiri hadi jioni.

“Kwa wakati huo tuliona tabu na mateso, ila sasa tunaona matunda yake. Lakini kuna kitu nakichukia hadi leo. Nachukia makande maana kila siku kabla ya kwenda shamba tulikula makande na chai kabla ya kupewa yai…mwenyewe akisema chakula cha kutia nguvu.

“Watu wengi walimjua babu kwa siasa zake, hayo nikiwa shule sikuyajua hadi nilipopata nafasi ya kwenda kusoma sekondari Kenya. Kwa kweli niseme wazi kuwa babu hakupenda uamuzi wangu wa kwenda kusoma huko. Aliniona nilikuwa bado mdogo kwenda kusoma mbali. Nikaona kama ananizibia ila baadaye shida ilikuja pale ambako alikuwa akiniuliza maswali ya historia ya Tanzania na kujikuta siijui vizuri, wakati wenzangu wakijibu bila tabu. Mimi nilijua vizuri historia ya Ulaya.

“Nikiwa Kenya nilikuwa nikimwandia barua nikimweleza jinsi watu walivyomzungumza kuhusu ushujaa wake ambao sikuujua awali, kwani kwangu mimi yeye alikuwa babu tu!

“Nilimweleza watu walivyonijali na kunipa huduma ya ziada walipojua kuwa ni mjukuu wake. Cha kushangaza alikuwa hajibu nikadhani labda hazifiki ila siku moja nikiwa likizo, tukiwa mezani bibi akamwambia ‘babu umemwambia Mwendo unapata barua zako?’ Alijibu, ‘Bibi, Mwendo amekua sasa.’ Babu hakutaka tujisikie tofauti au kujikweza.

“Nakumbuka tukiwa Butiama, TV ilikuwa katika library yake, hivyo ukitaka kuangalia mpaka umwombe funguo wakati hayuko ofisini. Na ukipewa funguo ukifika kule na kuanza kuchezea kazi zake ilikuwa lazima upigwe kwenzi. Babu alikuwa hachapi kwa kutumia fimbo. Yeye adhabu yake ilikuwa ni makwenzi. Wajukuu wote tumepigwa makwenzi!

“Babu alitufundisha kuheshimu kila mtu na kujua kuwa chochote unachopata ni kwa ajili ya jitihada zako, na si kwa kutumia cheo cha mtu mwingine. Namkumba babu yangu kwa kutuacha na peace of mind.”

Uanachama wangu NCCR-Mageuzi

Mwaka 1995 wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu, baba mdogo Makongoro alikuwa amejiunga NCCR-Mageuzi. Kipindi hicho nilikuwa nasoma Morogoro. Alipokuja nilivutiwa sana na kampeni zake, nikachukua kadi ya NCCR na nikakabidhiwa na Mheshimiwa Augustine Mrema.

“Baada ya siku chache babu akaja. Nilipokwenda kumwona aliniuliza kuhusu maendeleo yangu ya shule akiwa kama mzazi mwingine, kwani alikuwa ndiye anayelipa ada. Hakuniuliza kitu chochote kuhusu NCCR hadi mtu mmoja aliponiambia mbele ya babu, ‘Mwendo nimeona kwenye gazeti umechukua kadi ya NCCR-Mageuzi’. Kabla sijajibu, babu akasema, ‘Mwendo anaweza kujiunga na chama chochote’”.

“Na-miss those days! Ilikuwa mjukuu ukimaliza chakula kwenye sahani anakupigia makofi na kukupa chocolate kutoka Swiss Air. Hapa ikumbukwe kuwa alipenda sana kusafiri kwa Swiss Air. Chocolate alizopewa alituletea. Ilikuwa asipotuletea tunamwandama! Kwa chakula, mtindo ulikuwa kwamba upakue chakula unachoweza kukimaliza. Hakupenda kabisa kuona mtu akimwaga chakula na ilikuwa mwiko kuimba mezani wakati wa chakula.

“Watu wengi wanasema mjukuu kulelewa na babu na bibi anadekezwa. Kwetu sisi haikuwa hivyo, kwani alikuwa mkali kama mzazi. Nakumbuka tulikuwa tunaitwa ‘watoto wa bibi’. Babu akitoka safari, kama umefanya makosa utakuwa tumbo joto maana unajua adhabu ya kukurudi lazima utaipata.

 

“Babu nitamkumbuka kwa kuheshimu imani ya kila mtu. Nakumbuka katika harusi yangu, Balozi Job Lusinde alisema, ‘Petro umemuenzi babu yako kwani umeoa mwanamke wa Kiislamu’.

“Babu alijumuika na watu wa dini, kabila, rangu na hali zote. Ukifika Butiama ulikuta mezani amekaa na watu wa aina zote, hata wenye ukoma alikula nao mezani. Kuna masikini wengi waliofika nyumbani tukala nao meza moja.

“Babu hakutaka kudekeza mjukuu, mtoto au ndugu. Hakuna siku yoyote katika familia yetu aliyejiona yuko juu. Mara nyingi tulienda shule kwa kutumia usafiri wa UDA. Baba mdogo Manyerere alikuwa anaenda shule (Tambaza) kwa kutumia baiskeli aina ya Swala aliyopewa na babu,” anasema Petro.

Tukio ambalo sitolisahau

Petro anasema kuna mambo mengi yanayohusu maisha yake na babu yake, Nyerere, ambayo kamwe hawezi kuyasahau. Kati ya hayo, anakumbuka hili, “Kitu ambacho sitakisahau, babu alinipeleka polisi kwa sababu ya kuendesha trekta lake.

“Siku hiyo ilikuwa hivi; wakati tunatoka shamba aliniuliza kama najua kuendesha trekta. Nikamjibu, ‘naam, najua’. Akauliza kama najua kulima kwa kutumia trekta, nikamweleza ‘hapana’. Akanitaka nimwombe dereva aitwaye Ilendeja anifundishe.

“Mimi nikaona ndiyo nimepewa ruksa ya kuendesha trekta! Baada ya chakula cha mchana alipoenda kupumzika, nikaendesha trekta kwenda kijijini. Niliporudi nikakuta ananisubiri na kuuliza nani ameniruhusu kuendesha trekta? Nilipomwambia tulivyoongea naye kabla hajaenda kulala akasema, ‘unatakiwa kujifunzia shamba.’ Akaita polisi, nikalazwa rumande.

“Kesho yake akaamuru nitolewe. Akanipa pole na kuniambia hakumaanisha nichukue trekta ninapojisikia. Likawa fundisho kuwa usifuje mafuta au kuchezea trekta bila kazi ya msingi.”

Petro anasema ana mengi ya kuelezea kuhusu maisha yake na babu yake, na kwamba kwa kuwa kila mwaka anakumbukwa, basi hayo mengine atakuwa akiyaeleza kadri atakavyoweza.

ndiye Petro Nyerere John Guido Nyerere, mjukuu wa kwanza wa kiume wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere