Sasa ni mwezi tangu vilio vilipotawala Alhamisi, Desemba 17, 2015 baada ya wakazi wa maeneo ya Jangwani, Dar es Salaam kukumbwa na bomoabomoa, ambako nyumba zaidi ya 100 zilibomolewa katika maeneo ya Bonde la Mkwajuni na Magomeni katika Manispaa ya Kinondoni.
Inasemekana mamlaka za ubomoaji zinalenga kubomoa nyumba 4,000 huku nyingi zikiwa katika Bonde la Mto Msimbazi.
Vinara wa bomoabomoa hiyo; Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi; Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira, na Manispaa ya Kinondoni watabomoa nyumba zote na miundombinu mingine iliyokuwamo katika maeneo oevu, kando ya mito na bahari.
Kuna taarifa zinazokinzana ama za kweli, zilizokuwa zikitolewa mara kwa mara na Serikali ya Awamu ya Nne, iliyokuwa ikiongozwa na Rais Jakaya Kikwete, kwamba imekuwa ikiwasihi wakazi wa maeneo yaliyotajwa wahame kutoka maeneo hayo ya mabondeni, na iliwapa viwanja Mabwepande, Kinondoni ambako walitakiwa kwenda kujenga na kufanya mastakimu huko, lakini waliuza sehemu walizopewa na kurudi kuendeleza sehemu za mabondeni kinyume cha sheria za mazingira na mipangomiji.
Maeneo ya fukwe za bahari, kingo za mito na mikondo ya bahari ni maeneo hatarishi, hivyo kuwataka wananchi wahame, tena kwa hiyari zao, kabla kufikiwa na bomobomoa za mamlaka husika.
Huwezi kukana; ilikuwa ni zahma, taharuki, nguvu nyingi, ubabe, kukosa tafakuri, imani, ubinadamu, utu, ubinafsi vilivyotamalaki wakati ‘sherehe’ hizo za bomoabomoa zilipokuwa zikifanyika. Matingatinga yaliyokuwa na uwezo wa kubomoa, kufinyanga matofali, mbao, nondo, bati zilizochakaa na mpya kwa baadhi ya nyumba, milango, madirisha na vifaa vyovyote yalifanya kazi ipasavyo.
Kauli za kukosoa utendaji wa Rais wa Awamu ya Tano, ya Mheshimiwa John Pombe Magufuli (JPM), kwenye suala la bomoabomoa, zilitawala anga na duru za siasa, wananchi wakishutumu kwa kusema ‘alikuja huku mabondeni kuja kuomba kura zetu sasa anachofanya…Alikuja viwanja vya Jangwani ambako pia ni mabondeni na kuleta falsafa ya ‘Hapa Kazi Tu’. Nenda kaangalie miundombinu iliyopo pale ilivyowekewa alama ya ‘kosa’ ya nguvu na neno bomoa kando ya ‘X’. Wahanga wameweka kisasi, wanasubiri miaka mitano ipite. Hata hivyo, ni Serikali ya JPM iliyoamrisha kadhia hiyo?
Familia zilizowahi kuokoa vitu walau vya ndani kama vitanda, magodoro, masanduku ya nguo, vyombo vya kupikia na hata vyakula walikuwa na bahati kama ya mtende kuota mahali pasipokuwa na maji, kwa jinsi tendo la bomoabomoa lilivyowaduwaza wananchi hao. Hiyo ilikuwa ni ‘zahma’l karaadys’ kwani walishindwa kuokoa mali hizo, hali iliyoleta taharuki isiyoelezeka. Zipo taarifa za vifo kutokea pia.
Wakati ‘sherehe’ hiyo ya ubomoaji ikifanyika, mamlaka husika zilitumia nguvu nyingi mno pasipo lazima yoyote, kwani katika wale waliokuwa wakishuhudia nyumba zao na katika ile kuwania walau mtu aokoe kitu, alikutana na nguvu ya dola – askari waliokuwa kama wapo katika hifadhi ya taifa kwamba akitokea simba au mnyama yoyote wa hatari wakabiliane naye kwa kumfyatulia risasi na wammalize papo hapo.
Ndivyo hali ilivyokuwa katika eneo la ubomoaji, hasa Bonde la Mkwajuni bomoabomoa ilikoshuhudiwa ‘live’. Walitanda wakiwa na silaha za moto na yeyote aliyejaribu kuwania chochote alifurushwa si kwa nia ya kumwepusha asije labda akaangukiwa na ukuta utaofinyangwa na kijiko cha tingatinga, bali kumkomesha akome kuchukua chochote kama alivyokoma kunyonya ziwa la mama yake, akae mbali na akisogea atakiona cha mkata kuni.
Kama mamlaka husika haikuwafundisha yale mabaya waliyowafanyia wananchi waliokuwa wakikumbwa na bomoa ile, basi askari walikuwa wamedhukuru ubabe na ubaya wa hali ya juu wakiamini kuwa wao hawawezi katika wakati wowote wa maisha yao kuja kufikwa na lolote ili watu waje wawachukulie madhila yatakayowakuta kwa upole maridhawa. Si walikuwa wametumwa bwana kama vile mbwa anapotumwa na bwana wake akamng’ate mtu!
Ikaja zamu ya Serikali ya JPM. Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, ikiongozwa na Waziri wake aliyevalia kitanashati huku akiwa na miwani midogo iliyopamba uso wake unaoonesha sura ya umri mdogo, William Lukuvi, akishirikiana na mwenzake wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, na si mwingine bali kijana anayekuja juu katika siasa za nchi hii, January Makamba, kwa pamoja wakitangaza kinachowasibu wananchi, wakidiriki hata kuwaita ‘wavamizi’ huku wakiwa na jina la kawaida la ‘watu wanaoishi mabondeni,’ walishirikiana kuweka hanikizo la kuwasuduku wananchi hao kuwa walikwishaonywa na hawakusikia, hivyo kinachowakuta wasilie na mtu yeyote ila nafsi zao.
Walipokuwa wakihanikiza suala la kuvunjiwa na walikuwa wakitangaza kwa kupokezana kama watangazaji wa mpira wa siku hizi katika runinga ama radio; kwa mfano, mtangazaji akimtangaza mchezaji aliyepata mpira hadi anafika lango la wapinzani na kufunga bao, anamkaribisha mtangazaji mwenzake awaeleze wasikilizaji na watazamaji jinsi bao lile lilivyoingizwa kimiani, ndivyo walivyokuwa wakifanya mawaziri hao wa Serikali ya JPM.
Mmoja anasema ‘Serikali itaendelea na kazi ya ubomoaji kwa sababu ninyi ni wavamizi mmevamia maeneo ya wazi kinyume cha sheria’; mwenzake anapokea na kusema ‘hakutakuwa na fidia kwa yeyote hata angelikwenda kwa nani, (hata mahakamani mtakuwa mnapoteza pesa zenu bure kwa kuweka mawakili), kama kulikuwa na fidia au mlipatiwa mahali mbadala, basi ni huko nyuma si wakati huu sisi tukiwa tunaendesha kazi hii ya bomoabomoa.’
Huku ni kukosa tafakuri, utu, ubinadamu na ni ubinafsi wa hali ya juu, kwa sababu tu wao hawapo maeneo ya wazi yaliyovamiwa na ‘wavamizi’ hao na wanaoishi maeneo hatarishi ‘ambayo tukishawatimua tutayafanya maeneo haya kuwa ya ‘burudani’.’
Yamkini wananchi walikwishapata burudani ya kiutu huko mabondeni kwani walioana na kupata watoto, ambao leo wengine ni viongozi serikalini na walipakodi. Walifanya sherehe zao za kusherehekea sikukuu za Kiislamu, za Kikristo, matamasha ya kila aina, sasa leo burudani itakayokuwa huko baada ya bomoabomoa ni pasua kichwa.
Hawakusikitika na kwa mwendo huo hawatasikiliza chochote hata angesema nani!
Huku, kwa upande mwingine, ni kuonesha Serikali kuwa na dhamira ya kuwatesa wananchi wake kwa kuwalazimisha kuhama katika makazi yao bila sababu za msingi; japo Serikali hiyo hiyo haiwezi kuvumilia kuwaona wananchi wanaendelee kuishi katika sehemu ambazo ikinyesha mvua kubwa maisha yao yamo hatarini.
Katika ahadi zake, Chama cha TANU kilicholeta Uhuru hapa nchini, kilimwahidi mwananchi kwa kumwambia ‘Binadamu wote ni sawa’ maana kila mtu anahitaji chakula, mahali pa kulala na mavazi, hivyo anahitaji vitu hivyo.
Kwa bahati nzuri kwelikweli siku ile viongozi wale watanashaji na wanaokuja kwa kasi katika siasa za kweli nchini, walimnyang’anya mwananchi chakula chake siku ile walipovunja nyumba iliyosababisha akose makazi huku akiwa hakuokoa chochote pamoja na nguo zake zilizokuwamo katika masanduku na makabati ya kizamani ya mbao.
Hawakuwa na huruma, utu, ubinadamu, imani na kuhurumia binadamu kwa sababu tu wao leo wako kwenye mstari ulionyooka wakati hawa wavunjiwao wako kwenye mstari uliopindapinda.
Hali hiyo kwa ubaya wake haina kipimo, ilistahili kila mja na muungwana asikitike na kuonesha simanzi, lakini kwa wakati ule haikuwa hivyo kwa viongozi wale waliokuwa na dhamana ya ardhi na mazingira.
Lakini mwishoni mwa wiki iliyopita ya Ijumaa, Januari 7, mwaka huu, viongozi wanne walikutana na kufanya tathmini ya uhamishaji wa wakazi wa mabondeni katika Jiji la Dar es Salaam na taarifa kutolewa rasmi na Ofisi ya Makamu wa Rais.
Sasa viongozi hao wa Serikali wameingiwa na imani na huruma, nafsi zao zimejisuta na zikaonesha jitimai kwa wananchi. Wanajua wengi wa wananchi ni wa hali ya chini ndiyo maana wamejenga huko, wamejenga nyumba hizo kwa muda mrefu kwa kubandika tofali moja moja, wakijinyima huku wengine wakiwa wamepatiwa nyaraka maridhawa ama za kughushi na watumishi wa Serikali waliowamilikisha maeneo hayo.
Kwa mshangao, ni Serikali hiyo hiyo juzi tu iliyokuwa na jicho lililoiva wekundu na kutoa kauli za kuliza wananchi kuwa hata wafanye nini wataondolewa tu hata kwa sase, leo hii huruma hii wanayoonesha wameipata wapi!
Serikali imeonesha kuelewa kuwa kuna kesi za kupinga ubomoaji huo, hivyo itaheshimu amri za Mahakama kuhusu mapingamizi yaliyowekwa na baadhi ya wakazi hao wa mabondeni, lakini pia itafuatilia kesi hizo ziishe upesi ili taratibu zinazofuata zifanyike.
Je, kwa kuangalia maudhui na mienendo ya kesi Serikali inadhani itashindwa katika shauri hilo lililopo mahakamani?
Sasa Serikali inatambua watumishi waliopewa kazi ya kubomoa wakiwamo waliopewa kalamu nyekundu za kuandika alama ya kosa ‘X’ kwenye nyumba, hapana shaka walifanya kazi hiyo kinyume na misingi ya sheria zinazotekelezwa, na kinyume cha misingi ya haki na uwazi. Imesema itawachukulia hatua za kinidhamu watumishi wake hao, na mara moja itaanzisha dawati maalumu la malalamiko huko Wizara ya Mheshimiwa Lukuvi kupokea mlalamiko au maswali kuhusu jambo hili la bomoabomoa. Lakini hadi hapo nyumba zaidi ya 700 zimeshabomolewa kwa staili ile.
Tumeona sote kuwa Serikali haina simile na suala la ubomoaji, lakini hapo hapo imeagiza ofisi za Serikali za Mitaa kwenye maeneo yaliyoathirika kufanya tathmini na kuangalia familia zinazohitaji msaada wa kibinadamu zisaidiwe!
Mfalme wa mazingira, Makamba mwenyewe, alikubali kuwa kila utaratibu lazima ukumbwe na changamoto, hata mimi nalijua hilo na yeye akaliona, la waliobomolewa wakiwa na hati na vibali vya ujenzi vya Serikali, lakini wabomoaji, kwa jazba, ubinafsi na upendeleo hawakutaka kabisa kuangalia hayo. Alibainisha maeneo matatu – yaliyokwishabomolewa, yaliyowekwa alama ya kosa yaani ‘X’, lakini hayajabomolewa na yaliyo katika mazingira hatarishi, lakini hata hayajawekewa alama ya ‘kosa’ – je, ni jazba, upendeleo au ubinafsi?
Alipokuwa akizungumza na wananchi wa ‘mabondeni’ katika ziara yake hivi karibuni, Makamba aliyevaa shati moja ‘kali sana’ la rangi ya pinki, alionesha uso wa huruma, huku akiwa amekaa na mtoto wa miaka ipatayo mitano kuonesha moyoni kabisa ‘huyu maskini ya Mungu ana kosa gani hadi leo awe hana pa kuishi!’ Aliwasikiliza wananchi ambao japo walikuwa na taharuki, lakini walikiri na kuonesha kufahamu kuwa wamejenga kwenye mazingira hatarishi.
Dawa yake baada ya mtu kukiri kosa, si kama mahakamani kumwona mpumbavu kwa vile Mahakama zina tabia ya kuhangaishwa na kulazimishwa ‘mwelekeo wa rushwa’, na kumfunga miaka mia kwa sababu alikiri kosa.
Kwa Makamba haikuwa hivyo. Alikubaliana nao kwamba basi watafutiwe mahala mbadala. Ingelikuwa jambo kuntu kwelikweli kama kabla ya bomoabomoa wawe wamewatafutia mahala mbadala. Kwa wapangaji katika nyumba hizo linaonekana gumu ila kwa namna moja ama nyingine wakatafute mahali kwingine wakapange waendelee na maisha!
Hii maana yake ni kuwa JPM alichonga mwiko asije akaungua mkono wakati akipika. Mwiko ni Lukuvi na mdogo wake, Makamba, JPM hawezi kuungua mikono. Na ni rahisi JPM kusema kwanza hakuwatuma wakawanyanyase wapiga kura wake. Kama JPM hajasema hayo, bahati yao. Kwa hiyo lawama ni lao.