Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Simiyu
Mkoa wa Simiyu bado una takwimu kubwa za watu wenye maambukizi ya ugonjwa wa kifua kikuu (TB), ambapo takwimu zinaonyesha watu 3,321 walibainika kuwa na maambukizi mwaka 2023.
Akizungumza na waandishi wa habari kuelekea maazimisho ya siku ya kifua kikuu Duniani Machi 23, 2024 kwa niaba ya Mkuu wa mkoa, Mkuu wa Wilaya ya Itilima, Anna Gidalya amesema kuwa takwimu pia zinaonyesha bado kuna maambukizi mapya kwenye jamii.
“ Mwaka 2022 wagonjwa waliogundulika kuwa na TB walikuwa 3709 kati ya hao wagonjwa 3687 walikugundulika kuwa na maambikizi mapya na mwaka 2023 waliogundilika walikuwa 3,321 kati ya hao 3,302 walikutwa na maambukizi mapya” amesema Gidalya.
Kutokana na hali hiyo mkuu huyo wa wilaya amehimiza jamii kujitokeza mara kwa mara na kwa wingi katika vituo mbalimbali vya kutolea huduma za afya kwa ajili ya kupima dalili za ugonjwa huo kwani huduma ni bure.
Mganga mkuu wa mkoa Dkt. Boniphace Marwa amesema kuwa changamoto ambayo bado katika mkoa huo ni uwepo wa kiwango kikubwa cha maambuizi mapya ya wagonjwa wenye TB.
Amesema wameendelea kuweka nguvu kubwa katika suala la uhamasishaji wa jamii kupima, na wale ambao wamebainika wamewaanzishia dawa.