Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
IKIZINDUA msimu wa tano wa kampeni ya yake ya Benki ni SimBaking, Benki ya CRDB imetangaza kutenga zawadi kiasi cha shilingi milioni 240 pamoja na magari matano.
Akizindua kampeni hiyo, Mkurugenzi wa Wateja Wadogo na wa Kati wa Benki ya CRDB, Bonaventura Paul amesema kwa mwaka huu benki imejipanga kutoa magari manne aina ya Toyota IST na Toyota Harrier ‘New Model’ moja kwa wateja watakaoibuka kuwa vinara katika matumizi ya SimBanking katika kukamilisha miamala yao na huduma nyingine.
Bonaventura amesema azma ya Benki ya CRDB siku zote ni kuhakikisha inatoa huduma zinazokidhi mahitaji ya wateja wake na jamii ya Watanzania kwa ujumla hivyo itaendelea kuwekeza kwenye ubunifu wa kidijitali ili kukidhi mahitaji yaliyopo na yatakayojitokeza.
Katika kampeni ya mwaka huu ya SimBanking amesema kutakuwa na washindi wa kila siku na kila wiki watakaopata zawadi za fedha taslimu na gari aina ya Toyota IST na mshindi wa jumla ataondoka na Toyota Harrier.

“Tumetenga zaidi ya shilingi milion 240 zitakazotolewa kwa washindi wetu na kila baada ya miezi miwili tutatoa zawadi ya gari aina ya IST wakati mshindi wa jumla tutakayemtangaza mwishoni mwa mwaka atapata gari aina ya Toyota Harrier. Magari haya yote tutakayoyatoa kwa washindi wetu ni ‘New Model’ na yamekatiwa bima kubwa. Kwa wanafunzi wa vyuo, kuna simu za kisasa aina ya Iphone 16 zitakazokuwa zinatolewa kila baada ya miezi mitatu,” amesema Bonaventura.
Kwa miaka mitano ya kuendesha kampeni ya Benki ni SimBanking, amesema kumekuwa na mwitikio mkubwa ambao kwa sasa kwani kila mwezi takriban wateja milioni moja wanafanya miamala mingi kupitia programu hiyo inayowaruhusu kukamilisha malengo yao wakiwa mahali popote ndani ya saa 24.
Bonaventura amesema Benki ya CRDB inaamini katika kutoa huduma bora na za kisasa ili kuchangia maendeleo ya wateja wake na taifa hivyo kuhitaji kuwekeza katika ubunifu unaoendana na mabadiliko ya teknolojia duniani. Amesisitiza kuwa SimBanking ni kati ya huduma bora inayotambulika duniani kutokana na urahisi, usalama na uhakika wa kukamilisha miamala kidijitali.
“SimBanking ni kati ya huduma za Benki yetu ya CRDB ambazo zimeleta mapinduzi makubwa katika kuchochea ujumuishi wa huduma za fedha nchini. Kwa zaidi ya muongo mmoja sasa tangu kuanzishwa kwake mwaka 2011, SimBanking imetoa fursa kwa Watanzania wengi kujiunga na mfumo rasmi wa huduma za benki.