Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, ‘amewatoa jasho’ viongozi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) katika mkutano uliofanyika jijini Dodoma, Ijumaa iliyopita, JAMHURI limefahamishwa.

Waziri Simbachawene ametaka maelezo ya kina kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, Dk. Arnold Kihaule, ambapo taarifa kutoka ndani ya kikao hicho zinasema watendaji wa NIDA wameulizwa maswali magumu, ila nao wametoa majibu yanayohitaji uamuzi mgumu.

Wiki iliyopita JAMHURI limechapisha taarifa ikionyesha kuwa NIDA wameamua kununua mashine mpya mbili za kuchapa vitambulisho kutoka Ujerumani lakini kutokana na kupuuza ushauri wa wataalamu mashine hizo walizozinunua Euro 3,304,650 (karibu Sh bilioni 8), pamoja na kuwa na uwezo mkubwa wa kila moja kuchapa vitambulisho 9,000 kwa saa, haziwezi kufanya kazi kwa sasa.

Mkataba wa kununua mitambo hii miwili ulisainiwa Julai 22, mwaka jana. Mkataba umesajiliwa kwa Na. EA/061/2018-2019/HQ/G/01-LOT 3 wenye thamani ya kiasi hicho cha fedha.

“Mkurugenzi Mkuu wa NIDA [Dk. Kihaule] aligoma kusikiliza ushauri wa wataalamu, matokeo yake sasa tumegota. Taarifa hii [JAMHURI linaonyeshwa taarifa ya ‘kutisha’] wameiandaa pale NIDA, lakini wanatumia hadi mablanketi kuhakikisha Rais [John] Magufuli haimfikii. Mashine zimefungwa tangu Novemba, 2019, lakini zimeshindikana kufanya kazi.

“Mkurugenzi Mkuu wataalamu walimwambia kuwa kama tunanunua hizi mashine tunapaswa kununua na vifaa vyake, akakataa akasema zinunuliwe mashine vifaa vingine vitatumika hivi vinavyotumika katika mashine za zamani,” kimesema chanzo chetu.

Mashine hizo hazina vifaa vinavyohitajika: 1. HSM ambacho kina neno siri (passwords) za kuendeshea mashine hizo. 2. Compressor za kuendeshea mitambo hiyo; na 3. Servers kwa ajili ya kuhifadhi kumbukumbu za taarifa za Watanzania watakaotengenezewa vitambulisho.

Katika kikao kilichofanyika jijini Dodoma, inaelezwa kuwa uongozi wa NIDA umepangua tuhuma kadhaa, ukasema kwa hali yoyote hakuna namna, bali kuachana na mashine za zamani.

 “Kwa kweli walieleza kuwa kwa hali yoyote iwayo, teknolojia imebadilika na teknolojia tunayotumia katika vitambulisho vya taifa imepitwa na wakati kwani ni First Generation, wakati ipo Second Generation ambayo ndiyo mashine zilizonunuliwa na tayari kuna Third Generation,” kimesema chanzo chetu.

Inatajwa kwamba wamemweleza waziri kuwa vitambulisho vitakavyozalishwa na mashine hizi mpya zilizoletwa havitatumia teknolojia ya kuwa ‘laminated’, kwa maana ya kufunikwa na karatasi ya plastiki. Wamemwambia waziri kuwa hivi vipya vinavyotengenezwa hata vikitumbukia majini vinabaki salama.

JAMHURI limewasiliana na Waziri Simbachawene aliyesema: “Kuna mambo wamenieleza, nimewaambia haya bora wayaeleze wenyewe kwako [JAMHURI]. NIDA ni taasisi ya Watanzania, si mali ya mtu mmoja. Nimewaambia wayaeleze kwa ufasaha waeleweke kwenu na kwa Watanzania, ila hili la Compressor na Severs, nimewaambia wazi kuwa huu ni uzembe.

 “Lengo letu hapa ni kuhakikisha nchi yetu inakuwa salama. Nitahakikisha Watanzania wanapata vitambulisho kwa mifumo iliyo imara na kwa wakati, na hili jukumu limo mikononi mwa NIDA, ila mimi ninakuhakikishia nitawasimamia. Wewe wasiliana nao, nimewaambia wakupe majibu katika maswali yaliyoulizwa kupitia gazetini,” amesema Waziri Simbachawene.

Mtaalamu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (IT) aliyezungumza na JAMHURI amesema: “Kwa kweli nchi yetu inafanyiwa mchezo tu. Taarifa na kumbukumbu za wananchi hazihifadhiwi kwenye kadi, bali kwenye ‘chip’ iliyofunikwa ndani ya kitambulisho hiki. Kuiambia serikali kuwa kuna kizazi cha pili, cha tatu na nini sijui, ni kuhalalisha ulaji wa fedha za walipakodi. Hiki kitambulisho cha sasa mfumo wake hautapitwa na wakati hata miaka 100 ijayo. Kama yapo ya kuongeza kama utumiaji wa finger print [alama za vidole], hiyo wanayoita Third Generation ni kitu kidogo mno kisichohalalisha nchi kuingia gharama kubwa ya kubadili mfumo kabla ya kuutumia hata miaka 10.” Mfumo wa sasa wa vitambulisho ulianza kutumika mwaka 2012.

Kwa upande wake, Waziri Simbachawene amewabana watendaji hao kuwa hata kama teknolojia wanayotumia imepitwa na wakati, inakuwaje wamenunua mashine ambazo hazijakamilika?

“Amewaambia kwa mfano hicho kifaa cha HMS kinaweza kuwa kinasubiri vyombo vya usalama, sawa, lakini akawahoji hata compressor na severs zinasubiri nini? Hawakuwa na majibu… kwa kweli hakuwaficha baada ya hapo, akawaambia ni wazembe,” kimesema chanzo kingine.

Kwa vyovyote iwavyo, hatua ya kubadili teknolojia ya vitambulisho imetajwa kuwa italiongezea gharama kubwa taifa kwani itabidi kuuacha mfumo wa zamani; na kadi milioni 4.7 zilizopo itabidi ziharibiwe kama lilivyoandika gazeti hili wiki iliyopita. Hadi sasa NIDA ina akiba ya kadi za vitambulisho milioni 4.7 kwenye ghala. Baada ya wataalamu kufunga mitambo hii, walionyeshwa kadi zilizopo, wakasema mitambo hii haitumii kadi hizo.

Kadi hizi zimenunuliwa kati ya dola 2 na dola 2.5 au wastani wa Sh 5,000 kila kadi moja. Hii ina maana kuwa kadi milioni 4.7 zilizopo kwa kuwa hazitatumika kwenye mashine hizi mpya itabidi zitupwe. Ukizidisha kadi hizo mara Sh 5,000 serikali itakuwa imepata hasara ya Sh bilioni 23.5.

Hadi sasa NIDA wamesajili Watanzania milioni 21, na waliopata vitambulisho ni milioni 5.9 pekee; hivyo watu milioni 15.1 wanasubiri kuvipata. Kwa idadi hii, ikiwa hizi mashine mpya zitafanya kazi vizuri kwa saa 12 kila siku bila kupumzika, zinaweza kuchapisha wastani wa vitambulisho 200,000 kwa siku, hivyo kuchapa vitambulisho milioni 15.1 kwa siku 75, sawa na miezi miwili na nusu. Kwa mfumo huu mpya unaoelekea kukubalika.

Hata mfumo huo ukiachwa ukaletwa mfumo mpya, basi itabidi watu milioni 5.9 waliokwisha kutengenezewa vitambulisho vya taifa nao wabadilishiwe, kwani utakuwa mgogoro mkubwa kuwa na vitambulisho vyenye mifumo miwili katika nchi moja. ‘Mkoroganyo’ huu ndio umemsukuma Simbachawene awaite vigogo wa NIDA ofisini kwake jijini Dodoma.

Ikumbukwe suala la vitambulisho vya taifa lilizungumzwa tangu miaka ya mwanzo ya Uhuru na mchakato ulianza rasmi mwaka 2008. Kitambulisho cha kwanza kikatolewa Februari 8, 2013. Kabla ya hapo, kuanzia mwaka 2002 ulikuwapo mgogoro mkubwa wa aina ya software ya kutumika na kampuni ipi ipewe zabuni, suala lililochelewesha mchakato na sasa Mkurugenzi wa NIDA amerejesha mkanganyiko huo.

Kampuni ya IRIS Corporation Berhad ya nchini Malaysia iliyoanza kutengeneza vitambulisho mwaka 2012 ilifunga mashine tatu za kuchapa vitambulisho. Ufanisi wa mashine hizi ulikuwa ni kila mashine kuzalisha vitambulisho 5,000 kwa saa. Hata hivyo, mashine hizi hazikufanyiwa matengenezo (service) na zimepungua uwezo wa kuzalisha kutoka idadi hiyo kwa saa na kuwa vitambulisho 500 kwa siku.

Uchunguzi wa JAMHURI unaonyesha kuwa haikuwa kwa kusahau au kutofahamu umuhimu wa kuzifanyia matengenezo mashine hizi, bali wapo watu “waliopiga pasi ndefu” wakijua kuwa ufanisi wa mashine ukishuka, mzabuni hataongezewa muda wa kufanya kazi ya kuchapa vitambulisho, na kweli hili limetokea.

Tangu Machi 14, 2018 mkataba wa mkandarasi huyu ulipokwisha, NIDA inafahamu kwa nini iligoma kumwongezea mkataba angalau wa miezi 10 alioomba ili pamoja na mambo mengine, aweze kukarabati mashine hizo. Mashine moja imeacha kufanya kazi kabisa na mbili zilizosalia zina uwezo wa kuzalisha vitambulisho 1,000 kwa siku.

 “Ila uongozi wa NIDA umejenga hoja mbele ya waziri kuwa kwa mkataba wa zamani ingekuwa vigumu kutoa hata hizi namba kwa wananchi. Mkataba wanasema ulikuwa na masharti magumu, hivyo NIDA wameona kuuingia tena ilikuwa ni kuitia nchi kitanzini,” kimesema chanzo chetu.

Tuhuma za kunyanyasa wafanyakazi

JAMHURI limepata waraka ulioandaliwa na wafanyakazi wa NIDA ukionyesha madudu ya kutisha. Waraka huo unaonyesha kuwa uongozi wa NIDA unaongoza taasisi hiyo kwa mfumo wa nani anamjua nani, na si nani anajua nini.

JAMHURI limepata taarifa kuwa kuna baadhi ya wafanyakazi wanaolipwa wastani wa Sh 2,300,000 kwa siku [kwa mtumishi] wakipangiwa kazi, huku wengine wakifanya kazi usiku na mchana bila kulipwa hata senti tano. 

“Baada ya agizo la Mheshimiwa Rais kutaka wananchi wapewe namba hadi Januari 20, 2020, tumekuwa tukilazwa ofisini, lakini hatulipwi hata senti tano… kuna wafanyakazi ambao ni wanafamilia wao wanapeana fursa,” amesema mtumishi wa NIDA.

Mtumishi huyo (jina linahifadhiwa) ameliambia JAMHURI kuwa yupo mke wa kigogo ndani ya NIDA alitengeneza vitambulisho 10 kwa kutumia nywila (password) za baadhi ya wafanyakazi, na vitambulisho hivyo akawapatia hadi raia wa Kiarabu saba wasio Watanzania, lakini alipobainika hatua aliyochukuliwa ni kuhamishwa kituo cha kazi. “Alichofanya huyu mama ni uhujumu kwa nchi. Viongozi wamemlinda kwa kumhamisha kitengo tu.”

Wanasema uongozi wa juu wa NIDA na viongozi karibu wote waandamizi wanalindana kwa mfumo wa undugu, waliouita “Undugunaizesheni”, wakisema hata watu wasio na mamlaka ya kimuundo wanatoa maagizo kwa watumishi kuzalisha vitambulisho na kuwapa watu bila kufuata utaratibu ulioainishwa.

JAMHURI limewasiliana na Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, Dk. Kihaule saa chache kabla ya kwenda mitamboni juzi, aliyesema yuko nje ya ofisi na akaahidi kuwa angekutana na gazeti hili jana ofisini kwake kutoa majibu ya swali baada ya jingine. Majibu yake yatapatikana wiki ijayo.