Wakati tetesi za usajili zikizidi kushika kasi nchini katika klabu mbalimbali, uongozi wa Wekundu wa Msimbazi Simba Sports Club ya Dar es Salaam, umeonywa kuwa makini katika jambo hilo.
Simba inayohaha kushika angalau nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu Bara ili icheze Kombe la Shirikisho (CAF) mwakani, kuna taarifa kuwa ina ratiba ya kujaza mapengo.
Taarifa hizo zimewafikia baadhi ya wachezaji, wanachama ambao kwa nyakati tofauti wamemtaka Rais wa klabu hiyo, Evans Aveva, kuwa makini na kutorudia makosa ya kusajili wachezaji kwa sifa baadaye wanashindwa kuisaidia timu.
Mmoja wa wanachama hao, Hamisi Ng’ombo, mwenye kadi namba 02610, anasema kunahitajika umakini katika usajili ambako anapendekeza wachezaji waliopo wasiachwe.
“Mimi ninamshauri Rais wetu Aveva asisikilize maneno ya watu ambao wanampa ushauri mbovu, tusiivuruge tena timu kwa kusajili, bali tubaki na hawa wachezaji tulionao, tutawaacha wachezaji na baadaye tutajuta kama ilivyo kwa Amisi Tambwe,” anasema Ng’ombo na kuongeza:
“Kocha hakumpa nafasi ya kutosha Tambwe, akaonekana anashuka kiwango Simba, lakini leo amewapa ubingwa watani zetu Yanga. Haya ni makosa ya kuwasikiliza watu, uongozi ujaribu hata kumshauri kocha, tunao wachezaji wengi Simba ambao hawatumiki, naomba tusikimbilie kuwaacha tusije kujuta baadaye,” anashauri Ng’ombo.
Aveva hakupatikana kuzungumzia hilo, lakini Msemaji wa Simba, Haji Sunday Manara, anasema hivi sasa nguvu zao zote wanazielekeza katika mechi zilizosalia za Ligi Kuu, baada ya hapo ndipo watakapoangalia suala la usajili.
Alisema hawawezi kuzungumzia, au kujadili suala la usajili kabla Ligi kumalizika, ambako ikiisha watasikiliza kwanza mapendekezo ya benchi la ufundi na ndipo uongozi utatafakari kabla ya kulikabidhi jukumu hilo kwa Kamati ya Usajili.