Kipenga cha kuashiria kuanza kwa mashindano klabu bingwa barani Afrika kimepulizwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) huku ikuacha kitendawili kwa vilabu vya Tanzania kama vitauvunjwa mwiko wa kuondolewa kwenye mashindano hayo hatua za awali.
Wakizungumza na Gazeti la JAMHURI baada ya kutoka kwa ratiba ya mashindano hayo, makocha, wachezaji na watalamu wa soka wamesema bila kuwepo wa mipango madhubuti huenda matokeo yasiyoridhisha yakajirudia.
Katibu Mkuu wa klabu ya soka ya Mwadui ya Shinyanga Ramadhani Kilao amesema vilabu shiriki vinapaswa kujifunza kutokana na matokeo ya ushiriki wao wa miaka ya nyuma kimataifa.
“Kuna dhana ya vilabu vyetu kuishia katika hatua za awali katika mashindano ya kimataifa dhana tunayopaswa kuikataa kuanzia sasa” amesema Kilao.
Amesema dhana hiyo itaisha endapo washiriki wataingia katika mashindano wakiwa na mipango thabiti inayoakisi soka la sasa.
Amesema mojawapo ya mbinu zinazotumiwa na vilabu vikubwa kupata matokeo mazuri ni pamoja na maadalizi ya kisayansi kwa wachezaji na benchi la ufundi.
Kilao amesema ni lazima viongozi wakubali kujifunza hasa kutoka katika nchi zenye mafanikio katika mchezo wa mpira wa miguu Afrika hata Ulaya.
Kocha Mkuu wa Klabu ya Tanzania Prisons ya Mbeya, Abdallah Mohamed amesema soka ni mchezo unaohitaji maandalizi ya kisayansi.
“Wawakilishi wetu wanapaswa kuanza kujizatiti kwa kila namna kuwa tayari kutoa ushindani wa kweli na si kwenda kushiriki” ameshauri Abdalah.
Amesema uwepo wa vilabu imara nchini utasaidia uwepo wa timu ya Taifa imara, uimara huo huchangiwa na ushiriki wenye mafanikio wa vilabu kimataifa.
Amesema wadau wa mpira wanapaswa kutoa misaada ya hali na mali kuhakikisha ushiriki wa mafanikio wa vilabu na kuhakikisha vinafika mpaka hatua ya fainali.
Amesema kinachotakiwa ni uwepo wa maadalizi yenye tija kwa wachezaji na benchi zima la ufundi kuelekea katika mashindano haya yenye utajiri mkuwa ngazi ya vilabu Afrika.
Mchezaji wa zamani wa klabu ya Yanga na timu ya taifa, Sekilojo Chambua, amesema hakuna njia ya mkato katika kufikia mafanikio yoyote katika mashindano.
Amesema viongozi wa vilabu kwa kushirikiana na mamlaka husika wanapaswa ushiriki wenye tija kwa vilabu hivi.
“Wahakikishe vijana wanapewa maandalizi ya kisaikolojia na wajue kuwa wanaenda kukutana na wachezaji wenye viwango vya hali ya juu vya kimataifa”amesema Chambua.
Mkurugenzi wa ufundi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) Salumu Madadi, amesema TFF ipo tayari wakati wowote kutoa ushirikiano wa kiufundi kwa vilabu vyote.
“Milango iko wazi kwa klabu yoyote inayohitaji ushauri wowote wa kitaalamu iwe inashiriki mashindano ya kimataifa au ya ndani ” amesema Madadi.
Amesema huwezi kupata mafanikio bila ya uwepo wa maandalizi ya kutosha ya kiufundi katika mchezo wowote ule duniani.
“Suala la maandalizi lipo kokote kule ndio maana hata vilabu vikubwa duniani kama Manchester United, Barcelona huenda mechi za majaribio kabla ya msimu kuanza,”amesema Madadi.
Katika mashinadano hayo klabu ya Yanga itachuana na klabu ya St Louis ya Shelisheli huku Simba itakayoshiriki Kombe la Shirikisho ikipangwa kuanza na Gendamerie National ya nchini Djibouti.