DODOMA

Na Mwandishi Wetu

Dakika 90 za pambano la Ngao ya Jamii kati ya Simba na Yanga la Septemba 25, mwaka huu halikuishia Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam kama ilivyodhaniwa.

Pambano hilo lilihitimishwa kwa aina yake siku iliyofuata, Jumapili ya Septemba 26, 2021 kwa kuhamishiwa kwenye Kanisa Kuu la Anglikana jijini Dodoma.

Katika pambano la Uwanja wa Mkapa, Simba walifungwa bao 1-0; jitihada zikabaki kwa mashabiki wa timu hiyo kulipa kisasi kanisani, lakini bado wakaangukia pua pale waliposhindanishwa kwenye Changizo la Sadaka ya Mavuno.

Aliyelihamishia pambano la Simba na Yanga kanisani mwishoni mwa ibada ya matoleo ya Sadaka ya Mavuno, akihoji ni nani zaidi kati ya timu hizo kongwe, ni Mchungaji Kenneth Chimwaga.

Wakati akina baba na akina mama wa Anglikana wakitoa sadaka, Mchungaji Chimwaga alichombeza akitaka: “Sasa yatenganishwe mavuno yatakayotolewa na Mnyama (Simba) na ya Wananchi (Yanga) kwa waliomo leo kanisani humu.”

Awali, Mchungaji Chimwaga aliwahoji waamini waliokuwamo kanisani akihoji: “Nichomekee – nisichomekee?” Na akajibiwa: “Chomekea!”

Kwa ruhusa hiyo, mchungaji akaagiza kupelekwa mbele ya madhabahu vyombo viwili: “Kushoto kwangu kuwe na kikapu cha sadaka ya Mnyama; kulia kwangu kiwekwe kile cha Wananchi, tuone nani atashinda kwa kumtolea Mungu.”

Vikapu viwili vilipowekwa wapenzi wa pande hizo mbili wakiwa wamevishikilia, watu walianza kutoa sadaka; kila mmoja katika kikapu cha timu anayoishabikia.

Sadaka ikakamilika. Pambano likaisha, yakabaki yanasubiriwa matokeo. Fedha zikahesabiwa zikijumuisha ibada zote tatu tangu ile ya saa 12 asubuhi.

Katika kila ibada, Yanga walikuwa wakiongoza kwa wastani wa Sh 50,000!

Jumla ya Sh 300,000 zilikusanywa kama sadaka ya mavuno kutoka kwa mashabiki wa Simba na Yanga ndani ya Kanisa la Anglikana, Dodoma, na Yanga kuibuka washindi.

Mashabiki hao kila baada ya ibada walionekana wakipeana mikono kupongezana huku wakisifu ubunifu wa Mchungaji Chimwaga kukusanya sadaka kanisani kwa kutumia mambo ya kijamii.

Katika mnyukano halisi kati ya Simba na Yanga uwanjani, mchezo wa kufungua pazia la Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga walishinda Ngao ya Jamii kwa kuwatandika watani wao Simba bao 1-0 katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa. 

Bao pekee la Yanga lilifungwa na Fiston Mayele katika dakika ya 12 ya mchezo.