‘Uzalendo umetushinda, uzalendo umetushinda’, hayo yalikuwa ni maneno yaliyosikika yakiimbwa na mashabiki wa Yanga mwaka 1993 baada ya Simba kufungwa na Stella Abidjan katika mechi ya fainali ya Kombe la CAF (sasa Kombe la Shirikisho).
Stella Abidjan walishinda magoli 2-0 na Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, akawakabidhi kombe wakaondoka nalo.
Baadhi ya mashabiki wa Simba, akiwamo Prof. Philemon Sarungi, walilia hadharani. Ilikuwa ni jioni ya uchungu mkubwa kwa kila Mwana Simba.
Wakati Simba wakitafuta mchawi, Yanga walifarijika wakiona ni afadhali kombe hilo limekwenda Ivory Coast. Waliamini iwapo Simba ingeibuka mshindi katika fainali hiyo, basi huko mitaani ‘kusingekalika’ kwa vijembe kutoka kwa watani wao hao wa jadi.
Umekuwa ni utamaduni kwa Yanga na Simba kuombeana mabaya, imekuwa ni tabia ya kipuuzi ambayo mashabiki hawaoni kuwa inachangia katika kuyadumaza mafanikio ya klabu zetu katika anga za kimataifa.
Simba ilipokuwa ikikabiliwa na mechi ya kimataifa dhidi ya TP Mazembe, mashabiki wa Yanga kwa kipindi cha wiki nzima walikuwa wakiziulizia jezi za timu hiyo ya DRC, lengo ni kuwaunga mkono uwanjani ili Simba itolewe nje ya michuano na wakosaji wawili wabakie kuzifikiria mechi za ligi kuu peke yake.
Walifanikisha lengo lao, Simba wakatolewa, lakini maisha ya tukose wote hayakutusaidia. Yanga iliposhindwa kuitoa Al Ahly nje ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, baada ya Said Bahanuzi kukosa penalti ambayo ingeivusha timu, mashabiki wa Simba wakaingia gharama ya kutengeneza jezi zilizoandikwa ‘ASANTE BAHANUZI’.
Kwa Simba kuiona Yanga ikishindwa kuvuka kule Misri, ilikuwa ni ahueni, lilikuwa ni jambo la furaha, waliona ni afadhali Bahanuzi amekosa penalti, hivyo kuwapunguzia mzigo wa vijembe kutoka kwa mashabiki wa Yanga.
Tukose wote haiwezi kuishia kwenye kukosa wote peke yake, inaambatana na nchi kuonekana ni duni kwa wale wanaoziangalia takwimu za soka la Afrika. Yanga na Simba wanapoombeana dua mbaya, ni hasara kwao na hasa kwa wachezaji ambao mara nyingi huwa ndio asilimia sabini au themanini ya wachezaji wa Taifa Stars.
Ugomvi wetu unaotokana na msukumo wa kishabiki, ni neema kwa wanasoka wa kigeni wenye uwezo wa kawaida sana, vita ya panzi, furaha ya kunguru.
Yanga wanamtangaza kwenye magazeti mchezaji wao wa kigeni kwa wiki nzima, ili mradi tu Simba wawe wanyonge na Simba nao wakishampata mchezaji wa kawaida huko nje, wakishamleta na akaanza kufanya mazoezi kabla ya kipindi cha usajili, magazeti yote yanampamba kumbe ni mchezaji mbovu tu.
Yote haya yanafanywa na timu ambazo zinaongozwa na akili zisizobadilika, ambazo haziwezi kujifunza la maana wakati timu zikipata mechi za kimataifa huko nje. Huwa ninaupenda sana ushabiki wa Waingereza, wao watataniana siku timu mbili zikicheza, baada ya hapo wanatakiana yaliyo mema pekee.
Mashabiki wa timu moja ya Uingereza, wakiona timu yao inaongoza magoli mengi na mpinzani hana uwezo wa kujibu mapigo, wataanza kuimba nyimbo za kumsifu mfungaji wao au kocha wao na wakati huo huo watamtania kocha wa timu inayofungwa kwa kumwambia kuwa ajira yake ndiyo imefikia tamati.
Utani wao unawekwa pembeni wakati mmojawapo ya timu yao inashiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya au ile ya Europa, wote wanapokabiliana na adui wa nje hugeuka marafiki wenye kuzipenda timu zao.
Tukose wote si sehemu ya utamaduni wa ushabiki wa Waingereza, anayeiwakilisha nchi anaungwa mkono na kila Mwingereza, kwani mafanikio ya timu moja yanao uhusiano na timu nyingine ya Uingereza.
Wanaanza kufukuzana
Acha tu kwenye ushabiki, hata ndani ya uongozi klabu hizi ni kama pacha. Wakati Simba imemleta Sven van der Broeck kuwa mbadala wa Patrick Aussems, Yanga ni kama waliwaiga kwa kumleta Luc Eymael.
Kiwango cha chini kinachoonyeshwa na wachezaji wa Simba kwa sasa hakiwaridhishi mabosi na kuna madai kuwa hakuna maelewano ndani ya benchi la ufundi.
Kwa sasa anasubiriwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Mohammed ‘MO’ Dewji ili kuweka kikao kwa lengo la kuweka mambo sawa.
Yanga nako kuna wengine wana maswali kibao, ‘eti kocha kaletwa bila sisi kuambiwa’, huu ni unafiki.
Sven van der Broeck
“Nataka kupiga kazi na tutoke hapa tulipo, Tanzania kuna vipaji vingi, ila maswali pia yapo mengi, muhimu ni kusonga na kuipa faida klabu.”
Luc Eymaeel
“Ninachotaka ni kufanikisha lengo lililonileta, nataka kuiona Yanga bora itakayozalisha timu ya taifa bora, ninawaza zaidi kwa nchi hii kupata fursa ya kucheza AFCON, hayo mengine ni mapito.”
Mwina Kaduguda
“Hakuna mgogoro ndani ya Simba, kila kitu kipo sawa, wachezaji wapo sawa, benchi la ufundi lipo sawa na ninachoona kuna watu watazidi kutoa machozi kwa mafanikio ya klabu yetu.”
Dk. Mshindo Msolla
“Malengo yetu lazima yatimie na tulichoamua kitafanikiwa tu. Tutatoka hapa tulipo na tuna imani kubwa na kocha wetu.”
Ushauri wa bure
Ni unafiki wa wazi kabisa. Anayekuwa tayari kuihujumu klabu ya nchi aliyozaliwa kwani hawezi kuihujumu timu ya taifa?