Wakati mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara ulimalizika Jumapili iliyopita, kipa namba moja wa klabu ya Simba na timu ya taifa (Taifa Stars), Juma Kaseja, amehitimisha ngwe hiyo kwa huzuni, mashaka na wasiwasi mkubwa kutokana na kutukanwa, lawama na vurugu alizofanyiwa kuanzia Morogoro hadi jijini Dar es Salaam.

Chanzo cha yote hayo ni kitendo cha Simba kufungwa mabao 2-0 katika mechi yake ya 12 ilipocheza na Mtibwa Sugar ya Turiani kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro, huku mabao hayo yakidaiwa kusababishwa na uzembe wa kipa huyo.


Pamoja na kulia hadharani baada ya mwamuzi wa mechi hiyo kupuliza kipenga cha mwisho siku hiyo, kuichana jezi yake na kuitupa uwanjani, mashabiki wa Simba waliokuwapo hapo walipanga kumchapa makonde, lakini akapewa ulinzi mkali na Jeshi la Polisi na hivyo kunusurika. Kaseja aliyejiunga Simba tangu mwaka 2001 akitokea timu ya Reli ya Morogoro iliyokuwa ikishiriki pia Ligi Kuu wakati huo, kuhamia timu ya Yanga kwa msimu wa 2010/2011 kabla ya kurudi na kuendelea kuichezea tena timu hiyo, alinusurika kupata mkong’oto pia alipofika Kibaha wakati timu hiyo ikirejea Dar es Salaam.

 

Mashabiki hao walitaka kuliteka basi lililowachukua wachezaji na viongozi waliokwenda Morogoro, waliposhindwa wakaishia kumtukana matusi ya nguoni wakidai alifungwa kwa makusudi na kumtaka arudi tena Yanga.

 

Kesho yake, Jumatatu ya wiki iliyopita, mashabiki wengine waliandamana hadi Makao Makuu ya Klabu hiyo jijini Dar es Salaam huku wamebeba mabango, yakimtaka kipa huyo pamoja na Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage na Makamu wake, Geofrey Nyange ‘Kaburu’, waondoke katika klabu hiyo.


Tayari Kaseja ambaye pia ndiye nahodha wa timu hiyo ameuomba uongozi apumzike kwanza kuichezea hadi hapo baadaye, hatua iliyokuja huku zikiwepo taarifa mpya zinazodai kwamba amepanga kuachana nayo moja kwa moja kulinda heshima na hata maisha yake.

 

Habari zaidi zinaeleza kuwa alichopanga hasa ni kutotaka kusajiliwa kabisa na Simba msimu ujao, hivyo tayari ameshaanza kuwaaga wachezaji wenzake.


Mbali na kufungwa na Mtibwa Sugar, mashabiki wa Simba pia wanamtuhumu Kaseja kuwa amechangia kwa kiwango kikubwa timu yao isifanye vizuri ilipotoka sare mfululizo katika mechi zake tano ilizocheza dhidi ya Yanga, Coastal Union, JKT Mgambo, Kagera Sugar na Polisi Morogoro.


Kabla ya kuteremka dimbani kucheza mechi yake ya mwisho ya mzunguko huo wa kwanza, Jumamosi iliyopita kwa kukwaana na timu ya Toto African, Simba ilitoka kifua mbele uwanjani baada ya kuikung’uta Azam FC mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, lakini siku chache baadaye nayo ikachapwa na Mtibwa Sugar mabao 2-0 na kuwa janga kubwa kwa Kaseja.

 

Tayari ametetewa na uongozi wa timu hiyo, Shirikisho la Kandanda Tanzania (TFF) na wadau wengine wakisema kusuasua kwa timu hiyo tangu ilipokosa ushindi kwa Yanga huku ikionekana kubebwa na mwamuzi uwanjani, hakutokani na udhaifu wala hujuma zozote zilizofanywa na kipa huyo.


Mathalani, mashabiki wanaomtuhumu hivyo, wametakiwa wajiulize ni uhusiano gani uliopo kati ya Kaseja na timu hiyo kutoka sare mfululizo katika mechi zake dhidi ya Yanga, Coastal Union, JKT Mgambo, Kagera Sugar na Polisi Morogoro.

 

Badala ya kumshutumu katika hali yoyote, mashabiki hao mahali popote walipo, wanapaswa wampongeze kwa kulilinda vizuri lango lake na kuinusuru Simba isipoteze mechi hizo tano ambazo badala yake ingenyang’anywa pointi nyingi.

 

Kwanini wasiwashutumu viungo na washambuliaji wa timu hiyo kwa kushindwa kupachika mabao na kuipa ushindi timu yao dhidi ya Yanga, Coastal Union, JKT Mgambo, Kagera Sugar, Polisi Morogoro na Mtibwa Sugar iliyoinyang’anya kabisa pointi zote zilipocheza na kufungwa na kuleta kasheshe?


Kwanini hawawanyoshei kidole cha lawama akina Emmanuel Okwi, Felix Sunzu, Mrisho Ngassa, Daniel Akuffo, Edward Christopher, Amri Kiemba, Mwinyi Kazimoto na wengineo kwa kushindwa kupachika mabao kuipa ushindi Simba?


Kazi ya kipa uwanjani inakuwa nyepesi kutegemea uimara wa beki yake, vinginevyo hata kama Simba itawasajili makipa bora zaidi duniani kama Iker Casilas wa Real Madrid ya Hispani au Joe Hart wa Manchester City ya England, kutoka sare ama kufungwa kutakuwa palepale na vilevile iwapo safu nzima ya ulinzi, kiungo na ushambuliaji zitakuwa siyo lolote wala chochote dimbani.


Ndiyo maana ni vigumu kujua kama mashabiki hao wa Simba wanataka Kaseja adake na wakati huo huo acheze akiwa kiungo au mshambuliaji ili azitumie nafasi hizo pia, kupachika mabao na kuipa ushindi timu yake.


Simba wakumbuke kuna aina tatu ya matokeo ya mashindano; kushinda, kushindwa na au kutoa sare au suluhu (kutofungana).