Mna uhakika kwamba kocha Roberto Oliviera ataweza kufanya vizuri akiwa pamoja na Juma Mgunda na Selemani Matola au mnasubiri mambo yaharibike mumshushie lawama Selamani Matola?
Sisemi kwamba Robertinho hatafanya vizuri lakini ikiwa atapata matokeo mabaya hata mechi moja kwa sababu ya mbinu zake lawama zote zitakwenda kwa Matola na Mgunda kwamba wananuhujumu kocha huyo toka Brazil.
Robertinho katika moja ya mapendekezo yake aliomba aje na kocha msaidizi wake lakini pendekezo hilo halikukubaliwa na ndilo lilichelewesha sana deal ya mbrazil huyo kujiunga na wanamsimbazi hao. Pendekezo lake halikukubaliwa na ametua klabuni amemkuta mtangulizi wake Juma Mgunda ambaye amefanya vizuri sana na Simba.
Kitu muhimu Simba ifanye vizuri lakini Simba ikifanya vibaya atatafutwa mchawi kwa gharama yeyote ile kwa sababu kutakuwa kuna kundi la wachezaji wanaomhusudu Mgunda huku wengine wakiwa ni wafuasi wa Matola na baadhi watakuwa wafuasi wa kocha mpya.
Robertinho atakuja na hoja ya kukosa wasaidizi sahihi anaowataka yeye. Changamoto ngumu kwa mbrazil huyo ni mafanikio makubwa aliyoyapata Mgunda toka alipopewa timu mpaka ujio wa kocha mpya. Mazuri ya Robertinho yatasifiwa lakini matokeo mabaya yatawafanya Simba wakumbuke zama za Mgunda.
Tumezoea kocha akiachia timu baada ya matokeo mabaya lakini Mgunda ameiacha Simba akiwa amepoteza mechi moja pekee huku akiwa amerejesha morali ya timu ambayo amefanikiwa kuifikisha Simba hatua ya makundi ya Klabu Bingwa Afrika. Mgunda ‘hana baya’.
Katika mazingira ya Mgunda Hana baya ipo hatari ya kuwa kama kipimo cha Robertinho na hivyo akipoteza hata mechi moja inaweza kuleta kelele kubwa sana kwa sababu watu wanatarajia makubwa zaidi ya yale ya Mgunda jambo ambalo litamtesa Robertinho.