Na Isri Mohamed,JamhuriMedia, Dar es

Klabu ya soka ya Simba jana Januari 21,2024  imefanya mkutano wake mkuu wa kujadili katiba yao, kutoa mrejesho wa mapato na matumizi ya klabu kwa mwaka 2023, sambamba na makadirio kwa mwaka 2024.

katika mkutano huo uliofanyika kwenye ukumbi wa Mwalimu Nyerere jijini Dar, mwenyekiti wa Simba, Murtaza Mangungu amezungumza na wanachama kuhusiana na namna ya kuikosoa klabu pale inapotokea makosa ya wazi, lakini kubwa zaidi akatoa mrejesho wa fedha zilizochangwa mahsusi kwa ajili ya ujenzi wa uwanja.

“Lengo letu ni kujenga umoja. Mfano mtu anasema uwekezaji hauna faida wakati kabla ya uwekezaji mapato yalikuwa Tsh. 1.6 bilioni, mara baada ya uwekezaji yamepanda hadi Tsh. 6.9 bilioni. Afrika tulikuwa nafasi zaidi ya 80 kwenye ubora na sasa tupo nafasi ya saba. Tunataka ukosoaji wenye tija.



“Kama mnakumbuka mlichanga pesa kwa ajili ya ujenzi wa uwanja na pesa ile ilitumika kujenga ukuta wa uwanja wa Bunju na pesa zingine zilitumika kuimarisha kambi ya timu” amesema Mangungu

Kauli ya ujenzi wa ukuta badala ya uwanja imeonekana kuzua gumzo kwa wanachama wakihoji jumla ya fedha zilizochangishwa ni kiasi gani na kwanini zimebadilishiwa malengo bila ya wao kushirikishwa?

Aidha mwenyekiti Mangungu ameweka wazi kuwa viongozi wapo tayari kupokea maoni ya wanachama wao yenye lengo la kuboresha taasisi yao.

“Simba imeshafanya mambo mengi makubwa, yaliyopita, yanayofanyika sasa na mengine yanakuja.”

“Sisi mliotupa dhamana tupo tayari kupokea maoni ambayo yataipeleka Simba mbele.”