Dakika 90 kati ya 180 za mchezo wa robo fainali ya Kombe la Klabu Bingwa barani Afrika baina ya Simba SC na TP Mazembe zimekamilika katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kwa miamba hao kutoka suluhu.
Klabu ya Simba imekuwa ikiheshimika huko nje kwa kutumia vema uwanja wake wa nyumbani, hasa ikikumbukwa kwamba ilipata matokeo chanya dhidi ya Nkana FC, Mbabane Swallows, JS Saoura, Al Ahly pamoja na AS Vita.
Katika mechi zote hizo, wapinzani wa Simba SC walilala katika Uwanja wa Taifa na kuifanya Simba SC kuogopwa. TP Mazembe walionekana kucheza kwa tahadhari kubwa huku wakizuia kushambuliwa na kuruhusu goli.
Simba bado wanayo nafasi ya kusonga mbele endapo watalazimisha sare ya namna yoyote ile na TP Mazembe, mabingwa mara tano wa mashindano hayo yenye hadhi kubwa katika ngazi ya klabu barani Afrika.
Timu ya Simba ilitengeneza nafasi kadhaa ambazo zingeiwezesha kushinda mechi hiyo, lakini safu yake ya ushambuliaji ilikosa ubunifu mbele ya mabeki wa TP Mazembe ambao lengo lao lilikuwa kutoruhusu wavu wao kuguswa.
Bahati haikuwa upande wa Simba SC, maana hata baada ya mwamuzi kutoka nchini Algeria kuizawadia Simba mkwaju wa penalti, nahodha John Bocco alishindwa kuibeba timu yake baada ya kukosa penalti katika dakika ya 59 ya mchezo. Dakika chache baadaye, Meddie Kagere, alipiga ‘tik-tak’ akiwa ndani ya eneo la hatari, lakini mpira wake haukuleta madhara.
Mazembe inakuwa timu ya kwanza kutokufungwa na Simba katika Uwanja wa Taifa katika mashindano ya klabu bingwa. Simba imezifunga timu nyingi katika Uwanja wa Taifa – Mbabane Swallows, Nkana Red Devils, JS Saoura, Al Ahly na AS Vita.
Kocha wa Simba, Patrick Aussems, ana kibarua kizito kuhakikisha walau anapata sare yoyote nchini DR Congo katika Uwanja wa Stade TP Mazembe, jijini Lubumbashi, Jumamosi wiki hii.
Uzoefu wa TP Mazembe kwenye mashindano hayo umewabeba, maana kikosi hicho kilionekana kutulia na kucheza kwa kutafuta suluhu tu, hiyo ikimaamisha kwamba kuna namna ambavyo watajihakikishia ushindi jijini Lubumbashi.
Timu zote zilitengeneza nafasi nyingi, hasa timu ya Simba, lakini washambuliaji wake walikosa utulivu, huku walinzi wa TP Mazembe wakiwa na nidhamu ya ukabaji ya hali ya juu, wakiongozwa na Koffi Christian.
Hawakushambulia muda mwingi, lakini jinsi walivyokuwa wanacheza unagundua wapinzani walikuja kucheza ili wasipoteze mchezo wao.
Ukongwe wa Tresor Mputu haukumzuia kushindwa kuifanya timu yake itawale sehemu ya kiungo, alichuana kisawasawa na wadogo zake kina Jonas Mkude na James Kotei.
Kocha wa TP Mazembe, Pamphile Mihayo, aliyewahi kuichezea TP Mazembe, ni kocha kijana ambaye ameleta morali kubwa kwenye timu hiyo.
Mihayo ameleta utulivu mkubwa kwenye timu yake. Sambamba na hayo yote, Mazembe waliweza kuutumia uwanja wao wa nyumbani vema dhidi ya Club Africain, baada ya kuwalaza magoli 8-0.
TP Mazembe ni klabu yenye mafanikio makubwa barani Afrika kutokana na uwekazaji mkubwa unaofanywa na bilionea, Moise Katumbi, na imefanikiwa kutwaa taji la klabu bingwa mara tano.
Mwaka 2010, ilishika nafasi ya pili katika fainali za klabu bingwa duniani, baada ya kulazwa magoli 3-0 dhidi ya timu ya Inter Milan.
Kwingineko, katika mashindano hayo timu ya Mamelod Sundowns wamewaadhibu Waarabu – Al Ahly kwa mabao 5-0, katika mchezo wa robo fainali, mzunguko wa kwanza. Mchezo huo wa kwanza umepigwa jijini Johannesburg, Afrika Kusini.