SIMBA imeendelea kuthibitisha ni somo katika michuano ya kimaaifa baada ya leo kuifunga CS Constantine ya Algeria mabao 2-0 mchezo wa Kombe la Shirikisho Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Matokeo hayo yameifanya Simba ambayo tayari ilishafuzu robo fainali, imalize mechi za makundi ikiwa kinara wa Kundi A kwa pointi 13, ikifuatiwa na CS Constantine yenye pointi 12, Bravos yenye pointi 7 na CS Sfaxien yenye pointi tatu ilizopata leo baada ya kuifunga Bravos mabao 4-0. CS Constantine pia imefuzu robo fainali.

Mabao ya Simba yote yamepatikana kipindi cha pili wafungaji wakiwa Kibu Dennis na Leonel Ateba na kuibua shangwe kwa mashabiki wa timu hiyo, ambayo ndiyo mwakilishi pekee wa Tanzania aliyebaki katika michuano ya ngazi ya klabu inayoandaliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).

Mwaka huu Tanzania iliingiza timu sita katika michuano inayoandaliwa na CAF kwa klabu, ambapo tatu zilikuwa Ligi ya Mabingwa Afrika na tatu Kombe la Shirikisho (CAF).