Na Tatu Saad,JAMHURI MEDIA

Kikosi cha klabu wa wekundu wa msimbazi ‘Simba SC’ kinatarajia kuondoka mchana wa leo kuelekea nchini Morocco, kwa akili ya mchezo wa mwisho wa kundi C LIGI ya Mabingwa Afrika dhidi ya Raja Casablanca.

Meneja wa Habari na Mwasiliano wa Simba SC Ahmed Ally amesema mipango na maandalizi ya safari kwa baadhi ya Wachezaji wao imeshakamilika, huku wengine walioitwa katika timu za taifa wakitarajiwa kujiunga na timu baadae.

Kikosi chetu kinatarajiwa kuondoka Dar es salaam kuelekea Morocco saa tisa alasiri leo Jumanne kupitia Doha-Qatar, na kitafika Casablanca kesho Jumatano” Amesema Ahmed Ally

Ahmed amesema msafara wao Una wachezaji 22 lakini watakaondoka leo ni wachezaji 13 tu huku wengine watajiunga nao nchini Morocco moja kwa moja mara tu baada ya kumaliza majukumu yao ya Kitaifa.

“Msafara wetu utakuwa na wachezaji 22, lakini wanaoondoka leo ni wachezaji 13, huku wengine walioitwa kwenye timu zao za taifa wakitarajiwa kujiunga na timu moja kwa moja nchini Morocco baada ya kumaliza majukumu ya Kimataifa.” Amesema Ahmed Ally

Katika mchezo wa kwanza uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam mwezi Februari, Simba SC ilikubali kupoteza mbele ya Raja Casablanca kwa kufungwa 3-0.

Simba SC itacheza mchezo huo Jumamosi (April Mosi), ikiwa tayari imeshajihakikishia nafasi ya kucheza Robo Fainali ikikusanya alama 09 katika michezo mitano iliyocheza, ikitanguliwa na wenyeji wake Raja Casablanca wanaoongoza msimamo wa Kundi C, wakiwa na alama 13.