Ni shangwe kila kona ya nchi, mabingwa wa soka wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2017/2018, Simba SC imetoa zawadi ya Sikukuu ya Mapinduzi kwa Watanzania.
Simba imeiadhiri JS Saoura ya Algeria katika mashindano ya Klabu Bingwa barani Afrika baada ya kuibuka na ushindi wa magoli 3-0, mchezo huo umefanyika katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Mabao ya Simba yalifungwa na Emmanuel Okwi katika dakika ya 46, huku goli la pili pamoja na la tatu yakifungwa na Meddie Kagere, katika dakika ya 52 na 67. Kagere aliingia baada ya kuumia kwa nahodha John Bocco.
Katika mchezo huo kipindi cha kwanza kilianza kwa timu zote kusomana huku JS Saoura ikitumia winga za kushoto na kulia kupandisha mashambulizi, ambayo hata hivyo yalidhibitiwa vema na mabeki wa Simba SC.
Dakika ya 30 ya mchezo Simba SC ilianza kulishambulia kwa kasi lango la JS Saoura huku kipa Khaled Boukacem, akiwa na kazi ngumu ya kuzuia michomo ya Okwi.
Lakini muda mfupi baada ya John Bocco kuumia na kushindwa kuendelea na mchezo huo, Kagere aliingia na kuleta mabadiliko katika lango la JS Saoura na kusababisha kupata goli baada ya Clatous Chama kumtengenezea pasi ya goli Okwi.
Simba ilibadilika baada ya kuanza kwa kipindi cha pili ambapo walianza kushambulia lango la wapinzani wao kwa kasi hadi kusababisha kupata goli la pili na la tatu huku wapinzani wao wakionekana kuzidiwa idara zote.
Katika mchezo huo, Juuko Murshid, alicheza vizuri licha ya wadau wengi wa soka kutokuwa na imani naye baada ya Erasto Nyoni kukosa mchezo huo kutokana na kuwa majeruhi.
Simba SC wameweza kuutumia vema uwanja wa nyumbani, kwani hata mechi dhidi ya Nkana na Mbabane Swallows walishinda.
Baada ya kumalizika mchezo huo, Kocha Mkuu wa Klabu ya Simba, Patrick Aussems, aliwaambia waandishi wa habari: “Kwanza nimpongeze golikipa Aishi Manula na wachezaji wote kwa kucheza vizuri na kujipanga kwa mechi inayokuja.’’
Naye nahodha wa Simba SC, John Bocco, anasema: “Mchezo ulikuwa mzuri, naomba niwapongeze wachezaji wenzangu kwa kuibuka na ushindi na ushirikiano mzuri kutoka kwa mashabiki.”
Wakati kocha wa Simba na nahodha wake wakifurahia namna wachezaji walivyojipanga na kucheza ili kupata matokeo chanya, Kocha wa JS Saoura, Nabil Neghiz, aliwatuhumu wanahabari wa Tanzania kwa kuidharau timu hiyo.
Ikumbukwe mechi inayofuata Simba itacheza na Klabu ya AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) katika Uwanja wa Stade des Martyrs, Jumamosi ya wiki hii.
Simba imedhihirisha kuwa ina uwezo wa kucheza na kila timu, kwani iliweza kumiliki mchezo na kupiga pasi fupi fupi na kucheza soka la kisasa, hali iliyowapagawisha mashabiki waliojitokeza katika Uwanja wa Taifa.
Kimsingi Kocha wa Simba, Aussems, anatakiwa kuendelea kuwajengea wachezaji hali ya kujiamini zaidi ili kuhakikisha hata wanapocheza nje ya uwanja wa nyumbani waweze kupata ushindi.
Kihistoria mara ya mwisho Simba SC kufika katika hatua ya makundi ni mwaka 2003, ambapo iliweza kushika nafasi ya tatu; haikuweza kufuzu katika hatua ya robo fainali, huku Enyimba na Ismailia zikifuzu kucheza hatua ya robo fainali na wakakutana fainali, ambapo Enyimba ilikuwa bingwa wa Kombe la Klabu Bingwa barani Afrika msimu huo.