NI rasmi Aprili 20, 2024 Yanga SC watakuwa wenyeji wa watani zao Simba SC katika muendelezo wa kinyang’anyira cha Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2023-24.
Taarifa iliyotolewa leo na Idara ya Habari na Mawasiliano ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imesema awali mchezo huo namba 180 maarufu kama ‘Kariakoo Derby’ haukupangiwa tarehe kwenye ratiba ya maboresho lakini sasa ni wazi utapigwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam saa 11:00 jioni.
“Klabu za Yanga na Simba pamoja na wadau wengine wa Ligi Kuu ya NBC wamepatiwa taarifa zote kuhusiana na mchezo huo na maandalizi yake yanaanza mara moja ili kuhakikisha unafanyika katika kiwango cha juu
kinachoendana na hadhi ya michezo mikubwa ya Ligi ya sita kwa ubora barani Afrika,” imefafanua taarifa hiyo.
TPLB haikutaja sababu za mchezo huo kutopangiwa tarehe hapo awali, lakini duru zinaeleza, lengo lilikuwa kuepusha muingiliano wa ratiba za michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAFCL) ambapo timu hizi zimetolewa siku chache nyuma katika hatua ya robo fainali.
Mnyama Simba anaingia katika mchezo huo akiwa na kumbukumbu mbaya ya kukubali kipigo cha 1-5 dhidi ya watani zao Yanga, Novemba 05, 2023 Uwanja wa Benjamin Mkapa.