Mbunge wa jimbo la Babati Vijijini Mheshimiwa Daniel Sillo, amesema ndani ya kipindi cha miaka miwili akiwa madarakani yapo mambo mengi ambayo yamefanywa na serikali katika jimbo hilo na bado mipango inaendelea.

Mheshimiwa Sillo ambaye pia ni mwenyikiti wa kamati ya kudumu ya Bunge la Bajeti amezungumza hayo alipofanya ziara katika vijiji vya Merr kata ya Qameyu na Erri kata ya Kiru agosti 25,2022 akifikisha idadi ya vijiji 29 kati ya 102 alivyopanga kuvitembelea.

Akitolea mfano kwenye elimu amesema wamefanikiwa kujenga madarasa ya Sekondari zaidi ya 100.

Sillo amesema fedha za uviko 19 zilizotolewa chini ya rais wa awamu ya sita Samia Suluhu Hassan, zimejenga madarasa 78 ya shule za Sekondari ambayo kwa sasa yanatumika yakiwa na madawati.

Ameongeza kuwa zimejengwa shule shikizi za msingi 11 ambazo zimesaidia kuwapunguzia wanafunzi adha ya kutembea mwendo mrefu kwenda shuleni.

Akizungumzia upungufu wa walimu amesema serikali imeajiri walimu wapya 50 wa shule za Sekondari na 42 shule za msingi katika jimbo la Babati Vijijini.