Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Kibaha
WAZIRI wa ardhi , Nyumba na Makazi, Jerry Silaa aingilia kati mgogoro wa ardhi kati ya Mohammed Enterprises na wananchi wa Kipangege, Msufini kata ya Soga ,Kibaha Vijijini ,Mkoani Pwani ambapo amesitisha shughuli yoyote isiendelezwe kwa pande zote mbili.
Waziri huyo amechukua hatua hiyo baada ya kufanya ziara katika kijiji hicho kusikiliza changamoto ya mgogoro huo.
Alieleza, kuanzia sasa kila mmoja asiuze,asijenge wala mwekezaji asifanye lolote hadi hapo kero hiyo itakapofanyiwa kazi na kupatiwa ufumbuzi.
“Taarifa na historia inaelezwa 1954 lilipimwa eneo hilo na kupata hati tano, na kumilikiwa kihalali na Mohammed Enterprises “
Baada ya hapo watu walianza kuingia kwenye maeneo hayo na kujimegea vipande,ambapo 2010 kijiji kilipima eneo lililovamiwa na kupata hati ya vijiji.
Kutokana na hilo,Silaa alifafanua kwamba kilichotokea ni kuwepo hati za 1954 juu ya hati ya kijiji suala ambalo limezalisha mgogoro.
“Kazi aliyonipa Rais Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha sekta ya ardhi inakwenda vizuri kwa kuona migogoro inapungua kama sio kuimaliza kabisa “Kwa kutenda haki” anabainisha Silaa.
Kwa mujibu wa upande wa kampuni ya Mohammed Enterprises, inadai wapo kihalali, wana mashamba na hati tano zilizosajiliwa mwaka 1954 lenye hekari 9,023, 1957lenye hekari 2,574, 1957 lenye hekari 1,050,1959 lenye hekari 4,246 na jingine lenye hekari 3,175.
Inaelezea, kutokana na uvamizi na mgogoro walishindwa kuendeleza baadhi ya maeneo na baadae waliamua kuomba watoe hekari 500 ili kuondoa matatizo na wananchi.
Nae Mkazi wa Msufini Hemed Rajab alieleza, walipewa ruhusa ya kujikatia vipande vya shamba na Mwenyekiti wa Kijiji wakati huo ndugu Shomari.
“Shomari ndio alituruhusu kujikatia vipande, nilikuja hapa 2018 nikihitaji eneo la kuishi, na nilimuona Mwenyekiti huyo na nikapatiwa vipande viwili na ndipo nikaanza kuishi eneo hili”
Awali mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini, Michael Mwakamo alieleza kata ya Soga ina mgogoro kijiji cha Kipangege kati ya Mohammed Enterprises ambae analima mashamba ya mkonge na wananchi .
Alieleza, kampuni hiyo iliahidi kurudisha hekari 500 kwa Serikali lakini cha kushangaza hadi sasa utekelezaji bado.
Mwakamo alieleza, kuna mkanganyiko wa hekari hizo kwani wananchi wameambiwa zitakuwa ndani ya sehemu ya eneo wanaloishi na sio kumega hekari 500 nyingine .
Katika ziara hiyo ,Silaa aliendesha Samia klinik ya migogoro ya ardhi ,Mtongani Kibaha Vijijini na kuagiza mwekezaji Talik Ahmed Lupunga kuendelea na umiliki wake kwenye shamba lenye hekari 800 ambalo wananchi walilivamia.
Aliitaka Wilaya ya Kibaha kufanya utaratibu wa kuwaondoa wananchi wote waliovamia kwani waliingia kinyume na sheria.