Siku ya kupiga kura Novemba 2, mwaka huu, Dar es Salaam kulikuwa na utulivu na amani kweli. Ni matokeo ya kuitika mwito wa Rais na utiifu wa uamuzi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam. Watu tulipiga kura tukarudi majumbai kwetu kwa raha mustarehe. Laiti, maagizo yale ya CHADEMA eti “vijana lindenikura zenu” yangefuatwa sijui fujo za mwaka huu zingetupeleka wapi. Utii bila kushurutishwa ndiyo msingi wa amani duniani kote. Viongozi wanaoshabikia uvunjifu washeria na wapenda shari, ubabe hata Mungu huwanyima madaraka maana wataangamiza jamii. 

Kule Mbozi, malalamiko ya wasimamizi kutokukabidhi masanduku mpaka walipwe posho zao (Kigamboni, Temeke pia) na manung’uniko kadhaa wa kadhaa. Haya Tume inaweza kabisa kuyarekebisha huko mbeleni katika chaguzi zifuatazo. 

Lakini malalamiko ya wagombea kuwa taratibu zilikiukwa ni masuala ya kisheria. Walalamikaji wana haki ya kusikilizwa pale wanapoyawasilisha kunakohusika. Mimi sikubaliani na uchelewwshwaji wa matokeo eti msimamizi anashindwa kuzungumza mbele ya vyombo vya habari ana “aleji” ya TV (Mtoni) huo ni uzembe na hatua zichukuliwe. Kama kiongozi alikubali kapokea kazi hapo analazimika kisheria kuwajibika kwa umma. 

Tuipongeze Tume kwa kutoa matokeo ya kura mara kwa mara. Chaguzi zilizopita hayakufanyika hayo. Kadhalika, viongozi wetu wagombea wawe na ule ukomavu wa kisiasa. Tume haiwezi kuchakachua matokeo. Kama uko upotoshwaji basi mzizi wake ni kule kwenye majimbo ya uchaguzi, maana kule wanapaswa kubandika matokeo yakiwa yamekubaliwa na mawakala husika. Hapo Tume haina njia ya kugushi matokeo. 

Nimefarijika sana niliposikia kule Jimbo la Namtumbo baada tu ya kutangazwa mshindi wale wagombea wengine kutoka vyama vya ushindani walimpongeza mwenzao na kuahidi watashirikiana naye kuleta maendeleo ya Namtumbo. Pia Mgombea ubunge wa Arusha mjini, Godless Lema (Chadema), alionekana mwenye runinga na akasikika akisema kila liyechaguliwa katika Uchaguzi huu wa Oktoba 25 ajue anawajibika (answerable) kwa wananchi. Hili ni kweli hata kwa Rais atawajibika kwa wananchi waliompigia kura.

Dosari kadhaa zimeonekana hata waangalizi wa kutoka nje ya nchi wamesema. Katika kila uchaguzi dosari haziwezi kukosekana maana shughuli hii inaendeshwa na binadamu ambaye kwa kuzaliwa kwake hayuko mkamilifu. Hizo ndizo changamoto Tume ya Uchaguzi izianishe na wazifanyie kazi ili uchaguzi ujao uwe umeboreshwa.

Kuna usemi wa kale wa yule mwanafalsafa wa Kigiriki PLATO alioutoa akasema “Better be unborn than be unataught for ignorance is the root of misfortunes”, kwa tafsiri yangu ndiyo kusema “HERI KUTOKUZALIWA kuliko KUTOKUFUNDISHIKA kwa maana UPUMBAVU ndiyo MZIZI wa MABALAA”. Kumbe hata Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere tulipopata Uhuru alitaja moja ya maadui wetu wakubwa ni huo ujinga.

Lakini hapa Baba wa Taifa aliendeleza ufafanuzi kwa kusema ujinga unafundishika lakini upumbavu kamwe hauponyeki. Je, haya yaliyotokea baada ya uchaguzi yamesababishwa na ujinga au upumbavu?

Baadhi ya matukio tuliyoyaamua wakati wa kungojea kutangazwa matokeo ya kura yameashiria upungufu mkubwa wa elimu ya uraia miongoni mwa wananchi.

Kumetokea utekaji nyara gari lenye vifaa vya kura kule Sumbawanga, hiyo ni dalili tosha ya kutokuelimika kwa wananchi wetu. Kumetokea ugomeaji wa kusimamia uchaguzi kwa madai ya malipo kidogo – mathlani kule Kimara Stop over hata ikalazimika kura ipigwe siku iliyofuata ni kiashiria kingine cha ukosefu wa hiyo elimu ya uraia kuhusu uchaguzi.

Yamekuwepo matukioya kuchoma moto ofisi za Serikali za Mitaa (Sandali Temeke) ofisi za Chama Tawala na Mahakama huko Mbozi na Njiro kule Moshi malalamiko ya wasimamizi kutokukabidhi masanduku mpaka walipwe posho zao? (Kigamboni Temeke) na manung’uniko kadha wa kadha. Haya, Tume inaweza kabisa kuyarekebisha huko mbeleni katika chaguzi zifuatazo. 

Utulivu tuliouona siku ile ya uchaguzi tuuendeleze mpaka baada ya kutangazwa matokeo yote. Isitoshe amani tuliyoipata wakati wa uchaguzi ndiyo iendelezwe kutuwezesha kujenga nchi kwa utulivu. Tusitazame nyuma tulikotoka eti mbona huyu alitamka hivi sasa leo kasema hivi. Waingereza wana usemi mmoja mimi nupenda sana wanasema: “all ways fix or concentrate on forwards NEVER turn or reflect backwards” Kaza macho mbele kamwe usigeuke nyuma! Ya nyuma tusahau sasa. 

Sisi tuliokuwa tunafuatilia matokeo yakitangazwa katika ukumbi wa Mwalimu Julius Nyerere tumeona na tumesikia kura zilivyokitangazwa. Oktoba 29, 2015 wakati Mwenyekiti anatangaza majumlisho ya kura za urais, CHADEMA hawakuwepo katika ukumbi ule. 

Waliojiandikisha katika daftari la wapiga kura walikuwa watu 23,161,440 waliojitokeza kupiga kura walikuwa watu 15,589,639. Kura halali zilikuwa 15,193,862, kura zilizoharibika zilikuwa 402,248 Hivyo akaorodhesha matokeo hayo namna hii….. ACT Wazalendo waliambulia kura 98,763, ADC walipata 69,049 kuja CCM zilitajwa jumla ya kura 8,882,935, CHADEMA waliopata kura 6,072,848. Wenzetu wa NRA walipata kura 8,028 wakati CHAUMA walipata kura 49,256 huku TLP walivuna kura 8,198 na chama cha mwisho katika orodha walikuwa UPDP ambao walipata jumla ya kura 7,785. Hapo ndipo alipomtangaza mgombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Dk. John Magufuli kuwa mshindi wa kiti hicho cha Urais kwa kupata asilimia 58.46 ya kura zote dhidi ya mgombea wa CHADEMA aliyeungwa mkono na UKAWA Edward Lowassa aliyepata asilimia 39.97.

Hapo ule ubabe, majigambo na mbwembwe za CHADEMA zililoweshwa na uamuzi wa wananchi wapenda utulivu na Amani. Ni jambo lililotegemewa kuwa CHADEMA wasingalifika pale ukumbini kusikiliza matokeo.

Ustaarabu wa kupokea na kukubali kushindwa na hivyo kupongeza walioshinda haupo katika nchi hii. Kama ilivyotokea katika uchaguzi wa mwaka 2010 ndivyo ilivyotokea na mwaka huu, Dk. Slaa hakutokea katika ukumbu wa matangazo ya kura mwaka 2010 basi na mwaka huu vile vile Mzee Lowassa hakutokea mle ukumbuni. 

Hivyo basi kwa mujibu wa Katiba, mgombea kiti cha Urais akichaguliwa na mgombea mwenza anachaguliwa kuwa Makamu wa Rais. Kwa kuwa mshindi wa Uchaguzi huu ni Dk. Magufuli, hivyo mgombea mwenza wake, Samia Suluhu Hassan anakuwa Makamu wa Rais wa Tanzania. 

Hili haliwashangazi watanzania. Uamuzi wa wananchi juu ya nani awe Raisi wa Awamu ya Tano ulikwishakufanyika kupitia masanduku ya kura Jumapili ya Oktoba 25, 2015. Ushindani siyo uhasama.Ususiaji vikao imekuwa ni tabia iliyozoeleka kwa viongozi wa CHADEMA. Umefika wakati sasa mbinu hii ya ususiaji vikao kushindwa kutoa matokeo (impact) shinikizo kwa hoja za upinzani. Huo ni UBABE usiowaletea tija na ndio uliowakosesha kura za Urais mwaka huu. Haya ni maoni ya baadhi yetu. 

Kwa mlinganisho katika matokeo yale ya mwaka 2010 na haya ya mwaka huu 2015 CHADEMA wamepanda chati sana. Ni kwamba mwaka 2010 mgombea Urais CHADEMA alipata kura 2,371,491 kumbe mwaka huu mgombea Urais wa CHADEMA amekumba kura 6,072,848. Hapo mwamko umekuwa mkubwa kweli.Ushindani umeonekana kuwa mkali. 

Ni vema upinzani ukajaribu kubadilisha mbinu zake sasa. Kwanza waache ile tabia iliyozoeleka ya UBABE navya shari. Pili wana tabia ya ulalamishi wa kuibiwa kura. Wanazushina kukimbilia kuanzisha vurugu. Watu duniani wana usemi kuwa mfa maji hakosi kutapatapa. Sasa kilio chao kisije kutafsiriwa kuwa ni kilio cha mfa maji.

Kama yanayoandikwa mwenye baadhi ya magazeti ni sahihi basi upinzani wajibadilishe kimbinu za mapambano (reorganize or regroup). Mnakumbuka wakati wa mapambano yetu na Nduli Iddi Amin, 1978/1979 kuna wakati alitandikwa vibaya akatangaza hivi, “I was not defeated but I withdrew my forces tactifully to reorganize”. Ndiyo kusema badala ya kukubali kushindwa alisema tu kwamba amerudi nyuma kujipanga upya. Lakini si mnajua kwamba hatukumuona tena? Neno kushindwa ni gumu kulitamka, lakini zipo njia za kukubali yaishe sivyo?

Kutumia mtandao na kuleta watu wa nje hakuwapi ushindi. Siku hizi kila watu wamejanjaruka. Wana zana za kugundua mbinu chafu na hivyo kusambaratisha matamanio ya upinzani. Polisi wa leo wana zana za kisasa wana vijana wasomi, wanaweza kujam hata hiyo mitandao elekezi inayoletwa na wageni kwa nia ya kuchakachua kura za wananchi. 

Basi upinzani wajaribu kuja na hoja za nguvu ili kushawish wananchi lakini si hoja zile zile za miaka iliyopita za kuibiwa kura za uchakachuaji wa matokeo za kupinga matokeo na kuvunja sheria za nchi kwa kujitangazia matokeo, yao wenyewe. Viongozi wakuu wote hatuoni wanadundwa na Polisi barabarani wala kuwekwa selo.

Inakuwaje wanaosekwa rumande na kumwagiwa maji ya washa washa ni hawa vijana wa kawaida wa mitaani? Mbona watoto wa viongozi hatuwaoni wala kuwasikia kati ya vijana wanaorundikwa selo? Hili vijana wote walitafakari na mwisho wa siku waseme “HATUSHAWISHIKI” waache kuingia mitaani kwa lengo la kufanya fujo. 

Uchaguzi ndio umekwisha. Matokeo ndiyo hayo yametangazwa na Tume ya Uchaguzi kilichobaki sasa kwetu Watanzania ni KAZI tu. Tushikamane kitaifa, tuwe wazalendo wa kweli na tukaze macho yetu mbele kwenye mwelekeo wa mabadiliko ya kweli. Mkao wa kula kwa jasho lako”. Mtaji wa maskini ni nguvu zake mwenyewe”. Daima watanzania tukumbuke wimbo wetu wa Taifa – 

“Mungu ibariki Tanzania

Dumisha Uhuru na Umoja 

Wake kwa waume na watoto”

Hapo tunajiombea kuendeleza Uhuru wa Taifa letu na Umoja kati yetu sote. Suala la Uchaguzi sasa limepita tuishi kama watanzania huru, wamoja na wapenda Amani. ADIOS!