DAR ES SALAAM

Na Christopher Msekena

Niwapongeze wanawake kwa kusherehekea Siku ya Wanawake Duniani. Ni siku muhimu ambayo wanawake pekee waliothubutu kufanya mambo makubwa kwenye sekta mbalimbali ndio wanastahili kupokea pongezi hizo.

Nyakati zimebadilika na sasa ni majira ambayo tunaona wanawake wakiwa mstari wa mbele kwenye kila Nyanja, tofauti na miaka kadhaa iliyopita ambayo jinsia ya kike ilikuwa adimu kwenye sekta nyingi.

Ongezeko la wanawake kwenye sekta nyingi ni ishara kwamba sasa hakuna kuchukulia poa tena kama ilivyokuwa zamani ambapo wanaume ndio walikuwa wengi kuliko jinsia ya kike.

Miongoni mwa tasnia ambazo zimepata bahati ya kuwa na ongezeko kubwa la warembo ni burudani, yaani muziki, filamu na kwingineko ambako sasa tuna wasichana kibao wanafanya kazi zao.

Tasnia ya burudani imekuwa ikitawaliwa na wanaume kwa muda mrefu. Wanawake walikuwa wachache kiasi kwamba wanaume walionekana kutawala zaidi kwenye muziki na filamu.

Ila kwa sasa mambo ni tofauti. Tasnia ya muziki wa Bongo Fleva imekuwa ikipokea maingizo mapya ya wasanii wa kike kila uchwao, hivyo kufanya idadi ya waimbaji wa jinsia ya kike wawe wengi.

Wasanii kama Sarafina, Malkia Karen, Angela wa Konde Gang ni miongoni mwa wasanii wengi wa kike ambao mashabiki wamewapokea na sasa wanafanya vizuri.

Si tu wasanii, bali hata miradi mikubwa imekuwa ikibuniwa  ili kuzalisha bidhaa zinazowagusa moja kwa moja wasanii wa kike na inapendeza kuona serikali imekuwa ikiwapa sapoti.

Mfano ni mradi wa Dada Hood ambao ulianzishwa miaka kadhaa iliyopita na mtangazaji wa Clouds FM, Mamy Baby na kuwakusanya  marapa wa kike nchini na kufanya nyimbo za pamoja.

Tazama mradi huo umekua na sasa wamekuja na harambee ya kuchangisha fedha ili kuipa nguvu timu ya taifa ya mpira wa miguu ya wanawake ili izidi kufanya vizuri kwenye tasnia hiyo katika anga la kimataifa.

Ikiwa leo ndiyo Siku ya Wanawake Duniani, Dada Hood wameandaa jambo lao hilo katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam ili kufanikisha mpango huo.

Aidha, katika harambee hiyo itakayopambwa na burudani kibao kutoka kwa wasanii wa Dada Hood na wengineo, taasisi hiyo itazindua albamu yake inayoitwa ‘Orange’.

Mkurugenzi wa taasisi ya Dada Hood, Mamy Baby, ameweka wazi kuwa ndani ya albamu hiyo kutakuwa na ngoma kibao zilizoimbwa na wasanii mbalimbali wa kike.

“Tutaizindua Orange katika hafla hiihii ya kuwachangia Twiga Stars, albamu imeitwa Orange kwa sababu ni rangi ambayo kidunia inatumika kama alama ya kupinga ukatili kwa wanawake,” amesema Mamy Baby.

Kwa hiyo unaweza kuona ni namna gani warembo hawa wanavyoupiga mwingi kwenye tasnia ya muziki kiasi kwamba wanafikiria nje ya boksi kusaidia wanawake wenzao wanaoipigania nchi kwenye upande wa soka.

Si tu kwenye muziki – mpaka kwenye filamu. Ukiangalia miaka ya hivi karibuni filamu zimekuwa adimu na wengi wamehamia kwenye ulimwengu wa tamthilia zinazoonyeshwa kwenye ving’amuzi mbalimbali.

Mfano ni tamthilia ya Jua Kali ambayo imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kupenya kwenye macho ya mashabiki wengi wanaofuatilia burudani.

Jua Kali ni miongoni mwa tamthilia chache zinazopendwa zaidi kwa sasa hapa Bongo, na hiyo yote imetokana na ukweli kwamba aliyeiandaa, alikaa chini akaumiza kichwa na akafanikiwa kukonga nyoyo za mashabiki.

Habari nzuri zaidi ni kwamba tamthilia hiyo imeandaliwa na mwanamke, Leah Mwendamseke, maarufu kama Lamata, ambaye amefanikiwa kuonyesha kuwa wanawake wanaweza.

Ndani ya tamthilia hiyo ameweza kuwachanganya waigizaji maarufu na wasio maarufu, wote wakaweza kuifanya Jua Kali kuwa miongoni mwa tamthilia zinazofuatiliwa zaidi kwa sasa.

Hiyo yote ni kuonyesha kwamba wanawake wameupiga mwingi sana kwenye tasnia ya burudani na katika kilele cha siku yao, naamini kuna wanawake wengi zaidi wataendelelea kuingia kwenye muziki na filamu.

Kiu yangu kubwa ni kuona wanawake wenyewe kwa wenyewe wakishikana mikono na kupeana sapoti kwenye kazi zao za sanaa ili kuondoa ile dhana kwamba wanawake hawapendani au ule msemo wa mwanamke akiwezeshwa anaweza.