ARUSHA

Na Zulfa Mfinanga

Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani (IWD) hufanyika Machi 8 ya kila mwaka tangu yalipoanza kuadhimishwa kimataifa mwaka 1911.

Ni zaidi ya miaka 25 sasa tangu kufanyika kwa Mkutano wa Beijing ulioweka bayana makubaliano ya msingi hukusu mustakabali wa wanawake, hususan usawa wa kijinsia.

Maadhimisho ya siku hii yamechagizwa na vuguvugu la wafanyakazi ambapo wanawake takriban 15,000 waliandamana jijini New York, wakidai muda mfupi wa kufanya kazi, malipo bora na haki ya kupiga kura. 

IWD imekuwa siku ya kusherehekea wanawake walipofika katika jamii, siasa na uchumi.

Maadhimisho ya siku hii nchini Tanzania huambatana na wanawake kuonyesha shughuli zao mbalimbali ikiwamo kazi, fani na vipaji walivyonavyo.

Lengo hapa ni kuwainua na kuwahamasisha wanawake kujiamini katika kutimiza malengo yao.

Maadhimisho ya mwaka huu mkoani Arusha yalipambwa na kupendezeshwa na binti mwenye umri wa miaka 26, Muzna Hamad, ambaye ni mwajiriwa wa Halmashauri ya Jiji la Arusha.

Ajira ya Muzna ni ya aina yake kwa watoto wa kike, kwa kuwa yeye si karani, bali ni dereva wa mtambo wa rola katika miradi ya ujenzi wa miundombinu ya barabara.

Ama kwa hakika uwepo wa Muzna umekwenda sambamba na kaulimbiu iliyopitishwa na Umoja wa Mataifa (UN) kwa mwaka huu katika Siku ya Wanawake Duniani isemayo; ‘Usawa wa kijinsia leo, kesho na endelevu’.

Ni nadra sana kukutana na binti anayejiamini huku akifanya kazi ambayo haijazoeleka katika macho ya jamii kufanywa na wanawake. Muzna ameonyesha njia.

Katika mahojiano na JAMHURI, Muzna anasema alimaliza elimu yake ya sekondari kidato cha nne mwaka 2013, na kisha kujiunga na fani ya udereva mwaka 2014 na kupata cheti cha udereva daraja D. Ameongeza kusema kuwa mwaka 2015 alijiunga na Chuo cha Bandari na kusomea kozi fupi ya miezi miwili kwenye udereva wa foko.

Anaendelea kusema kuwa mwaka huo huo 2015 alisoma kozi nyingine fupi ya miezi miwili kwenye fani ya mashine za kunyanyua mizigo bandarini.  Anasema baada ya kuhitimu kozi zote aliomba kujitolea katika Halmashauri ya Jiji la Arusha kwa muda wa mwaka mmoja kwenye sekta ya kuendesha mtambo wa rola.

“Jitihada zangu wakati najitolea zilinisaidia kuniongeza ujuzi zaidi na kusababisha kupata ajira kwenye halmashauri hii, kazi ambayo naifanya hadi sasa ambapo imekuwa na mafanikio makubwa kwangu, kwani jamii na hasa watoto wa kike wamekuwa wakihamasika wanaponiona nikiwa kazini na kutamani kuwa kama mimi,” anasema Muzna.

Akizungumza katika maadhimisho hayo, mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongella, amesema kwa kutambua jitihada zinazofanywa na wanawake ndiyo maana serikali imeanzisha KanziData ambayo itasaidia kuhifadhi taarifa za wanawake wote wenye sifa, ujuzi na fani mbalimbali kwa ajili ya kurahisisha upatikanaji wao pindi watakapohitajika.

“Kwenye maadhimisho haya pia nitazindua rasmi KanziData ambayo itasaidia kujua nani ni nani, yupo wapi na anafanya nini, hii itasaidia kumpata pale ambapo atahitajika, ni suala tu la jamii kuendelea kuwahamasisha na kuwaendeleza wanawake kwani tumemuona huyo binti alivyoweza kuwavutia wengi kwa kuendesha mtambo ambao mara nyingi huonekana ukiendeshwa na wanaume,” anasema mkuu wa mkoa.

Anasema kwa sasa jamii inaendelea kuelimika na kutoa fursa kwa wote, ambapo pia serikali imejipanga kuhakikisha ulinzi wa mama na mtoto kupitia kamati ngazi ya kata hadi taifa ili kuweka usawa kwa wote na kufikia sera ya 50 kwa 50.

“Wanawake ni kundi linalotegemewa sana na jamii, na ili kufikia malengo yanayotarajiwa ni lazima washirikishwe kikamilifu, hasa kwenye zoezi la Sensa ya Watu na Makazi inayotarajiwa kuanza mwezi Agosti mwaka huu, hatuna budi kushirikisha wanawake katika kuhamasisha ushirikiano,” anasema Mongella.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Geofrey Pinda, anasema wizara inaendelea kutafakari miundombinu itakayowawezesha wanawake ikiwa ni pamoja na kufanya marekebisho ya Sheria ya Ndoa ya mwaka 2002 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2019 na Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009.

Naye Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Amon Mpanju, amewataka wakuu wote wa mikoa kusimamia kamati za Ulinzi na Usalama za wanawake na watoto kuanzia ngazi za kata hadi mkoa ili kuhakikisha makundi hayo yanaishi mazingiza salama na kufikia malengo yao.

Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Arusha,  Maximilian Irange, amesema kushindwa kwa wanawake wengi kunatokana na saikolojia iliyozoeleka ya kwamba wanawake ni daraja la pili, jambo ambalo si kweli, kwani hakuna kinachofanywa na mwanamume ambacho mwanamke hawezi.

Mstahiki Meya anasema kwa sasa wanawake wengi duniani wamefanya mapinduzi makubwa ya kifikra kwani licha ya wanawake kuongoza taasisi na mashirika ya umma au binafsi lakini pia wapo kwenye ajira zisizo rasmi kama vile kubeba zege na hata kuchimba mitaro.

“Kazi yoyote inahitaji kuipenda, kujiamini na kujitokeza, kwani kinachotakiwa ni ‘mechanism’, si kuwa na misuli au nguvu nyingi, na tunashukuru Mhe. Rais anajali sana hili na ndiyo maana unaona Wizara nyeti kama ya Ulinzi inaongozwa na mwanamke, maana hata nchi za wenzetu mawaziri wa ulinzi na usalama ni wanawake,” anasema Mstahiki Meya.

Akimzungumzia binti huyo, Mtunza Hazina wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, Mariam Mshana, licha ya kumpongeza lakini amewataka wasichana na wanawake kwa ujumla kujitokeza kusomea fani zozote ikiwa ni pamoja na kuomba kazi zozote zinazotangazwa bila kuangalia jinsia zao, kwani kinachoangaliwa ni elimu, uwezo na ujuzi walionao, si maumbile.

“Siku zote mimi huwa nasema, kinachofanya kazi si maumbile, ni ujuzi tulionao, kama mimi ni mkuu wa kitengo cha fedha lakini ni mwanamke, Rais wetu ni mwanamke lakini anaongoza nchi, na kikubwa zaidi anaweza kuongoza vizuri sana, sasa kwanini mabinti/wasichana na hata akina mama wasite kufanya jambo wanaloona ni jema kisa jinsia zao?” anahoji Mshana.