Katika toleo lililopita, simulizi yangu ya kupanda Mlima Kilimanjaro, iliishia pale nilipojikongoja kufika Horombo, baada ya kupata matatizo ya goti nikiwa njiani kutoka geti la Marangu kuelekea Mandara. Kama unakumbuka, nilisema nilifika Horombo nikiwa wa mwisho na hiyo ilikuwa ni kama baada ya nusu saa tangu wapanda mlima wenzangu wafike kituoni hapo.
Utani kutoka kwa baadhi ya rafiki zangu ulishamiri. Nakumbuka utani wa Dickson Busagaga pamoja na Ramadhan Mvungi, ambao walikuwa wakiniita ‘The Undertaker’ wakinifananisha na yule mcheza mieleka wa Marekani ambaye amekuwa akifahamika kwa jina hilo.
Kutoka Horombo kueleka Kibo ni umbali wa kilomita 15, si umbali mrefu sana, lakini hapo sasa ndiyo yale majibu ya kupanda Mlima Kilimanjaro unayapata kuanzia hapo, maana umbali kutoka usawa wa bahari unapanda mpaka zaidi ya mita 3,000.
Hali ya hewa inabadilika, kunakuwa na baridi huku mwongoza wapanda mlima, Faustine Chombo, akisisitiza kunywa maji, anasema maji ndiyo siri pekee ya ‘kutoboa’ yaani kuupanda Mlima Kilimanjaro mpaka kufikia kilele chake – ‘Uhuru Peak’.
Nikiwa njiani umbali wa kama kilomita nne hivi kutoka Horombo kuelekea kituo cha Kibo, huku nikiwa najikongoja na fimbo zangu mbili za kupandia mlima, nikiwa nimevaa mavazi maalumu ya kuzuia baridi pamoja na begi dogo ‘day pack’ mgongoni, ninaanza kuyasikia maumivu makali ya goti langu la kulia.
Haraka anakuja rafiki yangu Nocholaus Kabila, ananisaidia begi hilo dogo, wakati akiwa amebeba begi jingine lenye takribani kilogramu kama 20 hivi, namuuliza kama atamudu, anatabasamu na kuniambia;
“Kaka hii ndiyo kazi yangu kwa zaidi ya miaka 23, hakuna shida. Nitahakikisha unatoboa…usiwe na wasiwasi tukifika pale Kibo, hilo goti tutalifanyia maarifa tu. Tutalikanda kwa maji moto, pamoja na kulichua, tayari kwa safari ya kuelekea kilele cha Mlima Kilimanjaro.”
Maneno yake hayo yananipa nguvu na kuyasahau kwa muda maumivu ya goti ambalo hata hivyo tayari lilikuwa limefungwa ili kuniwezesha kutembea. Nikaendelea kutembea kuelekea Kibo.
Nikiwa njiani, Kabila akawa ananihadithia mambo yanayowapata wapanda mlima, huku akisisitiza nisiwe na haraka na badala yake niende pole pole. Katika mazungumzo yake akataja neno kikapu/kapu. Nikapata shauku ya kufahamu kuhusu msamiati huo, maana mimi nimezoea kapu lile linalotumika kwenda sokoni.
Kabila anacheka kidogo na kuendelea kusema, “Unajua, sisi huku tunazo lugha zetu ambazo wapagazi na waongoza watalii pekee ndiyo wanaoweza kuzielewa…nikisema kikapu/kapu, namaanisha mtu ambaye ameshindwa kutoboa na anahitaji msaada wa kushushwa haraka.”
Basi nikaanza kuwaza, je, sitakuwa kikapu? Maana tayari goti langu la kushoto lilishaanza kupata hitilafu. Nikapiga moyo konde kwamba nilikotoka ni mbali zaidi ikilinganishwa na sehemu iliyobaki kufika kilele cha Mlima Kilimanjaro.
Nilijitahidi pamoja na maumivu makali ya goti, lakini kadri nilivyokuwa napakaribia Kibo basi ndivyo maumivu yalivyokuwa yakizidi. Pamoja na maumivu hayo, sikuwa wa mwisho kufika katika kituo cha Kibo, bali mwenzangu mwingine alizidiwa, tena akiwa hana matatizo ya goti. Baada ya kutoka jiwe la Ukoya, sehemu ambayo mwinuko unakuwa mkali, akaanza kuwakumbuka watoto wake.
Hali ya kuwakumbuka familia ilikuwa ni kawaida kabisa kwa wapanda mlima wenzangu, maana baadhi walianza mpaka kusema hawakuwa wameandaa wosia, ilikuwa ni kama hali ya utani lakini katika utani huo kuna ujumbe ulikuwa unafika.
Sikusudii kukupeleka katika hadithi hizo nyingine, ngoja turudi katika simulizi yangu mwenyewe. Kutoka katika jiwe la Ukoya mpaka hapo Kibo ni umbali wa kilomita moja na nusu, umbali huo mdogo nakumbuka nilitembea kwa saa moja na nusu, huku nikinyeshewa na manyunyu ya barafu.
Hatimaye nikafika Kibo. Mara baada ya kufika nikapatiwa kikombe cha chai, ninainywa kama maji, saa kadhaa baadaye nagundua kwamba ngozi ya ulimi ilikuwa imechubuka, ndipo nakumbuka kwamba itakuwa imeunguzwa na chai ambayo kutokana na mazingira ya baridi kali iliyopo Kibo, nilihisi chai haina joto sana.
Haraka ninaelekea chumba cha kupumzika, ili nipatiwe huduma ya kuchua na kukanda goti langu tayari kwa maandalizi ya kupanda mlima usiku wa saa tano. Pale anaitwa kijana ambaye kwa bahati mbaya alinipatia jina lake moja tu, Lucas, huyo anakuja na maji ya moto na kuanza kunikanda huku, akinisisitiza kwamba lazima nitoboe, huku akilinganisha na umbali niliotembea kufika Kibo.
Kutoka Kibo mpaka kilele cha Mlima Kilimanjaro ni kilomita sita tu, lakini zilinishinda! Usishangae, sikushindwa kwa sababu ya goti, la hasha, usiku ule nikapata tatizo la kupungukiwa na hewa ya ‘oxygen’, hiyo ikiwa ni muda mfupi baada ya kuondoka Kibo kuelekea kituo cha Gilmans.
Usiku huo wa saa sita na nusu hivi, baada ya kutembea kwa dakika kama hamsini hivi, naanza kupata shida ya kupumua, pamoja na kizunguzungu. Nilikuwa kama mtu wa nane hivi katika kundi la wapanda mlima zaidi ya 30, ambao katika kupanda mlima tunakaa msitari mmoja.
Nakumbuka Kabila hakuwa mbali, alikuwa na kifaa maalumu cha kupima oxygen kinachoitwa ‘oxymeter’ akanipima na kukuta ilikuwa iko 57, akasikitika na kuniambia, “kaka hapa huwezi kuendelea tena kupanda mlima…hii ‘oxygen’ siyo nzuri kabisa, walau ingekuwa 80 ningesema tuendelee. Kadri tunavyozidi kwenda juu hali itakuwa mbaya zaidi.”
Nikapatiwa kijana mmoja anirudishe pale Kibo, nikiwa njiani nikawa mwenye huzuni, maana naona sikutimiza azma yangu ya kufika kwenye kilele cha Mlima Kilimanjaro nikiwa nimetembea zaidi ya kilomita 30. Pamoja na kutofika kilele cha mlima huo, nimeahidi kurudi kumalizia pale nilipoishia.
Siku iliyofuata, asubuhi sana nikaanza safari ya kurudi Horombo, wale waongoza wapanda mlima wanashauri kwamba Kibo ni sehemu nzuri kukaa kusubiri wenzangu ambao walikuwa wamefanikiwa kupanda, nilitamani kuwasubiri ila haikuwezekana badala yake siku hiyo jioni ya saa kumi na mbili ndiyo wakaanza kurejea pale Horombo.
Wengine wakiwa na maswali kwa nini nimeishia njiani, huku waliokuwa wakifahamu kilichonisibu wakinipa pole. Pamoja na kutofika kilele cha Mlima Kilimanjaro, nimepata hamasa ya kuwashawishi vijana wenzangu walau tuwe na kampeni ya kupanda Mlima Kilimanjaro, kama ambavyo limekuwa jambo la kudumu kwa Mkuu wa Majeshi mstaafu, Jenerali George Waitara.