Wakati Rais John Magufuli akikagua gwaride la maadhimisho ya miaka 55 ya Uhuru, kundi la wanahabari, askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) pamoja na wanadiplomasia walikuwa kwenye kilele cha Mlima Kilimanjaro.
Safari hiyo ilianza mapema Desemba 5, katika lango kuu la Marangu, njia inayosemekana kuwa rahisi kwa mpandaji wa Mlima Kilimanjaro. Hotuba kutoka kwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, pamoja na kiongozi wa msafara huo wa kupanda mlima ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Jenerali mstaafu George Waitara.
Katika hotuba yake kabla ya kuanza safari kuelekea kilele cha Mlima Kilimanjaro, Jenerali Waitara, ambaye amekuwa akipanda mlima huo kila mwaka tangu 2008, aliwaambia wanahabari pamoja na washiriki wengine sababu ya yeye kupanda mlima huo kila mwaka.
Jenerali mstaafu Waitara anasema alianza kupanda mlima huo baada ya kuombwa na Mkuu wa mstaafu wa Majeshi, Jenerali Mirisho Sarakikya, hasa baada ya umri wake kusogea, huku akitamani kuona utamaduni huo ukiendelezwa. Waitara hakusita na amekuwa anafanya hivyo kwa miaka minane mfululizo.
Safari ya siku sita ikaanza, huku washiriki wote 36, wakiwa na mabegi yaliyo na baadhi ya vifaa vyepesi vya kupandia mlima pamoja na maji wakianza msafara huo kwa mbwembwe nyingi. Njiani zilikuwa ni nyimbo tu, hasa ikizingatiwa katika msafara huo kulikuwa na vijana wazalendo kutoka jeshini.
Kwangu ilikuwa mara ya kwanza kupanda mlima huo mrefu kuliko yote barani Afrika, na mlima pekee unaojitegemea. Wakati nikiendelea na safari ya kufika kituo cha kwanza cha kupumzika, Mandara, umbali wa kilomita nane, kichwani nilikuwa na maswali ambayo hata baada ya kumwuliza Jenerali Waitara amekuwa akisisitiza kwamba nisiwe na wasiwasi, maswali yangu yatajibiwa na mlima.
Nimekuwa nikisikia hadithi nyingi kuhusu kupanda Mlima Kilimanjaro, lakini baada ya kumaliza hizo kilomita nane, nikaanza kupata picha ya huko niendako, maana pale ilikuwa ni kama robo ya safari nzima. Baada ya kufika Mandara, hali ya hewa inabadilika, kunakuwa na baridi kali ikilinganishwa na Marangu.
Mandara ni kituo cha kwanza kabla ya kufika Horombo, tunafika hapo baadhi yetu tukiwa tumechoka baada ya kutembea umbali huo mrefu. Hata baada ya kutembea umbali huo, jasho lilikuwa ni bidhaa adimu sana, kuoga ikawa historia tena, na pengine wengi tulioga siku ya Jumatatu asubuhi tukiwa bado tuko Moshi.
Baada ya kufika Mandara, ikanikumbusha wakati nikisoma sekondari, ambako tulikuwa tukilala katika mabweni na kushirikiana chumba kimoja watu zaidi ya wawili. Nikiwa Mandara, ndipo nilipokumbuka miaka kadhaa iliyopita baada ya kushirikiana chumba na wapanda mlima wenzangu wengine wanne.
Tukiwa njiani, utani kwa baadhi yetu hasa wanahabari ambao kwa namna moja ama nyingine tumekuwa tukifahamiana, ulikuwa sehemu ya kuchagiza safari ambayo kwa kweli sikuwa najua kitu ninachokwenda kukutana nacho. Nakumbuka baadhi ya uchagizaji wa waongoza wapanda mlima, wakisema ‘Kili Timu….who haaaa’.
Kwa wale wapenda mazingira, pengine safari hiyo ingewasikitisha, maana njiani unaona vilivyokuwa vijito sasa vimekauka, na kuacha alama tu kwamba maji yamewahi kutiririka katika eneo hilo, kichwani naanza kupata mawazo ya athari za uchafuzi wa mazingira pamoja na mabadiliko ya tabianchi.
Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro, kama zilivyo hifadhi nyingine za Taifa, haziruhusiwi kazi zozote za kibinadamu, lakini bado athari za mabadiliko ya tabianchi zinajionesha wazi, hiyo ikanikumbusha wajibu wa kila mwanajamii kushiriki kikamilifu katika kuhakikisha tunapambana na mabadiliko ya tabianchi.
Nimeona niliseme hilo maana ni wajibu wetu sote kuhakikisha tunapambana na mabadiliko ya tabianchi. Siku ya pili saa kumi na mbili alfajiri, kwa mara ya kwanza ratiba yangu inabadilika na hiyo ni kutokana na maelekezo ya mkuu wa waongoza utalii aitwaye Faustine Chombo.
“Poleni sana kwa uchovu ndugu zangu wapanda mlima, naomba niwapatie ratiba ya kesho…asubuhi saa kumi na mbili tutaletewa chai tukiwa bado tuko kitandani, baada ya chai hiyo tutajiandaa na kupata chai ili tuendelee na safari kuelekea Horombo.
“Siri kubwa ya kupanda Mlima Kilimanjaro, ni pamoja na kunywa maji ya kutosha kila siku, nitapenda kuona kila mmoja wenu walau anakunywa maji kuanzia lita tatu kwa siku…jitahidini mnywe maji, yatawasaidia sana,” anasema Chombo katika moja ya mabanda maalumu ya kupata chakula.
Mpaka tunafika Mandara, tayari nilishapata tatizo la goti, tangu sehemu inaitwa nusu-njia, goti langu la kushoto lilipata mshituko na hivyo kunifanya kutembea kwa tahadhari huku wakati mwingine nikihitaji msaada wa huduma ya kwanza ambayo ilikuwa ni sehemu ya huduma za msingi kwenye safari hiyo ambayo sitaisahau kamwe.
Baada ya kupata chai, safari inaanza kueleka Horombo, umbali wa kama kilomita 11 kutoka Mandara, hapo hata mwinuko wa mlima Kilimanjaro sasa unaanza kuuhisi kupitia upumuaji, maana unaanza kuhisi kama kifua kinajaa na kutoa pumzi kwa shida kidogo.
Mwendo huo wa kilimita 11 unachukua zaidi ya saa nane, huku goti likiendelea kunisumbua, nikajitahidi kufika Horombo – nakumbuka nilifika nikiwa wa mwisho, huku mmoja wa waongoza watalii, Nicholaus Kabila, akiwa nami bega kwa bega katika kuhakikisha ninafika katika kilele cha Mlima Kilimanjaro.
Usikose toleo lijalo la JAMHURI ambapo nitazidi kuandika kuhusu safari yangu kuelekea kilele cha Mlima Kilimanjaro.