Leo siku ya Jumanne tarehe 13 Julai, mwaka 2021, ni miongoni mwa siku kumi bora za Mwezi wa Dhil Hijja (Mfungo Tatu) Mwaka wa Kiislamu 1442 Hijiriyyah (toka Mtume Muhammad –Allaah Amrehemu na Ampe Amani – alipohajiri kutoka Makkah kwenda Madina), ambapo siku ya kumi ndiyo Sikukuu ya Eid Al-Adh-ha ambayo ni moja ya siku bora mbele ya Mwenyeezi Mungu Mtukufu kwa mujibu wa mafundisho ya Dini ya Uislamu.

Kuwapo kwa siku hizi bora na tukufu ni katika yanayoonyesha rehema kunjufu za Mwenyeezi Mungu kwa waja wake kiasi kwamba anawasamehe waumini makosa yao na anawafutia madhambi yao pale wanapotubu toba ya kweli na kuweka ahadi ya kutorejea kwenye maasi ambayo wameyaombea toba. 

Mwenyeezi Mungu Mtukufu amezitenga kwa waja wake siku bora, tukufu, zenye baraka, zinazokuja mara moja kwa mwaka ili waja wake waweze kumuelekea Mola wao mlezi kwa kumuomba msamaha na kumuomba haja zao.

Kwa mnasaba wa kuingia katika mwezi wa Dhil Hijjah makala hii itaangazia siku bora mbele ya Mwenyeezi Mungu Mtukufu kwa mujibu wa Uislamu ambazo ni: Siku ya Arafa, Usiku wa Cheo (Lailatul Qadri), Siku Kumi Bora za Mwezi wa Dhil Hijjah (Mfungo Tatu) na Siku ya Ijumaa.

Siku ya Arafa

Siku ya Arafa (Yaumu Arafah) ni siku ya tisa katika mwezi wa Dhil Hijjah (Mfungo Tatu) ambayo ni miongoni mwa siku bora kwa Waislamu, ambapo mahujaji husimama katika Mlima wa Arafa uliopo Makkah nchini Saudi Arabia, wakitekeleza moja ya nguzo muhimu za ibada ya Hijja.

Kuna rai mbalimbali juu ya sababu za mlima huu kuitwa ‘Mlima wa Arafa’ na mojawapo ni ile inayosema kuwa ni katika mlima huu ndipo baba yetu Adam alikutana na mama yetu Hawa na wakatambuana tangu walipotoka peponi.

Miongoni mwa yanayoipa ubora siku hii ya Arafa ni haya yafuatayo:

(1) Siku ya Arafah ndiyo siku lilipotoka tangazo la Mwenyeezi Mungu la kuikamilisha Dini ya Uislamu, siku ambayo waislamu wametekeleza na kuikamilisha ibada ya Hijja, moja ya nguzo tano za Uislamu. Mwenyeezi Mungu anatuambia katika Qur’aan Tukufu Sura ya 5 (Al-Maida) Aya ya 3 kuwa: “ … Leo nimekukamilishieni dini yenu, na nimekutimizieni neema yangu, na nimekupendeleeni UISLAMU uwe ndiyo Dini…”

(2) Siku ya Arafah ni miongoni mwa sikukuu za Uislamu na Waislamu. Mtume Muhammad (Mwenyeezi Mungu Amrehemu na Ampe Amani) amesema: “Hakika Siku ya Arafah (Mwezi Tisa Mfungo Tatu) na Siku ya Kuchinja (Mwezi Kumi Mfungo Tatu) na Siku za Tashriiq (Mwezi Kumi na Moja, Kumi na Mbili na Kumi na Tatu Mfungo Tatu) ni sikukuu zetu sisi Waislamu. Hizo ni siku za kula na kunywa.”

(3) Siku ya Arafah ni siku ambayo Mwenyeezi Mungu ameiapia na Mwenyeezi Mungu hakiapii isipokuwa kilicho kikubwa na kitukufu. Tunasoma katika Qur’aan Tukufu Sura ya 85  (Al-Buruuj) aya ya 3 kuwa:  “Na kwa shahidi na kinachoshuhudiwa!”

Wanazuoni wa Tafsiri ya Qur’aan Tukufu wamesema kuwa hapa ‘Shahidi’ ni Siku ya Ijumaa na ‘Kinachoshuhudiwa’ ni Siku ya Arafah. 

(4) Siku ya Arafah ni siku bora ambayo Mwenyeezi Mungu anawasamehe waumini madhambi yao na anajivunia watu wa ardhi (dunia) kwa watu wa mbinguni (malaika). Swahaba Jaabir (Mwenyeezi Mungu Amridhie) amehadithia kwamba Mtume Muhammad (Mwenyeezi Mungu Amrehemu na Ampe Amani) amesema: “Hakuna siku iliyo bora kabisa mbele ya Allaah kama siku ya Arafah. Anateremka Mwenyeezi Mungu Mtukufu mbingu ya dunia (ya kwanza) kisha anajivunia watu wa  ardhi kwa watu wa mbinguni.” 

Katika Hadithi nyingine, Mtume Muhammad (Mwenyeezi Mungu Amrehemu na Ampe Amani) amesema: “Hakika Mwenyeezi Mungu Mtukufu hujigamba kwa watu (walio katika viwanja vya) Arafah kwa Malaika wake jioni ya Arafah na husema: “Watazameni waja Wangu wamenijia wakiwa timtimu wamejaa vumbi…” (Hadithi hii inapatikana katika kitabu cha Hadithi za Mtume Muhammad kiitwacho Musnad Ahmad).

Pia Bibi Aisha (Mwenyeezi Mungu Amridhie) amehadithia kwamba Mtume Muhammad (Mwenyeezi Mungu Amrehemu na Ampe Amani) amesema: “Hakuna siku Mwenyeezi Mungu anayoacha huru kwa wingi waja kutokana na moto kama siku ya Arafah. Na huwa karibu kisha anajigamba kwao kwa malaika na husema: Wametaka nini hawa? Shuhudieni malaika wangu kwamba hakika mimi nimewasamehe (Nimewafutia madhambi yao).” (Hadithi hii inapatikana katika Kitabu Swahihu At-Targhiib).

(5) Siku ya Arafah ni siku ambayo Mwenyeezi Mungu hukubali maombi ya waja wake waumini kote duniani. Mtume Muhammad (Mwenyeezi Mungu Amrehemu na Ampe Amani) amesema: “Dua (maombi) bora kabisa ni dua katika siku ya Arafah, na yaliyo bora kabisa niliyosema mimi na manabii kabla yangu ni: Laa Ilaaha illa Allaah Wahdahu laa shariyka Lahu, Lahul-Mulku Walahul-Hamdu wa Huwa ‘alaa kulli shay-in Qadiyr. (Hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allaah mmoja pekee asiye na mshirika, ana ufalme na anastahiki sifa njema na yeye ni muweza juu ya kila kitu)”  

Usiku wa Cheo (Laylatul Qadri):

Usiku wa Cheo (Laylatul Qadri) ni usiku mtukufu unaopatikana ndani ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Usiku huu una fadhila nyingi na miongoni mwa hizo ni kuwa ibada ifanywayo katika usiku huu, ikikubaliwa, malipo yake ni sawa na ibada ya miezi elfu moja (Miaka 83 na miezi 3). Katika Qur’aan Tukufu Sura ya 97 (Surat A-Qadri) Aya ya 1 hadi ya 5, Mwenyeezi anatubainishia utukufu wa usiku huu kuwa: “Hakika sisi tumeiteremsha Qur’ani katika Laylatul Qadri, Usiku wa Cheo Kitukufu. Na nini kitakachokujulisha nini Laylatul Qadri? 

Laylatul Qadri ni bora kuliko miezi elfu. Huteremka Malaika na Roho katika usiku huo kwa idhini ya Mola wao mlezi kwa kila jambo. Amani usiku huo mpaka mapambazuko ya alfajiri.”

Miongoni mwa yanayoupa ubora usiku huu (Laylatul Qadri) ni haya yafuatayo:

(1)  Mwenyeezi Mungu Mtukufu ameiteremsha Qur’aan Tukufu katika usiku huu ndani ya Mwezi wa Ramadhani kama tunavyosoma katika Qur’aan Tukufu, Sura ya 2 (Surat Al-Baqarah), Aya ya 185 kuwa: “Mwezi wa Ramadhani ambao imeteremshwa humo Qur’ani kuwa ni uwongofu kwa watu, na hoja zilizo wazi za uwongofu na upambanuzi…”  

(2) Usiku huu ni bora kuliko miezi elfu moja na kwamba atakayekubaliwa ibada yake katika usiku huu malipo yake ni makubwa sana.

(3) Kama ilivyodhihirika katika Sura iliyotangulia kuwa katika usiku huu Malaika hushuka na amani hutawala.

Siku Kumi za Mwezi wa Dhil Hijjah (Mfungo Tatu):

Kama ilivyoelezwa mwanzoni mwa makala ni kuwa Jumanne ya leo ni moja ya masiku kumi ya katika mwezi mtukufu wa Dhul-Hijjah. Katika mwezi huu, siku kumi za mwanzo ni siku bora kabisa mbele ya Mwenyeezi Mungu ambazo amali yoyote inayotendwa humo ni yenye kupendwa mno na Mwenyeezi Mungu. 

Katika Hadithi iliyohadithiwa na Swahaba Ibnu Abbas (Mwenyeezi Mungu Amridhie), Mtume Muhammad (Mwenyeezi Mungu Amrehemu na Ampe Amani) Amesema:  “‘Hakuna siku ambazo amali njema zinazotendwa humo, zinapendwa mno na Mwenyeezi Mungu kama (amali zinazotendwa katika) siku kumi hizi.’ Yaani: Siku kumi za mwanzo wa mwezi wa Dhul-Hijjah (Mfungo Tatu). Wakauliza: Ee Mjumbe wa Mwenyeezi Mungu! Je, hata kuliko jihaad katika njia ya Mwenyeezi Mungu? Akajibu: ‘Hata Jihaad katika njia ya Mwenyeezi Mungu isipokuwa mtu aliyekwenda na nafsi yake na mali yake ikawa hakurudi na kimojawapo.’”  

Miongoni mwa yanayozipa ubora siku hizi kumi ni haya yafuatayo:

Katika siku kumi hizi ndipo ibada ya Hijja hutekelezwa na kwamba kama tulivyobainishiwa katika hadithi iliyotangulia hakuna siku ambazo amali zinazotendwa humo zinapendwa mno na Mwenyeezi Mungu kama amali zinazotendwa katika siku hizi.

Siku ya Ijumaa:

Siku ya Ijumaa ni siku yenye fadhila nyingi na ni sikukuu kwa Waislamu, ambapo Mtume Muhammad (Mwenyeezi Mungu Amrehemu na Ampe Amani) amewataka watakaokuja katika mkusanyiko wa siku ya Ijumaa waoge.

Miongoni mwa yanayoipa ubora siku ya Ijumaa ni kufunguliwa milango ya mbingu ili kuitikiwa maombi (Dua) za waja wa Mwenyeezi Mungu. Mtume Muhammad (Mwenyeezi Mungu Amrehemu na Ampe Amani) ametuambia kuwa siku ya Ijumaa kuna wakati ambao mja yeyote Muislamu atakayeomba katika wakati huo atapewa alichoomba.  

Pia Mwenyeezi Mungu ameifanya Swala ya Asubuhi ya siku ya Ijumaa kuwa ni Swala Bora na kukaja amri pia ya kufunga biashara na shughuli nyingine pale adhana ya Ijumaa inaponadiwa ili kwenda kutekeleza ibada ya Swala ya Ijumaa.

Nihitimishe makala hii kwa kutoa wito kwa Waislamu kunufaika na siku hizi bora kwa kukithirisha aina mbalimbali za ibada na kujitahidi kufanya matendo mema na kujiweka mbali na matendo mabaya, yakiwamo uzinifu, ulevi wa aina zote, ikiwamo dawa za kulevya, wizi, uongo, dhuluma za aina zote, ubaguzi wa aina zote, unyanyasi na unyayapaa wa aina zote, ufisadi, rushwa, fitina, majungu, hadaa na yote aliyotukataza Mwenyeezi Mungu Subhaanahuu wa Taalaa. 

Haya tukutane Jumanne ijayo In-Shaa-Allaah. 

Sheikh Khamis Mataka ni Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (Bakwata) na Katibu Mkuu wa Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania.