London
Na Ezekiel Kamwaga
Hapo zamani za kale, Simba iliwahi kuwa na mchezaji aliyeitwa Haruna Moshi ‘Boban’. Ni miongoni mwa wachezaji wakubwa wa Tanzania niliowahi kuwashuhudia kwenye ubora wao.
Akaenda Sweden kucheza Ligi Kuu. Riziki ikaisha, akarudi Tanzania kuchezea Simba. Baada ya muda, tukapata kocha mgeni. Sitamtaja jina.
Huyo kocha akawa na msaidizi wake. Akawa anawafanyisha wachezaji mazoezi wakati wote. Kuna kipindi Boban akagoma kufanya mazoezi ya kukimbia asubuhi. Kocha akamshitaki kwetu kwamba mchezaji anamdharau. Kikao kikaitwa.
Kwenye kujitetea, Boban akafunguka. Akasema Simba si timu ya riadha kwamba wachezaji kazi yao ni kukimbizwa tu. Akatoa mfano wa upungufu wa kiuchezaji wa baadhi ya wachezaji wa Simba ambao haufanyiwi kazi.
Kazi ni kukimbizwa tu. Na akasema kisayansi huwezi kuwakimbiza sana wachezaji wakati msimu umeanza na kuna mechi mfululizo. Mazoezi makali muda wake ni ‘pre-season’.
Boban akashinda hoja. Nitarudi hapa.
Kuna mchezaji mwingine, Victor Costa Nampoka ‘Nyumba’. Simba naye. Yeye alikwenda kucheza mpira wa kulipwa Msumbiji.
Aliporudi, kuna siku akanisimulia kuhusu timu moja ya Msumbiji. Akasema walikuwa wanajulikana kwamba wakikufunga bao moja halirudi. Kocha wao alikuwa anajua kupanga ngome.
Akanikumbusha yule Jose Mourinho wa Chelsea mara ya kwanza. Akikufunga bao moja mechi imekwisha. Victor alinifurahisha jambo moja – kwamba alijua ukiona timu ikikufunga ujue mechi imekwisha, basi hiyo ni kazi ya kocha. Matokeo ya namna hiyo hayaji hivi hivi.
Nataka kusema nini? Boban na Costa walitoka nje ya Tanzania na wakaona vitu tofauti. Ile Senegal unayoiona ikichukua ubingwa ina mchanganyiko wa Klopp, Tuchel, Pochetino, Spaletti, Moyes, Nagelsman na Alioua Cisse.
Wale wachezaji walio nje wanakuja na waliyojifunza kwenye klabu zao. Wanashea na wenzao. Wanashea na kocha wao. Ndivyo timu kubwa zilivyo.
Uzuri wa Senegal ni uzuri wa kocha na wachezaji. Tanzania itapiga hatua kubwa kisoka wakati wachezaji wetu wengi watakapotoka nje ya nchi kwenda kucheza mpira na kupata maarifa mapya.
Makocha wa kigeni wanapata taabu kufundisha wachezaji ambao ingawa wana vipaji, uwezo wao wa kupokea maarifa mengi kwa wakati mmoja si mkubwa. Wanatakiwa kulishwa kama dripu na kocha wa timu ya taifa hana muda huo.
Nakumbuka kumsikia Boban siku moja akimshauri Haruna Chanongo – wakati wote wakiwa Simba, kuwa apunguze kukaba kwa vile yeye ni winga na kazi yake kubwa ni kutengeneza mabao.
Na nikaona Chanongo akianza kutikisa nyavu mara kwa mara kuliko ilivyokuwa nyuma.
Kwa hiyo tusiseme tu kwamba makocha wazalendo wanafaa kwa sababu Cisse ametwaa ubingwa akiwa na Senegal.
Tuangalie je, wachezaji wake ni kina nani? Tusisahau pia Cisse naye ujanani alikipiga Ulaya kwenye soka la kimataifa.
Lugha…. Lugha… Lugha.
Kuna jambo moja la muhimu kwenye soka ambalo watu wanalichukulia poa. Jambo hilo ni umuhimu wa kufahamu walau lugha moja ya kimataifa kwa wananchi wa nchi fulani na wanamichezo wao.
Sisemi kwamba kujua lugha ndiyo kujua kucheza mpira. Lakini kama umeamua kuwa mpira uwe kazi yako, ni muhimu ukajifunza lugha moja ya kimataifa.
Kujua lugha moja ya kimataifa kunapanua wigo wako wa kupata taarifa na maarifa. Jitazame wewe mwenyewe na fikiria kama ungekuwa haujui kabisa Kiingereza, ungekuwa umekosa kujua vitu vingapi. Sasa muwazie mtu anayezungumza lugha tatu au tano.
Watu wanasema mbona Wabrazil hawajua Kiingereza au Kifaransa na mambo yao ni mazuri? Wanasahau kwamba wenzao wanazungumza Kireno ambayo ni lugha ya kimataifa na ina maarifa mengi sana.
Brazil ilianza kuwa na daktari kwenye timu yao ya taifa miaka ya 1960 kabla hata watu wa Ulaya hawajaanza.
Brazil walipoona wanafungwa tu miaka ya 1980; kwenye Kombe la Dunia mwaka 1982 walikuwa na kikosi kinachosemekana kuwa bora zaidi kushindwa kutwaa kombe, chini ya Kocha Tele Santana, wakakaa chini na kuja na mbinu mbadala.
Wakaibuka na nafasi wakaita ‘Volante’; yaani kiungo wa ulinzi. Jitu moja ngangari na lisilo na mambo. Zamani walikuwa hata kusogea uwanjani hawatakiwi lakini sasa wakatengenezwa.
Akaanza Carlos Dunga mwaka 1994 na wakatwaa Kombe la Dunia. Halafu wakaja akina Gilberto Silva na Lucas Leiva. Sasa unawaona Fabinho na Fernandinho.
Yaani wewe huko duniani ukitaka mambo yako yalainike mtafute Mbrazil akae namba sita.
Ili mradi asiwe Fred wa Man United.
Na walipoamua kwamba mpira wa kisasa unahitaji kipa kuanzisha mashambulizi, wao pia ndio walianza. Kwanza na Claudio Tafarrel na sasa watazame Alisson Becker na Ederson.
Liverpool kuna mtoto mwingine anaitwa Marcelo Pituluga. Wanadai anaweza kudaka kwa miguu.
Kwa hiyo msidanganyike na wanaosema eti Wabrazil hawajui Kiingereza wala Kifaransa. Wana lugha.
Na Kiarabu pia ni lugha kubwa duniani. Ukifanya utafiti wa haraka haraka, utaona kwamba nchi za Kiafrika ambazo walau zinakwenda Kombe la Dunia, ni za mataifa ambayo walau nusu ya wananchi wake wanazungumza lugha mojawapo katika zile zinazoitwa za kimataifa.
Mchezaji anayejua Kiingereza, ataangalia mpira na kusikiliza uchambuzi. Atajifunza. Yule ambaye hawezi ‘kurudisha pasi’ anaangalia mpira na wakati wa uchambuzi anabadilisha chaneli.
Na makocha pia hivyo hivyo. Na viongozi. Na mashabiki. Huwezi kutazama hata ‘You Tube’ na kuona nini unaweza kujiongezea. Suala la kujiongeza kwenye lugha nyingine haliepukiki.
Nimeamua kumulika haya mawili tu. Kuna mengi mengine lakini leo ni hayo; wachezaji wetu waende nje ili waje kuwa makocha wazuri zaidi wakimaliza mpira na wachezaji wawe imara zaidi kiufundi na kimaarifa na watu wa mpira ni muhimu kujifunza lugha ya pili.