Na Deodatus Balile
Kwa muda sasa nafuatilia siasa za Afrika na sehemu nyngine duniani. Leo nitajadili mataifa mawili; Marekani na Kenya. Nafuatilia kinachoendelea nchini Marekani. Nafuatilia kinachoendelea nchini Kenya. Narejea misingi ya uhuru wa mawazo na uhuru wa vyombo vya habari.
Nchini Marekani tangu umalizike uchaguzi mkuu wa Novemba, 2016, Rais aliyeshinda, Donald Trump amekuwa kwenye chetezo. Kutokana na sera zake ambazo wengine wanaziona ni za kibaguzi, wenye vinasaba na ubaguzi wanazifurahia, ila wenye kutamani amani duniani wanaona kuwa Dunia ipo katika kipindi cha majaribu, siasa za dunia zimeyumba.
Sitanii, ni muda mrefu kwa nchi kama Marekani kusikia kiongozi mkuu wa nchi akiingia katika vita ya wazi na vyombo vya habari. Imefika mahala Rais Trump akadai Shirika la Utangazaji la CNN haliiwakilishi sawa sawa Marekani kimataifa. Katika utamaduni usiozoeleka, CNN nao wakamjibu Rais Trump kuwa si kazi yao kuiwakilisha Marekani nje ya nchi, bali ni jukumu la Rais aliyeshinda uchaguzi.
Ukiacha hilo kuna vita kubwa nchini humo kati ya Rais Trump na wanaharakati wakiungwa mkono na Chama cha Democrat, wenye kuonyesha kuwa Trump alipata ushindi kwa kusaidiwa na Urusi. Kuna uchunguzi mzito unaendeshwa dhidi ya Rais Trump, familia yake na washirika wake juu ya ushirika wao na Urusi.
Sitanii, vyombo vya habari vya nchini Marekani vinaandika kila kitu bila kificho. Sina uhakika kama kwa hapa Afrika nchi zetu zina uvumilivu sawa na Trump au Marekani kwa ujumla. Wiki iliyopita joto la vyombo vya habari limemsukuma Trump kuchapisha taarifa ya siri ya CIA. Sasa baada ya kuichapisha umeibuka mgogoro mpya kuwa timu ya Trump imeihariri taarifa ya CIA.
CIA wameeleza kutoridhishwa kwao na utaratibu wa kuanika taarifa za siri za chombo hicho kikubwa cha uchunguzi hadharani. Democrat wamesema wao wanadhani hatua hiyo imechukuliwa kufifisha uchunguzi juu ya kazi iliyofanywa na timu ya Trump kwenye uchaguzi wa mwaka juzi kumsaidia ashinde. Sijasikia polisi wa Marekani, Trump au waziri mwenye dhamana na masuala ya habari akitishia kufungia gazeti, radio au TV zinazorusha matangazo ya mzozo huo wa hatari.
Sitanii, sasa njoo hapa kwetu Afrika. Nchini Kenya taifa hili mwanzo lilionyesha kujipambanua na kuwa taifa lenye kuheshimu uhuru wa vyombo vya habari na Mahakama. Haya yameshuhudiwa nchini Kenya hasa baada ya Katiba Mpya ya Mwaka 2010, ambayo Ibara yake ya 34 inatoa uhuru wa vyombo vya habari.
Kama hiyo haitoshi, tulishuhudia Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta akiheshimu uamuzi wa Mahakama baada ya Uchaguzi wa Agosti, mwaka 2017 uliompa ushindi uliotenguliwa na Mahakama. Raila Odinga aliyekuwa mshindani wake mkuu alidai ameshindwa kimizengwe na mahakama ikathibitisha hivyo na kutengua uchaguzi. Kenya ikarudi kwenye uchaguzi baada ya siku 60.
Sitanii, leo ikiwa imepita miezi takribani minne tangu Uhuru aithibitishie dunia kuwa yeye ni nguli wa kuheshimu uhuru wa Vyombo vya Habari, wiki iliyopita ametenda kinyume. Serikali yake imezima mitambo ya kurusha matangazo ya Citizen TV, Inooro TV, NTV, na KTN News kwa kutangaza shughuli ya Odinga kujiapisha kuwa Rais wa Wananchi.
Nimejaribu kupitia sheria za Kenya, hakuna kosa linalotamkwa na sheria za Kenya kwa mtu kujiapisha kuwa Rais wa Wananchi. Ikiwa Waziri wa Usalama wa Ndani, Fredy Matiangi anataka hili liwe kosa, anapaswa kupeleka sheria bungeni ikazuia kuapisha mtu kuwa Rais wa Wananchi. Sheria ya Kenya kama ilivyo hapa kwetu inazuia mtu kujiapisha kuwa Rais wa Jamhuri ya Kenya. Ndiyo maana Odinga si mjinga. Hakuuingia mtego huo.
Kwa upande mwingine, Wakenya na dunia inayo haki ya kuona kilichokuwa kinaendelea kwenye Viwanja ya Uhuru jijini Nairobi. Ni kazi ya vyombo vya habari kuuhabarisha umma. Ni kwa masikitiko Serikali ya Kenya imeamua kuvifunga vyombo hivyo, na hata kuamua kutotii amri ya mahakama iliyoelekeza vifunguliwe kwa siku 14 wakati kesi ya msingi inaendelea.
Kenya sasa imeingia kwenye mtego wa kurejesha ufalme. Rais Trump pamoja na upungufu wake, hajachukua hatua ya kufungia vyombo vya habari bali anafafanua na kukanusha inapobidi. Najiuliza nini kinaitafuna Afrika? Viongozi wetu wanaficha nini kwa kufungia uhuru wa vyombo vya habari na watu kutoa mawazo yao?
Kinachotokea Kenya kipo mataifa mengi ya Afrika. Hii inaleta fikra kuwa enzi za Ufalme zinarejea kwa kasi Afrika kwa kiwango ambacho Mfalme alikuwa anafahamu kila kitu na kamwe ilikuwa hakosolewi. Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alitwambia, TUJISAHIHISHE. Naamini wakati umefika, TUJISAHIHISHE.
Ends…