Sijasikia ACACIA wakijitetea, bali namsikia Mtanzania mwenzetu Tundu Lissu katika maandishi na video zinazoenezwa mtandaoni kwa kasi ya ajabu akiwatetea kwa nguvu na kwa pumzi zake zote. Ni kuhusu mchanga wenye madini uliozuiwa na Serikali bandarini. Amezungumzia mambo ambayo nitayajibu hapa kwa lengo kubwa kabisa la kutaka Watanzania wafahamu.
Je, sheria inasema mchanga ni mali ya ACACIA?
Lissu anasema kuwa kwa mujibu wa sheria mchanga ule ni mali ya ACACIA na hivyo Serikali kuuzuia ni sawa na kuzuia mali ya mtu. Kuhusu hili sijui amezungumzia sheria ipi? Katika Sheria Namba 14/2010 Sheria ya Madini hakuna jambo la namna hii kama Tundu Lissu anavyotaka kuliweka.
Hakuna popote ilipoandikwa kuwa mchanga wote unaochimbwa ni mali ya ACACIA. Na hili linajulikana kwani hata leseni za uchimbaji hutolewa kwa ajili ya uchimbaji madini na siyo umiliki wa ardhi. Ardhi ambayo hujumuisha mchanga hubaki mali ya Taifa.
Lakini pia katika hilo hilo lazima ieleweke kuwa hawakuwa wakichukua mchanga kwa sababu ni mali yao kama Lissu anavyosema. Hata wao hilo wanalikataa. Wanasema wanalazimika kubeba mchanga kwa kuwa hapa Tanzania hakuna kiwanda/mtambo wa kuchenjua mchanga na kupata wanachokitaka. Hawasemi walikuwa wanachukua mchanga kwa sababu ni mali yao, hapana. Ni utetezi wa Watanzania wenzetu unaosema mchanga ni mali yao.
Je, Acacia wametenda kosa lolote?
Lissu na kundi lake wanawatetea ya kuwa hawajatenda kosa lolote. Ni hivi, ukweli ni kuwa kuna makubaliano maalumu kati ya Acacia na Serikali kuwaruhusu kuchukua mchanga kwenda kuuchenjua katika kipindi ambacho Serikali itakuwa haijajenga mtambo wake.
Hata hivyo, lazima ieleweke kuwa makubaliano haya yanakwenda sambamba na wajibu wa kisheria wa kutoa taarifa sahihi kuhusu uzito wa kile wanachochukua pamoja na sampuli zilizomo.
Kuthibitisha kuwa wajibu huu upo, ndio maana mchanga huo hukaguliwa, na wao hukubali ukaguliwe na TMAA, TRA, nk. Mchanga haukaguliwi ili kujifurahisha, hapana. Unakaguliwa ili kujua uzito na sampuli za kile kinachochukuliwa.
Basi, hatua ya wao kukubali kukaguliwa na mamlaka hizi kwa malengo haya ya kujua wanachukua nini inathibitisha hata wao kuutambua wajibu wao wa kusema ukweli kuhusu uzito na sampuli za kile wanachobeba.
Sasa swali ni kama wajibu huu upo na wao wanautambua kwa kiwango hiki; je, kuukiuka kwa kudanganya kuhusu uzito na sampuli ni kosa au si kosa? Akili ya kawaida tu ya mtu ambaye hata siyo mwanasheria itapata jibu. Halafu anatokea Mtanzania anasema hawajafanya kosa lolote.
Lakini pia ukidanganya kuhusu uzito na sampuli utatoa mrahaba ulio chini ya kiwango, chini ya kile ulichotakiwa kutoa. Bado baadhi ya Watanzania wenzetu wanasema hilo nalo si kosa! Inasikitisha sana.
Makala yaliyopita nilieleza kwa urefu kosa la udangayifu hapa kwetu na huko kwenye mahakama za kimataifa. Muda huu itoshe tu kusema kuwa, jamani udanganyifu ni kosa (fraud/deceitful).
Na ni kosa pote mahakama za ndani (local courts) na katika hizo za kimataifa (International Arbitral Tribunal). Na hakuna shaka imethibitika makosa haya wameyatenda. Haya iko wapi hiyo kesi inayopigiwa debe kwa nguvu zote kuwa lazima tunashindwa?
Je, ni kweli ripoti ya Mruma ni takataka kama inavyoitwa?
Lissu anaiita Ripoti ya Tume ya Mruma- takataka, na kusisitiza kwa Kiingereza kuwa ni ‘rubbish’. Kwanza niseme kuwa maneno haya ni ya dharau kubwa kwa Profesa Mruma na wasomi wote aliokuwa naye kwenye kamati. Lakini pia ni dharau kwa rais aliyeunda kamati hiyo.
Kwa mtu mstaarabu na msomi ingetosha tu kusema ripoti ya Profesa Mruma haina ukweli, au haina mashiko, au si ushahidi mzuri, n.k. Kuiita takataka si tu ni uhuni, bali pia ni kudhihirisha kiwango cha hila na chuki aliyonayo kwa kile alichofanya rais.
Wakati mwingine waweza kuwa na hoja nzuri, lakini ukaiharibu kwa lugha. Lazima ifike hatua tujue kuwa staha katika kukosoa ni sehemu ya msingi katika misingi inayojenga demokrasia.
Niseme tu kuwa si kweli hata kidogo kuwa ripoti ya Profesa Mruma haina maana kiushahidi. Ripoti hiyo ni ushahidi muhimu sana tena sana kuthibitisha udanganyifu wa Acacia. Kama leo kesi ya udanganyifu inasimama, ni ripoti ya kisayansi kama ya Mruma itakayotumika kuthibitisha uwepo wa udanyifu.
Lakini pia sisi huo ndio ushahidi wetu tuliokusanya, na wao kama wanao ushahidi mwingine unaosema hawajadanganya, basi watauleta- shida iko wapi? Iko wapi haja ya kuiita kamati iliyopata mamlaka ya rais takataka –‘rubbish’? Hakuna kabisa.
Je, tunayo matatizo ya sheria na mikataba kama wanavyodai?
Ndio tunayo. Yako mara mbili. Kwanza, sheria kama sheria kwa maana ya maudhui. Pili, sheria kwa maana ya usimamizi wake. Sheria kwa maana ya maudhui, yako maeneo yanayohitaji marekebisho na siyo sheria nzima.
Sheria hiyo ya Madini namba 14/2010 inaweza kurekebishwa maeneo yanayohusu leseni za madini, haki za kumiliki madini na ardhi yake, mrahaba na kodi na ile sehemu ya 10 inayoongelea adhabu, nk. Huo ni upande wa maudhui.
Kuhusu sheria upande wa usimamizi. Tatizo la usimamizi wa sheria ni kubwa kuliko upungufu ulio katika sheria yenyewe (maudhui). Kwa mfano, hii sheria iliyopo tunayosema ina upungufu, hakuna popote inaposema tuibiwe hata hicho kidogo tunachotakiwa kupata. Lakini tunaibiwa. Tatizo ni nini kama si usimamizi?
Hata tukitunga hiyo sheria mpya na kila mtu akaikubali, kama hatuna mtu wa kuisimamia ni kazi bure. Kwa hiyo tunahitaji mtu wa kusimamia sheria kuliko tunavyohitaji sheria yenyewe. Na dalili zote zinaonyesha kuwa mtu huyo tayari tumempata na sasa tunaanza kuondokana na tatizo hili. Mikataba nayo halikadhalika inahitaji kupitiwa kimaudhui pia ipate msimamizi.
Tatizo la akina Lissu katika hili ni kutaka kutwambia kuwa kwa kuwa tuna matatizo ya sheria na mikataba, basi haturuhisiwi kuzuia na kudhibiti hata wizi ambao tumebahatika kuugundua na kuuona. Ni upotofu na bila shaka ni hapana. Wizi huu tunaushughulikia na hayo mengine ya sheria na mikataba nayo muda unakuja yatashughulikiwa.
Kitendo cha rais kuunda kamati ya pili ya wachumi na wanasheria ni ushahidi kuwa tayari tatizo la sheria na mikataba limeanza kumulikwa rasmi.
Je, mchanga kuhakikiwa na TMAA kunafuta udanganyifu wao?
Lissu anasema kuwa mchanga huo ulihakikiwa na TRA, TMAA, n.k na kuwa zote hizi ni taasisi za Serikali na hivyo kuwaambia tena wameiba ni kuwakosea. Hivi kwani tunaposema kosa la ACACIA ni kutufanyia udanganyifu maana yake nini?
Maana yake si ni kwamba waliidanganya Serikali? Na Serikali si ni TRA, TMAA, nk? Sasa maajabu yako wapi? Kosa la ACACIA ni hilo kuzidanganya hizo mamlaka za Serikali wakati wa ukaguzi.
Kwa hiyo tunaposema wametuibia maana yake walizidanganya mamlaka hizo. Sisi hatujui walitumia njia gani, iwe rushwa au vinginevyo- sisi hatujui. Tunachojua ni kwamba tulichokuta wanachukua ni tofauti na kile walichosema wamechukua; jambo ambalo ni kosa. Iko wapi hoja hapo?
Mwisho ni kuwa tuache kupinga na kulalamikia kila kitu. Hili hatutaacha kulisema hata zipite karne 100. Madhali linaendelea kuwepo, tutaendelea kulikemea. Pia kurejearejea historia mara mwaka 1998 tulishauri hivi, mara vile nk. haina nafasi wala msaada kwa sasa.
Tumeshampata mtu wa kutushika mkono. Kazi yetu ni moja tu- kuungana naye kwa kuchangia utaalamu ili tutoke hapa tulipo. Kama huna utaalamu hata kumpa moyo nao ni mchango. Kama yote huwezi ni heri kukaa kimya kuliko ukabwabwaja.
Maajabu ni kutumia miaka zaidi ya 18 ukilalamikia jambo, halafu akatokea mtu wa kulitatua jambo hilo, badala ya kushirikiana naye, wewe ukafungua tena mlango mwingine wa malalamiko kulalamikia tena kile kile ulichopigania kishughulikiwe. Ni maajabu yanayostahili kuingia kwenye maajabu ya dunia!
Mwandishi wa makala hii, Bashir Yakub, kitaaluma ni mwanasheria. Anapatikana kupitia namba 0784482959.