Simba, Yanga lazima zibadilike
Na Charles Mateso
CECAFA Senior Challenge Cup ya mwaka huu imekuja na maneno mazuri sana kutoka kwa wadau wa soka wa Kenya.
Wameamua kutuambia ukweli baada ya miaka kadhaa ya Tanzania kuhangaika na wachezaji kutoka Kenya na Uganda.
Wadau wa soka wa Kenya kupitia taarifa zao za habari wanatuambia tuandae wachezaji wetu. Hilo si neno baya hata kidogo, ndio ukweli wenyewe wa mambo.
Fikiria, kuna rundo kubwa la wachezaji kutoka Kenya ambao baada ya misimu michache hupungua kiwango na kuamua kurudi kwao au kwenda kucheza katika ligi za mataifa mengine. Wakenya wanatuambia tufike mahali tuanze na sisi kuuza wachezaji wetu kwao. Hilo si tusi, bali ni ukweli wenyewe unaotakiwa kusemwa na kuibua fikra miongoni mwa wadau wa karibu wa soka la Tanzania.
Wakija wachezaji watatu kutoka Ligi Kuu ya Kenya hakuna Mtanzania hata mmoja anayekwenda kucheza katika ligi yao ndani ya msimu huo huo. Wanakuja Wakenya na Waganda kila mwaka na sisi wala hatujiulizi kwanini ligi za kwao haziwapambi hata hao wachezaji wetu wachache wanaocheza katika ligi zao.
Tuko tayari kumzungumzia kwa kumpamba mchezaji wa Gor Mahia ambaye hana hata misimu mitatu uwanjani, lakini hatutumii nguvu kubwa katika kuuzungumzia udhaifu wa wachezaji wetu wengi, tena wenye umri mdogo kama wa huyo kijana tunayemsifia.
Tuanze kwa kuwapenda wachezaji wetu kwanza, halafu ndipo mapenzi hayo tuyagawe kwa wachezaji wa kigeni wanaokuja kuchuma fedha na kuondoka zao. Timu zetu ni kama ziko pale pale licha ya uwepo wa mara kwa mara wa wachezaji kutoka mataifa ya jirani.
Wakenya ni kama huwafanyia tathmini wale wachezaji wao wanaokuja kucheza katika Ligi Kuu yetu, wamegundua hakuna cha maana zaidi ya fedha. Yanga, Simba na Azam FC wanaona sifa kupamba kurasa za michezo kwa kutumia picha za wachezaji wapya kutoka Kenya na Uganda.
Lakini uwakilishi wa timu zetu kwenye michuano ya ngazi ya bara bado hauna jipya licha ya mbwembwe nyingi za kwenye kurasa maalumu kwa ajili ya michezo. Yanga watafungwa na Al Ahly hapa hapa uwanjani na ndani ya uwanja watakuwepo wachezaji wawili au watatu kutoka Kenya.
Simba watachapwa na UD Songo hapa hapa Tanzania na katika kikosi cha kwanza atakuwepo Mkenya mmoja na Mganda mmoja! Azam FC watafungwa na El Merreikh na kikosi chao kitakuwa na Mganda au Mkenya mmoja na tunapotolewa nje ya michuano sababu za kufanya vibaya wala haziwajumuishi wachezaji wa kigeni tuliowanunua kwa fedha nyingi.
Tutakuwa na sababu nyingi za nje ya uwanja na si kwamba Wakenya au Waganda wametuchoka, bali wameamua kutuambia ukweli kwamba ligi yetu bado haina kitu kipya kwa wachezaji wao, zaidi ya uhakika wa fedha na umaarufu.
Wakati huo Kipre Tcheche ndiye mshambuliaji ambaye uwepo wake unatoa matumaini ya ushindi wakati Azam FC inapokutana na timu za viwango vya juu barani Afrika. Azam FC pamoja na kuwa na benchi la ufundi ambalo ni kubwa, bado shabiki anashindwa kuuona mtiririko wa uchezaji mpira wenye kujiamini kwa dakika zote tisini.
Kila mwaka viongozi wa klabu zetu kubwa wanaona ufahari kusajili wachezaji kutoka Kenya na Uganda, huku hakuna tathmini ya kina inayofanywa kuhusu wachezaji wetu na udhaifu wao ili waweze kwenda Kenya na Uganda na kutengeneza fedha za maana na baada ya hapo wafikirie kucheza soka nje ya Bara la Afrika.
Patrick Aussems
Kocha aliyetimuliwa Simba wakati anaondoka alizungumza nami kitu kimoja na kuniambia kuwa kuna kazi kubwa kuifikisha Tanzania katika mafanikio ya soka.
“Kila kocha atafukuzwa, wanataka mpira wa jukwaani, sawa, lakini umewekeza nini huku chini? Una watu ambao wanaweza kufanya kile unachotaka?
“Mpira si kipaji tu, bali una mambo mengi ambayo yanahitaji mwongozo, lakini Tanzania ina uwezo mkubwa wa kufika mbali iwapo ikiamua kutoka hapa ilipo,” anasema.
Mwinyi Zahera
Kocha wa zamani wa Yanga ambaye naye alifungashiwa virago vyake, anakiri aliamua kuwa mkweli ili kusaidia soka la Tanzania lakini akaonekana ni adui namba moja.
“Bila ukweli hakuna kitakachoendelea, hizi sifa zisizo na maana wala hazisaidii, lazima mfumo wote wa soka la Tanzania ufumuliwe na kuandaliwa upya, tusitegemee matokeo ya muda mfupi, iwekwe mikakati maalumu ya kutoka hapa ilipokwama,” anasema.
Mo Dewji
Labda Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Simba, Mohammed Dewji Mo anaweza kuanza nalo kama mwenyewe alivyotanabaisha katika mkutano mkuu wa wanachama.
Mo anadai anataka kuhakikisha Simba inakuwa na falsafa yake huku akiziimarisha timu ya wakubwa na zile ndogo za vijana mpaka wanawake ili kufikia malengo anayotaka.