Moja ya majukumu yangu nikiwa Butiama ni usimamizi wa kutangaza Kijiji cha Butiama kama kivutio cha utalii ndani ya programu ya Utalii wa Utamaduni inayoratibiwa na Bodi ya Utalii Tanzania.
Butiama inajumuisha vivutio vya utalii vya aina mbalimbali, ikiwa ni pamoja na vile vya utamaduni wa kabila la Wazanaki, vivutio vya mazingira, na – pengine muhimu kwa wageni wengi – kivutio cha historia.
Historia inayowavutia wageni wengi kutembelea Butiama ni ile ya mmoja wa waasisi wa chama cha Tanganyika African National Union (TANU), wa Tanganyika, na wa Tanzania, na hatimaye wa Chama Cha Mapinduzi (CCM). Nazungumzia historia ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Mwalimu Nyerere alizaliwa Butiama na, kwa maelekezo yake mwenyewe kabla hajafariki, amezikwa Butiama. Kwa wageni wenye shauku ya kufahamu ni wapi alipotokea na wapi hatimaye alirudi, kutembelea Butiama kunawaongezea ufahamu wa kiongozi huyu aliyekuwa rais wa kwanza wa nchi yetu – iite Tanganyika au Tanzania kulingana na fasili yako ya historia.
Butiama ipo Makumbusho ya Mwalimu J.K. Nyerere inayosimamiwa na Makumbusho ya Taifa; sehemu yenye maelezo na vielelezo juu ya maisha ya Mwalimu Nyerere na matukio muhimu ya maisha yake, kuanzia shuleni, nyakati za kusaka Uhuru kutoka kwa wakoloni Waingereza, pamoja na harakati za kuikomboa Tanzania wakati wa Vita ya Kagera dhidi ya majeshi ya Idi Amin.
Mwitongo, eneo la makazi ya Mwalimu Nyerere na eneo ambalo amezikwa, pia ni kivutio muhimu kwa wageni wanaotembelea Butiama. Ni eneo ambako yalikuwa makazi ya Mtemi Nyerere Burito, baba yake Mwalimu. Kwa kifupi Mwitongo ni eneo lililosheheni vivutio vya utamaduni na vya historia.
Katika mazingira haya na kwa nafasi yangu kama Mratibu wa Butiama Cultural Tourism Enterprise sikuona cha kusimulia nilipopigiwa simu siku chache zilizopita kutoka kwa mtia nia Makongoro Nyerere kuniarifu kuwa mtia nia Profesa Mark Mwandosya atatembelea Butiama siku hiyo. Siku moja kabla yake tulitembelewa na mtia nia Edward Lowassa na safari yake ilizua mjadala mdogo kwenye baadhi ya mitandao ya jamii niliyotembelea. Ujio wa Mheshimiwa Lowassa ulizua cha kusimulia.
Kuna watu ambao kutokana na sababu za kisiasa (bila kumaanisha kuwa sababu za kisiasa hazina maana au si hoja halali) walitoa maoni kuwa kuna baadhi ya watia nia hawastahili kutembelea Mwitongo. Nimeona maoni haya yanahitaji jibu kwa sababu moja tu: Kazi ya msingi ninayosimamia ni kupokea wageni wanaotembelea Mwitongo na naamini ni muhimu kwa wale wanaopanga kufika huku siku zijazo kusikia ujumbe wa moja kwa moja kutoka Mwitongo.
Kwanza, na muhimu kabisa kwa taratibu za vivutio vya utalii wa utamaduni, eneo la Mwitongo ni eneo la wazi na linatembelewa na mtu yeyote, awe mtia nia au mpita njia. Hatulioni kama eneo la kisiasa au ni kuwa ni eneo la aina fulani tu ya wanasiasa, hata kama wanasiasa wanapendelea kutembelea hapa. Kwetu sisi jambo la msingi ni kutunza kumbukumbu za kitamaduni na kihistoria za eneo hili.
Watia nia wote hawa ni wanachama wa Chama Cha Mapinduzi. Kwa sababu ambazo baadhi ya wachambuzi wamefafanua, muasisi huyu ambaye alistaafu miaka zaidi ya 29 iliyopita na ambaye amefariki karibia miaka 16 iliyopita, bado leo hii tunazungumzia uongozi wake. Wapo wanaozungumzia vibaya uongozi wake, lakini tumeshuhudia kwa watia nia kuwa, kwa yale tunayoyasikia, wanaomtaja wanamtaja kwa mazuri.
Kwetu sisi tunaopokea wageni Butiama tunapaswa kuwa wanyenyekevu na kutambua kuwa heshima hii, hasa kama ni ya dhati na inatoka moyoni, tunaipata kwa sababu yake; sisi kazi yetu kubwa ni kukaribisha na kupokea heshima hiyo.
Wanaofikia uamuzi wa kutembelea Mwitongo kwa muasisi wa chama chao, wajiandae kukumbana na ukarimu wa wakazi wa Butiama na wa Mwitongo. Ni sehemu ambayo watakuta watu wanaosikiliza zaidi wageni kuliko wale wanaotaka kusikilizwa na wageni.
Lakini kusema kuwa tunasikiliza zaidi kuliko kuongea hakumaanishi kuwa hatuna maoni yoyote juu ya tukio muhimu kabisa la kisiasa la mwaka huu – Uchaguzi Mkuu wa Oktoba. Kwetu sisi wenyeji tunasema siasa za Tanzania zinaishia kwenye geti la Mwitongo, ndani ya uzio wageni wanapokewa kama Watanzania, ingawa hatukatai kupokea ujumbe wao wa kisiasa. Tukitoka nje ya uzio, basi tunazitosa pingu za maoni yetu na tunaendelea kujadili yale ambayo tunaamini ni muhimu katika mchakato wa kupata rais wa tano wa Tanzania. Binadamu ambaye hana maoni hayupo.
Lililo kweli kwa wana-CCM ni kweli kwa kila mgeni anayatembelea Mwitongo. Sehemu kubwa ya wageni wa Mwitongo si wanasiasa, lakini hata wale wanaotokana na vyama vingine zaidi ya CCM wanakaribishwa kwa ukarimu ule ule wa Kitanzania. Mgeni akishakula yuko huru kuongea. Kama hana la kusema, tunamshukuru kwa kututembelea.
Binadamu ambaye anafahamu kwa hakika nani atakuwa rais wa tano wa Tanzania bado hajazaliwa, na hatazaliwa. Kuchagua kiongozi anayefaa kuiongoza Tanzania katika mazingira na changamoto zilizopo sasa ni kazi muhimu sana na ni wajibu ambao kila mpigakura anapaswa kushiriki. Lakini hata katika utaratibu ambao ni mzuri kwa kila kipengele bado hutokea wapigakura kumchagua rais bomu. Na akishachaguliwa linakuwa bomu la wote; la waliomchagua na wale waliompinga kwenye kura. Wote tutaanza kumuita “Mheshimiwa Rais”.
Mungu akipenda, baada ya Oktoba Watanzania tutachagua kiongozi bora kuliko wote waliyojitokeza na ataapishwa awe rais wetu wa tano. Mungu akipenda kuna siku na yeye atatembelea Mwitongo na nitapata fursa ya kumkaribisha na kumwongoza kwenye baadhi ya vivutio vya utamaduni na vya kihistoria vilivyopo Mwitongo. Napenda kuamini hatakuwa bomu.