Tunatambua na kuheshimu haki ya kila Mtanzania ya kushiriki siasa.
Siasa katika mfumo wa vyama vingi zina changamoto ambazo Taifa lisipokuwa makini linaweza kujikuta watu wake wakigawanyika.
Kinachoendelea sasa katika vyuo vikuu si kitu cha kufumbiwa macho. Mamia kwa maelfu ya vijana wamegawanyika kiitikadi.
Wiki iliyopita tumeshuhudia wakigawanyika kwenye mahafali yao kwa misingi ya kiitikadi. Kwa maneno mengine, mfuasi wa Chama Cha Mapinduzi haruhusiwi kujumuika na wafuasi wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa). Vivyo hivyo, Ukawa hawaruhusiwi kuonekana karibu na shughuli inayowahusisha wana CCM.
Ingawa jambo hili linachukuliwa kama dogo, sisi JAMHURI tunaona ni la hatari kwa mustakabali wa umoja na mshikamano wa Watanzania.
Tunapokuwa na mahafali yanayohusisha vijana wa itikadi fulani pekee, tunajenga Taifa la vijana wasiokuwa wamoja na kwa njia hiyo tunakaribisha uvunjifu wa tunu ya mshikamano iliyotengenezwa na waasisi wetu.
Vijana katika vyuo vikuu wana haki ya kushiriki siasa kulingana na utashi wao. Maeneo ya kuendesha siasa yawe nje ya vyuo.
Tukikaribisha utengano huu kwa upofu wa kuamini kuwa ni haki ya watu wenye itikadi na malengo yanayofanana kuketi pamoja, tutakuwa tunafanya makosa.
Makosa hayo yanakuwa makubwa zaidi pale maeneo ya umma kama vyuo vikuu yanapovikwa taswira za kiitikadi.
Mwenendo huo unaweza kutufanya siku moja tujikute vijana wetu wakidai kupangwa katika madarasa kulingana na itikadi zao.
Kama alivyosema Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, dhambi ya ubaguzi ikishatendwa, itaendelea tu. Tunaweza kutoka kwenye siasa na kujikuta tukiingia kwenye imani za kidini. Tunaweza kufika mahali pa madhehebu fulani kupinga kusogelewa ma madhehebu fulani.
Tunaweza kujikuta dhambi hii ya ubaguzi na utengano ikitupeleka hadi kwenye migawanyiko ya kimikoa, kikanda na pengine kikabila. Tunaweza kujikuta watu wa itikadi fulani wakikataa kulazwa au kutibiwa katika hospitali fulani kwa sababu mmiliki ni wa itikadi tofauti.
Serikali ya Awamu ya Tano ilione jambo hili kama ufa hatari unaolinyemelea Taifa letu. Siasa zisiruhusiwe kutumika kwa namna hii inayoendelea sasa katika vyuo vikuu. Wale wanaoona ni busara kukutana kiitikadi, wakusanyike kwenye viwanja vyao nje ya maeneo ya kitaaluma.
Mahafali yenye vimelea vya kiitikadi ni hatari ambayo wanaoitakia mema nchi yetu wanapaswa kuungana kuikabili mapema. Vyuoni ni sehemu ya kusoma, na si kubaguana kiitikadi. Serikali ichukue hatua sasa. Isisubiri mambo yaharibike.