Ma Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma

Serikali imesema si sahihi na hakuna utaratibu wa kufanya ukaguzi katika kila kaya ili kubaini kama zinazotumia kuni au mkaa na badala yake kinachotakiwa ni kufuatilia na kuhakikisha misitu haikatwi ovyo.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Kibamba Issa Mtemvu aliyetaka kujua kauli ya Serikali kuhusu madai ya kuwatafuta watumiaji wadogo wa mkaa kwenye makazi.

Amesema kuwa ukimfuata mwananchi mmoja mmoja huwezi kujua kama mkaa huo alionao una kibali au hauna hivyo ametoa wito kwa taasisi za Serikali kurejea masharti ya matumizi ya kuni na mkaa.

Aidha, Mhe. Dkt. Kijaji amesema kuwa ili kuhakikisha kila mwananchi anamudu gharama za nishati safi ya kupikia ikiwemo ya gesi, Serikali inashirikiana na wadau mbalimbali katika kupunguza bei za nishati hiyo na vifaa vyake.

Halikadhalika, amesema kuwa kwa sasa Serikali inaendelea kufungua milango kwa wawekezaji wa nishati hiyo kuwekeza katika nishati safi hiyo rafiki kwa mazingira ili kulinda misitu isiendelee kukatwa.

Katika jibu la msingi la Mbunge Mtemvu, Mhe. Dkt. Kijaji amesema Serikali imeandaa na inatekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024-2034) ambao unatoa mwelekeo wa nchi wa kuhamia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Mkakati huu unalenga kuhakikisha angalau asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034 na kupunguza gharama za nishati safi, vifaa na majiko sanifu ya kupikia.

Halikadhalika amesema kuwa Mkakati umelenga kuimarisha upatikanaji wa malighafi na miundombinu ya uhakika ya nishati safi ya kupikia; kuhamasisha uwekezaji katika nishati safi ya kupikia.

Katika kuhakikisha jamii inapata uelewa wa kutosha kuhusu umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia na kuachana na kuni na mkaa, Mhe. Dkt. Kijaji amesema Serikali inaendelea kuta elimu ili kupunguza ukataji wa miti

Vilevile, amesema kuwa Serikali kupitia Mkakati wa Nishati Safi imeweka kipengele cha kuona uwezekano wa kushusha bei ya nishati safi ambayo pia inakwenda sanjari na kuweka ruzuku katika eneo hilo.

Amebainisha hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Ilemela Mhe. Dkt. Angeline Mabula aliyeuliza Serikali haioni uwezekano wa kutoa ruzuku katika mitungi ya gesi.

Please follow and like us:
Pin Share