Wake wenza wawili waliishi katika makazi tofauti na mume wao katika mji mmoja. Kila mmoja alijitahidi kumtunza mume na kumuweka katika maisha ya furaha, upendo na utulivu pasi na mwenzake kujua mapenzi anayepewa mume.
Mke mkubwa na mke mdogo kila mara walipokutana katika harusi, ngoma au kwenye msiba walioneshana makeke, kejeli, msuto hata kuonesha dalili za kutaka kupigana. Sababu ni kila mmoja alimuona mwenzake si chochote. Na wote walipenda kusikiliza uheke kutoka kwa ndugu, marafiki na majirani. Hayo yalikuwa ni sehemu ya maisha yao.
Kwa kudura za Mwenyezi Mungu, mke mdogo alifariki dunia. Alizikwa kwa heshima na upendo mkubwa na mume wake, ndugu na jamaa. Siku moja mke mkubwa na shemeji yake walipokuwa matembezini walipita njia iliyo pembeni na makaburi.
Mke mkubwa jicho lake lilitua kwenye kaburi lililojengwa kwa ustadi na kusanifiwa na marumaru zenye kuvutia jicho la mtu yeyote apitaye njia ile. Alisema, “Kaburi lile limejengwa vizuri na linapendeza. Aliyejenga ni fundi kweli kweli.”
Shemeji yake alimjibu, “Kweli. Hilo ni kaburi la aliyekuwa mke mwenza wako na limejengwa na mume wako.” Ghafla mke mkubwa alijibu, “Ndiyo maana ukuta mmoja umepinda.” Alilitia kasoro. Kasoro ile si ya bure ina chochote.
Neno ‘chochote’ lina maana ya ‘isiochagua’. Katika matumizi chochote inaweza kuwa hakuna kitu au kuna kitu. Hana chochote kwa maana yu mweupe. Ana chochote kwa maana ana jambo. Leo nawasikia mara kadhaa baadhi ya watu wakiwamo viongozi wa siasa na watumishi wa umma wanavyobeza na kukashifu kazi zinazofanywa na mamlaka mbalimbali zikiwamo mashirika na Serikali.
Wapo wengine wanasifu na kufurahia kazi zinazofanywa na mamlaka husika. Wao wanaona kuna chochote na wanapenda kuona kasi ya utendaji iwe maradufu. Ni vyema ikaeleweka pasipo na chochote kuna chochote. Tusipuuze, tujali.
Nimepata kusikia pia watu wakisema CUF na wapinzani kule Zanzibar hawana chochote ni fujo zao tu! Hawataki kushiriki marudio ya uchaguzi Machi 20, kwa madai ni uchaguzi batili. Ingawa wanaonekana hawana chochote mbele ya ZEC na Serikali ya Zanzibar, ukweli wana chochote wasipuuzwe.
Chadema na baadhi ya raia wanaona hakuna chochote kinachofanywa na Rais Dakta John Magufuli katika dhana yake ya kutumbua majipu na kupambana na wala rushwa na mafisadi, ukweli Magufuli ana chochote. Tutafakari.
Chama Cha Mapinduzi (CCM) na mashabiki wake msidharau eti Chadema walikutana Mwanza wiki iliyopita hawana chochote zaidi ya kupanga mikakati ya kufanya maandamano na fujo dhidi ya Serikali! Jamani, wana chochote hao! Umakini hauna budi kuzingatiwa.
Mwaka jana, Oktoba 25 kwenye Uchaguzi Mkuu, CCM waliwaona Ukawa si chochote. Wakati wa kupiga kura na kutangaza matokeo CCM walitambua kuwa kumbe Ukawa walikuwa na chochote. Naamini CCM wamejifunza, na lililo mbele yao ni kujipanga mwaka 2020.
Hadi leo kuna baadhi ya watumishi wa umma, majangili, wauza dawa za kulevya, wala rushwa, mafisadi, matapeli na wengine wengi wa aina hiyo katika kuhujumu uchumi, wanaamini hakuna chochote kinachofanywa na Serikali ni nguvu ya soda tu. Itashindwa. Sawa! Hata hiyo nguvu ya soda kumbuka ina chochote.
Mke mkubwa aliamini kuwa mke mdogo si chochote na wala hakupendwa na mume wao. Lakini alishtuka na kushangaa alipoambiwa ujenzi na usanifu wa kaburi lile ulifanywa kwa mikono ya mume wake. Ndipo alipotambua kumbe mke mdogo alikuwa na chochote.
Hiyo ni baadhi ya mifano niliyotoa kuonesha chochote ina muhimu wake. Linapoundwa jambo daima kuna chochote – iwe katika michezo, utani, siasa na kadhalika ndani yake kuna kitu na kitu hicho kinaweza kuwa chanya au hasi chenye sura ya chochote.
Iwapo chochote hicho kina chanya, kina salama ndani yake na kwetu jamii. Kwa sababu itaishia kuzungumzwa, kutaniana na kuchekeshana kama vile kwenye timu za mchezo wa mpira. Lakini, ikiwa na hasi si salama kwetu. Inabeba chuki na shari na kurembeshwa na liwalo na liwe. Maisha, uchumi na upendo yapo mashakani. Kwenye siasa hakuna utani wa kudumu seuze vichekesho.
Wake wenza walipolumbana kwa maneno ya si chochote yenye sura ya chanya, mashoga na wapambe hawakujali zaidi ya kutabasamu na kucheka. Walipolumbana kwa maneno yenye sura hasi ya matusi na kuonesha dalili ya kupigana, watu makini na waadilifu waliwazuia kupigana na ikawa salama kwao.
Je, Watanzania wenzangu wazalendo kweli tunatamani na kukubali kupigana kwa sababu ya chochote? Nadhani hapana! Nawaomba wanasiasa, Serikali na wapambe chonde chonde tuchukue hadhari kabla ya shari kutokea. Wahenga wamesema mwanzo wa ngoma lele.