Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Dar

Ofisa Elimu Taaluma wa Mkoa wa Dar es Salaam, Eva Mosha, ametoa rai kwa wamiliki na walimu wa shule binafsi za awali na msingi kuimarisha ufanisi wa ufundishaji na kuboresha ubora wa elimu, ili kuinua taaluma katika shule zao.

Amesisitiza ,shule hizo zinapaswa kuongeza ubunifu na kujiendeleza kwa kupata mafunzo mbalimbali ya namna ya kuendesha shule zao, ili kuepuka changamoto za kushindwa kuendeleza shule au kukosa wanafunzi.

Mosha alitoa rai hiyo katika hafla ya kupongeza walimu na wamiliki wa shule binafsi za awali na msingi, ambazo zinatoa ada nafuu, waliopatiwa mafunzo ndani ya miaka mitatu kupitia mradi wa Opportunity International ,kwenye ukumbi wa Victoria uliopo Kimara Temboni, Dar es Salaam.

Mosha alieleza kuwa, shule nyingi binafsi zimekuwa zikikumbwa na changamoto za kufa au kushindwa kupata wanafunzi kutokana na kukosa usimamizi mzuri, mipango thabiti, na mbinu bunifu za ufundishaji.

Alisisitiza umuhimu wa kuboresha usimamizi na mbinu za ufundishaji ili shule binafsi ziweze kudumu na kuongeza idadi ya wanafunzi.

Mratibu wa Mradi wa Opportunity International Tanzania (HES Tanzania), Oliver Kapaya, alieleza kuwa mradi huo ulianza mwaka 2018 na umefanikiwa kuhusisha shule 101 katika kipindi cha miaka mitatu.

Alieleza, shule 74 zilipata mafunzo na kufuzu kwa kipindi cha miaka minne na shule 15 zimefanikiwa kupata tuzo za kutambua ufanisi wao huku, shule nane zimetunukiwa tuzo kwa utendaji bora.

Oliver aliongeza, mradi huu ni endelevu, ambapo shule na walimu wanaosajiliwa wanapata mafunzo na kila baada ya miaka mitatu shule nyingine zinajiunga na mradi.

Violet Oketch, mratibu wa Mradi wa Opportunity International Afrika (HES Africa), alibainisha kuwa mradi huu unatekelezwa katika nchi nane za Afrika, ikiwa ni pamoja na Tanzania, Rwanda, Zambia, Ghana, DRC Congo, Uganda, Kenya, na Nigeria.

Oketch alieleza kuwa lengo kuu la mradi ni kuhakikisha watoto wa shule za awali na msingi wanapata elimu bora ili kuinua taaluma zao na kufungua fursa za maendeleo.

“Leo tunasherehekea miaka mitatu ya utekelezaji wa mradi huu, na mwaka mmoja wa majaribio ambao umeonyesha mafanikio katika kusaidia shule kujitegemea.”

Violet Oketch alishukuru serikali ya awamu ya sita kwa ushirikiano wake na wawekezaji na wafadhili mbalimbali katika sekta ya elimu. Alisema kuwa ushirikiano huu unachangia kuboresha sekta binafsi na shule za serikali.

Brayson Ephata Maleko, Ofisa Elimu Vifaa na Takwimu Temeke, alisema kuwa mradi huu unahusisha wanafunzi wa shule za awali na msingi katika wilaya za Temeke, Kinondoni, Ubungo, na Kigamboni.

Alieleza kuwa, kupitia mradi wa “Edu Quality,” walimu wamefundishwa namna ya kuendesha shule kwa ufanisi, kupanga mipango, na kusimamia rasilimali fedha.