Na Padri Dk. Faustin Kamugisha

Kuna ambao wanatazama walivyonavyo wanashukuru. Kuna ambao wanatazama wasivyo navyo wanalalamika. 

Shukrani ni mtazamo. “Shukuru kwa ulivyonavyo; utaishia kuwa na zaidi. Ukifikiria ambavyo hauna, havitatosha kamwe,” alisema Oprah  Winfrey.   

Wanawake ambao hujishughulisha na kufua nguo katika baadhi ya sehemu za Mexico wamebarikiwa . Sehemu hizo zina chemchemi zenye maji moto na baridi sambamba. Wanawake huosha nguo zao kwenye maji moto na kuzisuuza kwenye maji baridi. 

Mtalii ambaye alishuhudia upendeleo huu alimwambia rafiki wake wa Mexico: “Nafikiria kuwa wanawake wanamfikiria Mama Dunia, Mama Maumbile kuwa ni mkarimu.” Rafiki yake alijibu: “Hapana bwana, kuna ambao wanalalamika kuwa Mama Dunia au Mama Maumbile hatoi sabuni.” Huo ni mtazamo hasi.  Mwenye mtazamo hasi anasisitiza anachokikosa, si kile alichonacho. Furahia ulicho nacho. Shukuru kwa ulichonacho. Thamini ulichonacho.  Pendezwa na ulicho nacho.

Mtume Paulo wa Tarsus anatuasa. “Shukuruni kwa kila jambo.” (1 The 5:18). Usilalamike wakwe hawaeleweki. Shukuru una mke. Shukuru una mume. Umezaa mtoto usilalamike mbona ana pua kubwa. Mshukuru Mungu una mtoto. 

Kushukuru kunahitaji mtazamo chanya, si mtazamo hasi. Mwenye mtazamo hasi akiosha vyombo vingi baada ya chakula analalamika vyombo vimekuwa vingi. 

Lakini mwenye mtazamo chanya anasema ninamshukuru Mungu mapochopocho yalikuwa mengi. Mwenye mtazamo hasi analalamikia sana msongamano wa magari kwenye miji mikubwa. Lakini mwenye mtazamo chanya anamshukuru Mungu kwa kuwa na gari. 

Mwenye mtazamo hasi kila mara analalamika anaona tunda nje ya lango lake ni tamu na nyasi nje ya uzio wake ni za kijani sana.

Shukrani ina nguzo saba. Kwanza, kushukuru ni kusifu. Kuna aliyesema: “Kumsifu Mungu ni mwanzo wa shukrani, mtu ambaye hamsifu Mungu hajamshukuru.” Mungu anasimama juu ya masifu. Katika shida Ayubu alimsifu Mungu. Alisema: “Bwana ametoa, Bwana ametwaa, jina lake litukuzwe.” (Ayubu 1:21). Mungu hakumwacha.

Nguzo ya pili ni kusema, asante, ni kukiri na kutangaza. Shukrani ambayo haijasemwa ni kama ujumbe ulioandikwa kwenye simu usitumwe. 

Ni barua iliyoandikwa isitumwe. Shukrani ni suala la moyo na mdomo. Sema “Asante sana” kwa machache na makubwa, kwa vitu vya kawaida na visivyo vya kawaida. 

“Kile ambacho hauwezi kukilipa kwa fedha angalau kilipe kwa shukrani,” alisema Karl Simrock. Hauhitaji fedha kusema maneno “Asante sana.” 

Kushukuru ni kulipa deni. “Yeyote anayepokea tendo jema kwa moyo wa shukrani tayari huwa amelipa awamu ya kwanza ya deni,” alisema Seneca, mwanafalsafa wa Kigiriki. Maneno “asante sana” ni sala nzuri sana ambayo mtu yeyote anaweza kusali mara nyingi.

Nguzo ya tatu ni upendo kwa mtoa zawadi. “Tunapotoa shukrani zetu, tusisahau kuwa upeo wa juu wa kushukuru si kutaja maneno ya shukrani bali kuyaishi,” alisema John F. Kennedy. 

Upendo ni maisha. Wahaya wana methali isemayo: “Chumvi iwe tamu, muuzaji anuke?” Kuna wanaofurahia chumvi lakini hawampendi muuza chumvi. Penda mtoaji.

Nguzo ya nne ni kukumbuka. Tatizo kubwa ni kusahau tunayopaswa kukumbuka na kukumbuka tunayopaswa kusahau. Kukumbuka ulichopewa ni jambo muhimu. 

Waluya wa Kenya wana methali isemayo: “Nyama choma haiwezi kuwa tamu sana ukamsahau aliyeichoma.” Maisha hayawezi kuwa mazuri tukamsahau Mungu na wale wanaoyafanya yawe mazuri.

Nguzo ya tano ni kuthamini zawadi. Kuna maneno kwenye kanga yasemayo: “Zawadi ni chochote kupokea usichoke.” Ulivyovipokea vina thamani, vithamini. 

Kuthamini ni kutotumia zawadi vibaya kwa namna ambayo haimpendezi mtoaji. Kipimo cha shukrani ni namna tunavyotumia yale Mungu aliyotujalia.

Nguzo ya sita ni unyenyekevu kwa mtoaji na mpokeaji. Kuna methali ya Wahaya isemayo: “Orwokubimpa okampera oreka nsiba.” (Heri kushinda njaa kuliko kupewa chakula na matusi juu yake). 

Unyenyekevu ni kutambua kuwa mazuri yote yaliyopo duniani hukuyatenda wewe na mabaya yote hukuyatenda wewe. Waliokusaidia wape heshima. Daraja lililokuvusha usilitukane.  Ngarawa iliyokuvusha mtoni, usiite kinyangalika. 

 Pango lililokusitiri, lisitiri. “Nani amekupendelea wewe? Una kitu gani wewe ambacho hukupewa? Na ikiwa umepewa, ya nini kujivunia kana kwamba hukupewa?” (1 Wakorintho 4:7).

Nguzo ya saba, kushukuru ni kuomba tena. Kushukuru ni maombi na maombezi. Shukrani ni moyo wa kutegemea kupata misaada siku za baadaye. 

“Fikiri kama ungempatia mtu zawadi na akadharau kukushukuru kwa zawadi uliyompa je, ungempa nyingine? Maisha ni hivyo hivyo. 

Ili kuvuta baraka  zaidi ambazo unaweza kupata maishani lazima kushukuru kile ambacho unacho tayari.” (Ralph Marston). Ili kusisitiza ukweli huo Wahaya wanazo methali mbalimbali: Entasima ehabwa limoi (Ambaye hashukuru hupewa mara moja); Entasima ekalya omutima gw’emanzi (Asiye na moyo wa kushukuru alimkatisha tamaa mtoaji).