Na Stella Aron, JamhuriMedia, Bagamoyo

Imeelezwa kuwa kati ya vyanzo vinavyochangia migongano kati ya binadamu na wanyamapori ni kufanyika kwa shughuli za kibinadamu kama kilimo na ufugaji kwenye mapito ya wanyamapori.

Hayo yamebainishwa leo Septemba 5, 2024 na Ofisa Mhifadhi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Isaac Chamba wakati akitoa mada kwenye mafunzo yaliyoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) kwa wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari wilayani Bagamoyo mkoani Pwani.

Chamba amesema kutokana na uvamizi huo wanyama hushindwa kupata mahitaji yao kama maji na chakula.

Amesema kuwa pia uvamizi wa mifugo maeneo ya hifadhi, mabadiliko tabia nchi na kutokuwepo kwa matumizi bora ya ardhi ni kati ya sababu zinazochangia kuibuka kwa migongano hiyo.

” Kutokana na sababu hizo Wilaya ya Manyoni mkoani Singida inaongoza kwa kuwa na migongano mingi hivyo ni vyema jamii ikaelimishwa juu ya umuhimu wa shoroba” amesema.

Ameongeza kuwa matukio ya migongano baina ya wanyamapori na binadamu yalikuwa 997 kwa mwaka 2018 lakini yameongezeka kwa kasi hadi kufikia matukio 3,496 mwaka jana na mengi yakihusisha uvamizi wa tembo.

Amesema takwimu za mwaka 2023/2024 zinaonyesha kuwa Wilaya ya Manyoni mkoani Singida ilikuwa na matukio 410, Nachingwea matukio 312, Lindi 260, Tunduru 218, Busega 214, Rufiji 202, Bunda 158, Liwale 112 na Chamwino matukio 111.

Amesema tembo amekuwa akichangia kwa asilimia 80 kwenye migongano hiyo akifuatiwa na Simba asilimia sita, Kiboko asilimia tano, Kifaru asilimia nne, Mamba asilimia tatu na Fisi asilimia mbili.

“Kuna wakati mifugo ya kawaida inavamia hifadhini kwa mazingira ya kawaida wanyamapori hawapatani n kwa sababu wanaofugwa wengine wanaofuungwa hufungwa kengele au kupuliziwa dawa za aina mbalimbali.

“Kwa hiyo wanyamapori wanapokutana na mazingira hayo ya harufu ya dawa au kelele za kengele huona kero hivyo wanahama maeneo yao na wanajikuta wamehamia kwenye maeneo yenye makazi ya watu na hapo ndipo migongano inapoanza,” amesema.

Pia amesema imani potofu imekuwa ikichangia baadhi ya makabila kuwatumia wanyama wakali kama fisi kama chombo cha usafiri na chombo cha kufanyia mawindo kwenye maeneo yao.

“Kuna makabila baadhi ya watu wanafuga fisi kwenye makazi yao sasa hao wanyama wakati mwingine wanavamia na kuua mifugo ya wananchi wengine na kusababisha migogoro na wenye mifugo,” amesema.

Awali Mkurigenzi Mtendaji wa JET, John Chikomo amesema mafunzo hayo ya siku mbili ni sehemu ya mradi wa kupunguza migongano baina ya binadamu na wanyamapori unaotekelezwa na Wizara ya Maliasili na Utalii nchini Tanzania kwa miaka mitano unaofadhiliwa na Serikali ya Ujerumani kupitia Shirika la Maendeleo ya Ujerumani (GIZ).

Amesema kuwa mradi umelenga katika ukanda wa Ruvuma kwa maana Wilaya ya Tunduru, Wilaya ya Namtumbo na Wilaya ya Liwale mkoani Lindi.

Chikomo amesema kuwa kazi kubwa inayofanywa katika mradi huu ni kufundisha waandiahi wa habari ambapo mafunzo ya awali yalifanyika Februari mwaka huu.

“Lakini pia tulikuwa na mkutano na wahariri wa vyombo vya habari kutoka JET na waandishi wanaotekeleza mradi huu na tulikuwa na midahalo ambayo ilifanyika kwenye televisheni ya TBC Safari na tunategemea Septemba 11 kufanya mdahalo mwingine” amesema.

Please follow and like us:
Pin Share