Matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA), yameshika kasi na kurahisisha upatikanaji wa taarifa mbalimbali kwa urahisi kwa wananchi kuhusiana na masuala ya kijamii, kiuchumi, kielimu, kiafya na kisiasa. Kutokana na ukuaji wa kasi ya matumizi hayo ya TEHAMA, taasisi ambazo zimelegalega kuendesha shughuli zake kwa njia ya mtandao zimejikuta zikiachwa na pengine kuwa na mkwamo wa kiuchumi. Kampuni mbalimbali zimeamua kuingia katika biashara kwa njia ya TEHAMA na kurahisisha shughuli zake kwa kuwafikia watu wengi kwa muda mfupi, kuongeza masoko ndani na nje ya nchi kukuza uchumi kwa mtu mmoja mmoja na kwa taifa. Mfano wa kampuni hizo ni Kampuni za simu za viganjani na zile zinazojihusisha na uuzaji wa bidhaa katika nchi mbalimbali kwa njia ya mtandao. Hata hivyo taasisi nyingi umma nchini, zimechelewa kuingia katika mfumo wa huu wa TEHAMA na kujikuta zikikumbwa na mkwamo mkubwa wa kiuchumi na zaidi sana kujiendesha kwa kutegemea ruzuku kutoka serikalini huku zingine zikifa kabisa. Shirika la Posta Tanzania (TPC) likiwa miongoni mwa mashirika machache ya umma makongwe yaliyosalia nchini mwaka huu linakusudia kuboresha mifumo na miundombinu yake kwa lengo la kusambaza huduma za kisasa za kimtandao katika maeneo yote nchini. Kaimu Posta Masta Mkuu, Fortnatus Kapinga, anasema mpango wa kuboresha mifumo hiyo ni kuchangia kwa kasi juhudi kubwa zinazofanywa na serikali za kuleta maendeleo ya haraka kwa wananchi. Kapinga anasema chini ya mpango huo huduma mbalimbali ikiwemo ya usafirishaji na usambazaji usiku kucha (Overnight Mail Delivery Services) unaohusisha barua, vifurushi, vipeto, magazeti na bidhaa nyingine utaboreshwa na kupanuliwa katika mikoa mingi zaidi hapa nchini. Anaelezea mikakati hiyo ya Shirika la Posta nchini wakati wa maadhimisho ya siku ya Posta barani Afrika, Kapinga kwamba itatoa hakikisho kwa wananchi kufikishiwa bidhaa zao ndani ya saa 24.
Mtandao wa Shirika la Posta Tanzania ni miundombinu ya kitaifa wenye ofisi zipatazo 375 zilizounganishwa katika mfumo wa pamoja wa zaidi ya ofisi 30,000 za Barani Afrika na pia zaidi ya ofisi 650,000 duniani kote. Anasema kupitia mtandao huo wa kitaifa Shirika hilo litatekeleza kwa kasi zaidi mpango wake huduma za uwakala kwa niaba ya taasisi nyingine za kiuchumi na kijamii ikiwa ni pamoja na Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB), Shirika la Ugavi wa Umeme (TANESCO), Benki ya Posta (TPB), Benki ya CRDB, NMB, Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na Taasisi nyingine ili zichangie vyema maendeleo ya Watanzania wengi zaidi. Pamoja na hayo, Kaimu Posta Masta Mkuu wa Shirika hilo, anasema kwa kutambua jitihada zinazofanywa na serikali ya awamu ya tano kuboresha huduma mbalimbali kwa wananchi wake ikiwa ni pamoja na kupambana uhalifu wa kimtandao ambao unajumuisha matukio ya baadhi ya wateja kutuma au kutumiwa vitu hatarishi visivyoruhusiwa kwa mujibu wa sheria za hapa nchini na kimataifa. Anasema licha baadhi ya watu kujihusisha na uhalifu huo wa kutuma vitu hatarishi uhalifu mwingine ambao umeshika kasi ni utoaji wa taarifa zisizo sahihi kwa shirika na mamlaka zingine zinazosimamia sheria hapa nchini. “Shirika linaendelea kuwakumbusha wananchi kuwa vitu visivyoruhusiwa kusafirishwa katika mtandao wa Posta kwa mujibu wa sheria ni bidhaa za kemikali za sumu, dawa za kulevya, silaha za moto, milipuko, wanyama hai, nyara za serikali, vifaa vya mionzi, vyakula vinavyooza, betri za aina mbalimbali, vimiminika, fedha haramu, utakatishaji wa fedha na vitu vyote hatarishi,” anasema Kapinga.Hata hivyo anaeleza kuwa katazo la vitu hivyo hatarishi kusafirishwa katika mtandao wa Posta limezingatiwa katika Sheria na taratibu mbalimbali za kitaifa ikiwa ni pamoja na Sheria ya Mawasiliano ya kielektroniki na Posta (EPOCA) ya mwaka 2010, Umoja wa Posta Duniani (UPU), Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO) na Shirika la Forodha Duniani (WCO). Anasema Shirika kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usimamizi wa sheria mwaka huu litaimarisha uhakiki wa mifumo yake ya ulinzi na usalama na ukaguzi wa barua, vifurushi na vipeto vinavyowasilishwa na wateja ili kujiridhisha juu ya usalama na uzingatiaji wa sheria.
Licha ya sheria ya hiyo ya uhakiki wa mifumo yake ya ulinzi, shirika hilo litaendelea na wajibu wake wa kisheria wa kutunza siri za vitu vilivyomo kwenye barua, vifurushi na vipeto vya wateja. Kwa upande wa matumizi ya TEHAMA, anasema ili kuhakikisha wananchi wa kawaida wanapata huduma za kisasa mifumo ambayo itapewa msukumo ni ule wa Posta wa kimataifa (IPS), wa Fedha wa kimataifa (IFS) na huduma za kaunta za mauzo (CAS). Kapinga anasema kutokana na uboreshaji wa mfumo wa IPS, wateja wataweza kufuatilia kwa urahisi mwenendo wa barua, vipeto na vifurushi vyao kwa wakati na mahali popote ili kafahamu vilipo kwa kutumia tovuti ya Shirika hilo. Pia kwa mfumo wa fedha wa IFS wananchi wataongeza wigo wa kutuma au kutumiwa fedha katika nchi za nje kama vile Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Comoro, Zimbabwe, Malawi na nchi nyingine zitakazoongezwa katika kipindi cha mwaka huu. Naye Meneja Masoko wa Shirika hilo, David George, anasema kwa kutumia mfumo wa kisasa zaidi ujulikanao kama Post Global Netsmart ofisi 103 zimeunganishwa katika mfumo huo ili kuboresha huduma zake na lengo likiwa kuunganisha mtandao wa ofisi zote za Posta nchini. Anasema kwa sasa soko la mtandao (online shopping) linashika kasi kubwa hivyo shirika limejiandaa kuendesha shughuli zake kwa njia ya kisasa kwa lengo la kuongeza faida na kukabiliana na ushindani wa soko. Shirika la Posta kwa sasa litakuwa wakala mkubwa wa mabenki kwa mujibu wa sheria ya mwaka 2013 na lengo ni kufikisha huduma za kibenki ambako huduma hizo hazijafika na kuongeza mapato kwa serikali. Kwa upande mwingine Kaimu Posta Masta Mkuu, Kapinga anasema kuenea kwa madai ya watu wengi kwamba matumizi ya mitandao ya mawasiliano yalivyoshika kasi nchini yanaweza kuliua shirika hilo hayana ukweli wowote ule kwani sio rahisi kwa shirika kufa kwani bado wananchi wanalitumia na kuliamini. “Licha ya matumizi makubwa ya mitandao ya mawasiliano, kwa upande wa serikali na mashirika mengine yanahitaji vielelezo halisi (Documents) kwa watu wanaoomba kazi ama huduma nyinginezo na kwa vyovyote watalazimika kutumia shirika kusafirisha barua au nyaraka hizo,” anasema. Akitoa mfano wa kuhakikisha uhai wa shirika hilo, anasema mashirika makubwa ya kimataifa kama DHL yana mtandao mkubwa katika nchi mbalimbali duniani na kuingiza mapato makubwa kwa usafirishaji wa barua na vifurushi, hivyo suala la kufa haliwezi kutokea. Kutokana na hali hiyo anasema biashara ya kusafirisha barua na mizigo ipo na inawaingizia faida kubwa wengi wanaofanya biashara hiyo na kwa Jiji la Dar es Salaam ziko zaidi ya kampuni 50. Katika mkakati wa kuhakikisha wateja wa shirika hilo na wananchi wananufaika na huduma bora za kisasa na salama ambazo ni pamoja na biashara ya mtandao, ununuzi , matibabu na elimu ili kuongeza kasi katika matumizi ya teknolojia na kuwarahisishia uendeshaji wa maisha yao ya kila siku na kukuza uchumi kwa jamii. Siku ya Posta Barani Afrika inaongozwa na kauli mbiu isemayo ‘Posta kichocheo cha maendeleo ya kiuchumi na kijamii’ mikakati ikiwa imejikita katika utoaji wa huduma bora kwa wananchi ikiwa dira ya taifa ya mwaka 2025 ya Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini (Mkukuta), Sera ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Sera ya Posta, mfumo wa anwani za makazi na postikodi na mkakati wa sasa kufufua viwanda.