Hali ya kifedha ya Shirika la Ndege la Afrika Kusini (SAA) imezidi kudorora na kulilazimisha shirika hilo kusitisha safari za ndani isipokuwa kwenda na kutoka Johannesburg na Cape Town.

Hilo limetangazwa wiki iliyopita na timu maalumu ya wataalamu wa biashara iliyopewa jukumu la kuhakikisha shirika hilo halifi.

Kwa mujibu wa Les Matuson na Siviwe Dongwana ambao wamo kwenye timu hiyo, hatua hiyo inalenga kuwezesha mabadiliko yanayofanywa ndani ya shirika hilo, yanayolenga kulifanya lianze kuzalisha faida. Pia hatua hiyo itasaidia kubana matumizi ya fedha.

Timu hiyo ilitangaza pia kuwa wanakusudia kuuza baadhi ya rasilimali za shirika hilo na kuthibitisha kuwa kupunguza wafanyakazi ni moja ya hatua ambazo zitatekelezwa.

Hatua hizo zilitangazwa muda mfupi tu baada ya Chama cha Wafanyakazi cha Numsa kuonya kuwa kuna mpango wa SAA kupunguza fedha za mishahara kwa kupunguza wafanyakazi.

Hivi karibuni Benki ya Maendeleo ya Afrika Kusini inayomilikiwa na serikali ilitoa kiasi cha Rand milioni 3.5 kwa shirika hilo ili kuliwezesha kuendelea na shughuli zake kwa muda.

Novemba mwaka jana, kabla SAA haijaanza mipango ya kujiokoa, shirika hilo lilitangaza dhamira yake ya kufanya mabadiliko ambayo yatahusisha kuwafukuza wafanyakazi 944. Numsa inahisi kuwa idadi ya wafanyakazi watakaopunguzwa ni zaidi ya hao.

Kwa mujibu wa tangazo lililotolewa hivi karibuni, safari zote za ndani ikiwemo za Durban, East London na Port Elizabeth, sitasimamishwa kuanzia Februari 29 mwaka huu. Badala yake safari hizo zitahudumiwa na Shirika la Mango, ambalo halitaathiriwa na mabadiliko hayo.

“Kwa mtandao wa safari za ndani, SAA itaendelea kushughulikia safari za Cape Town lakini zitapungua,”

inasema taarifa hiyo.

Itakapofika Februari 29, mwaka huu, SAA pia itasitisha safari za kimataifa kati ya Johannesburg hadi Abidjan kupitia Accra. Pia safari za Entebbe, Guangzhou, Hong Kong, Luanda, Munich, Ndola na Sao Paulo nazo zitaathirika.

SAA itaendelea na safari za kimataifa kati ya Johannesburg na Frankfurt, London Heathrow, New

York, Perth na Washington kupitia Accra.