Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Msalaba Mwekundu na Hilali Nyekundu (IFRC) limesema “limekasirishwa” kwamba madaktari wanane wa Kipalestina waliuawa pamoja na wahudumu sita wa Ulinzi wa Raia na mfanyakazi wa Umoja wa Mataifa na vikosi vya Israeli kusini mwa Gaza mapema mwezi huu.

Magari matano ya kubebea wagonjwa na lori la zima moto yaliyopelekwa kusaidia watu waliojeruhiwa, pamoja na gari la Umoja wa Mataifa, yalishambuliwa katika eneo la al-Hashashin tarehe 23 Machi wakati wanajeshi wa Israel wakielekea katika mji wa Rafah, kulingana na afisa wa Umoja wa Mataifa.

Miili 15 ilipatikana Jumapili kutoka kwa kile alichokiita “tukio la uharibifu”. Chama cha Hilali Nyekundu cha Palestina (PRCS) kilisema kuwa daktari wa tisa alitoweka na kushutumu vikosi vya Israeli kwa kuwalenga wafanyakazi wanaotekeleza majukumu ya kibinadamu.

Jeshi la Israel limesema wanajeshi wake walifyatulia risasi magari kadhaa yaliyokuwa “yakienda kwa mashaka” bila taa za mbele wala ishara za dharura. Ilisema mfanyakazi wa Hamas na “magaidi wengine wanane” ni miongoni mwa waliouawa.

IDF haijazungumza kuhusu mahali alipo daktari wa PRCS aliyetoweka.

Afisa mkuu wa Hamas Basem Naim alilaani shambulio hilo. “Mauaji yaliyolengwa ya waokoaji, ambao wanalindwa chini ya sheria ya kimataifa ya kibinadamu ni ukiukaji wa wazi wa Mikataba ya Geneva na uhalifu wa kivita,” alisema.

Israel ilianza tena mashambulizi yake ya kijeshi huko Gaza tarehe 18 Machi baada ya awamu ya kwanza ya usitishaji mapigano iliyoanza Januari kukamilika, na mazungumzo ya awamu ya pili ya makubaliano hayo yalikwama.

Zaidi ya watu 900 wameuawa baada ya mashambulizi ya Israel huko Gaza, wizara ya afya inayosimamiwa na Hamas imesema.

Vita hivyo vilianza wakati Hamas iliposhambulia kusini mwa Israel tarehe 7 Oktoba 2023, na kuua takribani watu 1,200 na kuwarudisha 251 huko Gaza kama mateka.

Israel ilijibu kwa mashambulizi makubwa ya kijeshi, ambayo yameua zaidi ya Wapalestina 50,000, wizara ya afya ya Gaza inayoendeshwa na Hamas inasema.