Anayedaiwa kuwa kinara wa kusambaza dawa za kulevya nchini, Ally Haji (Shikuba) na wenzake wawili, Lwitiko Adam (Tiko Tiko) na Iddy Mfuru wanatarajiwa kupandishwa kizimbani mapema wiki hii, jijini, Texas nchini Marekani.
Taarifa za uhakika zilizolifikia JAMHURI zimeeleza kwamba Shikuba na wenzake watafikishwa mahakamani ikiwa ni mara ya pili tangu wasafirishwe na kukabidhiwa kwa vyombo vya dola nchini humo.
Watuhumiwa hao wa usafirishaji wa dawa za kulevya walisafirishwa kimyakimya kwenda nchini Marekani April 2017.
Novemba 20, mwaka jana walipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza na kesi yao ilianza kusikilizwa katika hatua za awali (pre-hearing) kufuatana na sheria za nchi ya Marekani.
Akizungumza na JAMHURI, Mwanasheria wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Nchini, Edwin Kakolaki amethibitisha kuwa watuhumiwa hao tayari wameshafikishwa mahakamani.
Kakolaki amesema anachofahamu ni kwamba Marekani wana utaratibu wa ‘pre-hearing’ ambapo mtuhumiwa husomewa mashtaka yake na iwapo atakubaliana na mashtaka hayo mahakama humpatia mtuhumiwa unafuu katika adhabu.
“Kwenye pre-hearing wao wanakwambia bwana sisi tuna kesi na wewe hii na hii na hii, ushahidi wetu ni huu hapa, unakubali lipi kati ya haya. Kama unakubali, ukikubali mashitaka haya sisi tunaweza tukakupunguzia adhabu, ila ukikataa na tukakomaa na wewe hadi mwisho adhabu yake ni hii.”
Amesema utaratibu huo hutumika mwanzoni mwa mashtaka na iwapo mtuhumiwa akikubaliana nayo mahakama huendelea kama ilivyopangwa ikiwa ni pamoja na kutoa adhabu kwa mtuhumiwa.
JAMHURI limemuuliza Kakolaki iwapo watuhumiwa hao wana mawakili au la, amesema kwamba kwa sasa hajafahamu kama wamepata mawakili wa kuwatetea mahakamani, labda apewe muda wa kufuatilia kwa kina suala hilo.
Alipoulizwa watuhumiwa hao wanashtakiwa kwa kosa gani amesema wanatuhumiwa kuingiza dawa za kulevya Texas kiasi cha kilo 1.8 ya heroine. Lakini walikuwa na kesi nyingine zaidi ya tano zilizowahusisha kutokana na mtandao wao.
“Zipo kesi za awali ambazo unakuta mmoja kati ya hao yuko connected, ila Shikuba alikuwa na kesi ambayo watu wake walikuwa convicted kule na yeye mwenyewe alishitakiwa in absence na akawa convicted mpaka wakawa wametoa order ya kukamata mali zake ambazo zilikuwa ziko Marekani,” anasema Kakolaki.
Amesema kwamba Tiko Tiko na Iddy walipelekwa Marekani kutokana na mashtaka ambayo yalikuwa yametolewa na washirika wao wa kibiashara ambao waliwataja ikiwa ni pamoja na Serikali ya Marekani kuwa na ushahidi wa jinsi walivyohusika.
Kuhusu mali za Tiko Tiko ambazo zimekamatwa na Polisi (magari 8 yaliyopo Polisi Oysterbay) amesema kwamba, itafuatana na kesi iliyopo mahakamani na sheria stahiki zitafuatwa.
“Kama kuna kesi mahakani itabidi iendelee, lakini kama kuna kesi ilitangulia before na imetolewa hukumu pengine, tunaweza tukaendelea na utaratibu wa kuchukua hizo mali. Vinginevyo kama zitakaa kwa muda mrefu, zinaweza zikachukuliwa kwamba ni un-clamed properties na ikiwa ni vielelezo na ni un-clamed properties huwa kuna utaratibu wa kufanya kwa maana kwamba vinapigwa mnada.”
“Lakini nafahamu kwamba kulikuwa na tuhuma kwamba hayo magari ya Lwitiko yaliibwa Afrika Kusini, sasa hiyo kesi sijajua iliishia wapi,” amesema Kakolaki.
Makubaliano na Jeshi la Polisi
Amesema kwa sasa Mamlaka ipo kwenye mchakato wa kukubalina na jeshi la polisi ili kuwepo kwa utaratibu mzuri wa mali za watuhumiwa wa dawa za kulevya kuwa chini ya mamlaka.
“Ni kweli kwamba tumeshazungumza na polisi. Kimsingi hatujafikia agreement bado ndio tuko kwenye mchakato wa kuainisha mambo ya kukubaliana. Lakini lazima tuweke utaratibu wa jinsi gani makabidhiano yatakavyofanyika kwanza kuna suala la utawala, utunzaji wa nyaraka. Vinahitaji kuweka utaratibu mzuri wa makubaliano ya jinsi ya kukubaliana,” amesema Kakolaki.
Amesema iwapo makubaliano na makabidhiano hayo yatakamilika mali zote za watuhumiwa zitakuwa chini ya mamlaka ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya.
Jinsi walivyoingia mtegoni
JAMHURI limeelezwa kuwa Shikuba na wenzake walilengeshwa kwa kuandaliwa mtego na Serikali ya Marekani wakaingia makubaliano na wateja wao (maafisa usalama) kuwatumia dawa za kulevya kama walivyohitaji jambo ambalo walilifanikisha.
Baada ya mzigo huo kuwasili Marekani serikali ilipata ushahidi wa moja kwa moja mbinu ambazo wamekuwa wakizitumia kuingiza dawa za kulevya nchini humo. Shikuba na wenzake walisafirishwa kimyakimya kwenda nchini Marekani bila kutoa taarifa kwa mawakili wao wala ndugu.
Taarifa za kupelekwa Marekani Shikuba na wenzake; Iddy Mfuru na Tiko Adam, zilipatikana vyanzo mbalimbali ikiwa ni pamoja na mke wa mfanyabiashara huyo na mawakili wao.
Aprili 12, mwaka jana, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, ilikubali maombi ya aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Harrison Mwakyembe ya kutaka Watanzania hao washikiliwe na kusafirishwa kwenda Marekani kujibu mashtaka ya kusafirisha na kusambaza dawa za kulevya yanayowakabili nchini humo.
Baada ya uamuzi huo, kesho yake Aprili 13, mwaka jana, mawakili wa Shikuba na wenzake; Hudson Ndusyepo, Majura Magafu na Adinani Chitale, waliwasilisha katika mahakama hiyo nia ya kukata rufaa na tayari waliwasilisha sababu za kukata rufaa Mahakama Kuu ya Tanzania kama sheria inavyowataka endapo hawakuridhika.
Aliyekuwa wakili wao, Ndusyepo alikaririwa akisema kwamba, “amesikia wateja wao wameondoka nchini usiku, huku Serikali ikijua kwamba kuna rufaa Mahakama Kuu.” Wakili Magafu alipotakiwa kuzungumzia suala hilo, alisema alipata taarifa ya kuondoka kwao kutoka kwa Ndusyepo.
Aprili 10, mwaka jana, Serikali iliwasilisha maombi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu pamoja na vielelezo mbalimbali, ikiomba watuhumiwa wasafirishwe kwenda Marekani kujibu tuhuma za kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya.
Mahakama ilisikiliza maombi hayo Aprili 11, na kutoa uamuzi Aprili 12, mwaka jana ikibariki watuhumiwa hao kwenda nchini humo baada ya kujiridhisha kwa ushahidi uliotolewa mahakamani.
Hakimu Mkazi Mfawidhi, Cyprian Mkeha aliposoma uamuzi baada ya kusikiliza hoja za pande mbili, alisema mahakama kabla ya kuamua ilijiuliza maswali kadhaa, ikiwamo kama mashtaka wanayohusishwa nayo wajibu maombi yako katika utaratibu wa kubadilisha wahalifu.
Pia mahakama ilijiuliza na kubaini kuwa kuna makubaliano ya kubadilishana wahalifu kati ya nchi hizo mbili. Hakimu Mkeha alisema kama wajibu maombi watakuwa wanapingana na uamuzi huo, mahakama inawapa nafasi ya kukata rufaa ndani ya siku 15 na walifanya hivyo.
Jamhuri iliwakilishwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Edwin Kakolaki, katika kuiridhisha mahakama iliwasilisha maombi na ushahidi dhidi ya wajibu maombi, kuonyesha uhusika kwao wao katika matukio hayo.
Ushahidi ulionyesha kwamba Marekani iliwachunguza wajibu maombi kwa miaka minne na walitumia Dola 10,000 kununua dawa hizo kutoka kwa taasisi yao kubaini ukweli.
Wajibu maombi ilibainika walikuwa wakisafirisha heroin na cocaine kwa kutumia magari, na wakifikisha dawa hizo Marekani huwatumia watu kusambaza kwa kutumia ndege binafsi na Shikuba ndio kiongozi wa taasisi hiyo.
Shikuba, ambaye amekuwa akihusishwa na biashara kubwa ya usafirishaji dawa za kulevya kati ya Afrika Mashariki, Asia, Ulaya na Marekani, alikamatwa mwaka 2014 nchini, akihusishwa na shehena ya kilo 210 za heroin zilizokamatwa mkoani Lindi mwaka 2012.
Serikali ya Marekani iliamua kutaifisha mali za mfanyabiashara huyo na kupiga marufuku kampuni za nchi hiyo kujihusisha na biashara zake.
Taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Udhibiti wa Mali za Nje cha Wizara ya Fedha ya Marekani, ilieleza kuwa Shikuba ametambuliwa kama kinara wa usafirishaji wa dawa za kulevya kwa mujibu wa Sheria ya Utambuzi wa Vinara wa Dawa za Kulevya wa Nje ya nchi hiyo.
Kwa mujibu wa gazeti la The New York Times, sheria hiyo imekuwa ikitumiwa na Marekani kufuatilia wahalifu kadhaa wanaojihusisha na biashara hiyo duniani na kwamba Shikuba amekuwa akijaribu mara kadhaa kurubuni viongozi wa Serikali za Afrika kuepuka kukamatwa na kufunguliwa mashtaka kutokana na biashara zake haramu.
Inadaiwa kuwa tangu mwaka 2006, Shikuba amekuwa akiongoza wanachama wa mtandao wake kutuma shehena za dawa za kulevya kwenda sehemu kadhaa duniani kama China, Ulaya na Marekani.
Uchunguzi umebaini kuwa Rais John Magufuli alitoa maelekezo kupitia kwa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga avunje mtandao wa dawa za kulevya na kuwa anataka kuiona Tanzania isiyokuwa na wauzaji na watumiaji ‘unga’.
Rais amenukuliwa akisema haiwezekani wauza unga wakawa na nguvu kuliko Serikali. Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Jeshi la Polisi ilianzisha operesheni ya kukamata wafanyabiashara wote wanaohusishwa na dawa za kulevya jijini Dar es Salaam.
Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni ulifanya msako mkali wa kimyakimya kwa wafanyabiashara hao na kufanikiwa kumkamata Lwitiko Samson Adam ambaye anasemekana kuwa kati ya mapapa waliokuwa wakisakwa kwa udi na uvumba.
Lwikito ambaye anaelezwa kuwa ana makazi nchini Afrika Kusini, alikamatwa nyumbani kwake Magomeni jijini Dar es Salaam akiishi maisha ya tofauti na watu wengine.
“Huwezi kuamini. Lwitiko aliishi maisha ya peponi. Ukiiona nyumba yake pale Magomeni, nje si nyumba ya maana, lakini ukiingia ndani utashangaa. Nyumba imejengwa chini ya ardhi (underground). Huko kuna maisha ya peponi,” kimesema chanzo.
Katika makazi yake chini ya ardhi, kulikuwa na bwawa kubwa la kuogelea, baa na magari yote ya kifahari yapatayo manane yaliyokuwa yameegeshwa kwenye zuria.
Magari yaliyokuwa huko chini ya ardhi yana thamani hadi Sh milioni 500. Magari hayo ni pamoja na BMW X6, Lexus, Lumma CLR RS, Cooper na mengine ya kifahari.
Tiko anatuhumiwa kuwa amekuwa anauza dawa aina ya heroine kutoka Pakistan; cocaine kutoka Brazil, huku akiishi maisha ya kifahari nchini Tanzania na Afrika Kusini.
Kuvunjwa kwa mtandao
Jeshi la polisi nchini lilifanya uhamisho kwa askari wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni na Tanga kuvunja mtandao wa uhalifu, hususan dawa za kulevya ndani ya Jeshi hilo.
Asilimia kubwa ya ‘mapapa’ wa biashara hiyo haramu wapo jijini Dar es Salaam, hasa maeneo ya Kinondoni, Magomeni na Mbezi Beach.
Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani Charles Kitwanga alikabidhiwa orodha ya polisi wanaojihusisha na biashara hiyo haramu ambako majina hayo aliyakabidhi kwa aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Inspekta Jenerali Ernest Mangu.
Baada ya Mangu kukabidhiwa majina hayo, aliwataka askari wa Oysterbay kumkabidhi orodha ya majina ya wauza ‘unga’ haraka.
Mpango huo ulienda sambamba na kuwapangua baadhi ya polisi walioonekana kushindwa kuukabili mtandao wa wauza ‘unga’.
Maofisa waliohamishwa ni Kamanda wa Polisi wa Mkoa (RPC) wa Kinondoni Camillius Wambura na Mkuu wa Utawala Kinondoni, pamoja na baadhi ya askari wa kitengo cha upelelezi na wengine kutoka idara mbalimbali.
Kuhamishwa kwao inadaiwa kulitokana na kushindwa kwao kudhibiti mtandao wa dawa za kulevya nchini, kiasi cha kuifanya Tanzania kuwekwa kwenye orodha ya nchi zinazojihusisha na biashara hiyo kwa kiwango cha juu.
Awali, kabla ya matukio hayo, Tanzania ilikuwa ikitumiwa kama njia ya kupitishia dawa za kulevya kwenda Afrika Kusini, Ulaya na Amerika, lakini kadri siku zinavyokwenda inakuwa soko la dawa hizo.
Shikuba alivyokamatwa
Baada ya kuzikimbia mamlaka mara kadhaa, Shikuba (49), alikamatwa Februari 28, 2014 kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) Dar es Salaam, baada ya msako mkali wa miaka miwili.
Shikuba anahesabiwa kama mmoja wa mapapa wa unga wenye nguvu na ushawishi zaidi Tanzania, akiwa amewekeza nguvu hadi serikalini kwa baadhi ya vigogo waliokuwa wakimlinda.
Kwa mara ya kwanza alipandishwa kizimbani Machi 13, 2014, akiunganishwa na watuhumiwa wengine, Maureen Liyumba ambaye ni binti wa Amatus Liyumba aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Othman Mohammed Nyamvi aliye maarufu kwa jina la Ismail Adam na Upendo Mohammed Cheusi ambaye kwa sasa ni marehemu.
Awali baada ya Liyumba kukamatwa na heroin yenye thamani ya Sh bilioni 9.4 mkoani Lindi, walimtaja Shikuba kuwa ndiye mmiliki wa mzigo huo hivyo polisi walioanza kumfuatilia.