Ninaitaja Chadema na kuitolea mfano kwa sababu sasa hivi ndicho chama ambacho kinakabiliwa na tatizo ninalotaka kulizungumzia.
Pamoja na Chadema, karibu vyama vingine vyote vimepitia tatizo la watu kujiunga navyo kisha baadaye kuamua kuachana navyo.
Hivi sasa nchi inazungumzia hatua ya aliyekuwa Waziri Mkuu, Frederick Sumaye, kujivua uanachama wa Chadema siku chache baada ya kushindwa katika uchaguzi wa ndani wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini.
Sumaye alikuwa anawania kuchaguliwa tena kuwa mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Pwani. Lakini katika hatua ya kushangaza, akiwa mgombea pekee, alipigiwa kura nyingi za hapana, hivyo kuikosa nafasi hiyo.
Kwanza, Chadema inapaswa kupewa pongezi kwa kuweka utaratibu wa mtu kupita bila kupingwa katika kuwania nafasi ya uongozi. Ni utaratibu mzuri kwa sababu unawapa wanachama nafasi ya kuchagua mtu wanayeona anafaa.
Ni utaratibu mzuri pia kwa sababu unampa mtu anayewania uongozi nafasi ya kupimwa na wale anaotaka kuwaongoza.
Mtu anaweza kuteuliwa kugombea bila ya kuwa na mpinzani kwa sababu tu amekidhi vigezo vya uteuzi lakini hilo haliwezi kuwa uthibitisho kuwa mtu huyo anakubaliwa na wapiga kura wote kiasi kuwa anapokosa mpinzani, basi uchaguzi usifanyike na atangazwe kupita bila kupingwa. Ndicho kilichomkuta Sumaye.
Katika kauli yake ya kutangaza kujivua uanachama wa Chadema, Sumaye ametoa sababu kadhaa lakini kubwa amerusha tuhuma kwa Mwenyekiti wa taifa wa Chadema, Freeman Mbowe, na kumtaja kama mtu ambaye ndiye aliyesababisha yeye kushindwa katika uchaguzi wa kanda.
Sumaye anadai kuwa Mbowe amefanya njama ya yeye kushindwa kwa sababu tu yeye (Sumaye) alionyesha nia ya kutaka kuwania nafasi ambayo Mbowe anaishikilia kwa sasa ya uenyekiti wa taifa ambayo ni dhahiri kuwa ataiwania tena.
Kumekuwa na maneno mengi kuhusiana na suala hili la Mbowe kung’ang’ania uenyekiti wa Chadema kuwa sababu inayowafanya watu wengi wakose imani na chama hicho.
Lakini Sumaye si mtu wa kwanza maarufu kujiunga na Chadema, kisha kuondoka. Walikuwapo wengi kabla yake na ni dhahiri kuwa kwa kuwa Chadema ni chama kinachokua na kusinyaa, wapo wengine wengi maarufu watajiunga na kuondoka ndani ya Chadema. Hilo si jambo la kufikirisha sana.
Kinachopaswa kuwa kitu cha kufikirisha ni sababu ambazo wale wanaojiunga na kuondoka wanazitoa kwa uamuzi wao wa aidha kujiunga au kujiondoa Chadema. Ukiangalia wengi wa waliofanya uamuzi wa aina hiyo, ni wachache sana ambao wanazungumzia mambo ambayo ni ya msingi katika chama chochote cha siasa.
Tuanze na Sumaye na wale wote ambao wanasema Mbowe kung’ang’ania uenyekiti ndilo tatizo linalowaondoa Chadema.
Labda wanasahau tu kuwa hicho wanachomtuhumu Mbowe, na wao wanaweza kutuhumiwa kwa hicho hicho. Kama wameamua kuondoka Chadema kwa sababu Mbowe hataki kuachia nafasi ya uenyekiti, basi wanatuthibitishia kuwa walijiunga Chadema ili kuwania nafasi hiyo na walipoikosa, basi hakuna sababu nyingine yoyote ya wao kuendelea kubaki katika chama hicho. Wanafanana na Mbowe, kwa sababu wote lengo lao ni moja – uenyekiti, na kwa kuwa Mbowe amewazidi maarifa au kete, basi hawana kingine kinachoweza kuwabakisha Chadema.
Kuna watu wengi wanaoamini kuwa kilichofanywa na Sumaye kitakuwa na madhara makubwa kwa Chadema. Sikubaliani nao.
Ni kweli kuwa alichokifanya Sumaye kitakuwa na madhara kwa Chadema lakini si madhara makubwa na ya kudumu kama ambavyo baadhi wanaamini.
Nitaanza kuionea huruma Chadema pale ambapo watu hawa maarufu wanaoikimbia watafanya hivyo kwa kigezo cha chama hicho kutokuwa na itikadi nzuri inayoendana na hali halisi ya kisiasa iliyopo nchini na inayolenga kukifanya chama hicho kuwa imara.
Watu wanaodhani kuwa uimara wa chama unatokana na umaarufu wa mtu wanakosea sana. Chama ni itikadi, hivyo uimara wa chama unapaswa kutokana na itikadi.
Tutofautishe umaarufu na uimara. Chama kinaweza kuwa maarufu sana kwa sababu tu kina mwanachama maarufu. Tuliliona hilo pale Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, alipohamia Chadema na pale ambapo gwiji la siasa visiwani Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad alipojiunga na ACT-Wazalendo akitokea CUF.
Vyama hivyo vilipata umaarufu wa ghafla kutokana na umaarufu wa watu waliojiunga navyo. Lakini hilo halikumaanisha kuwa vyama hivyo vilikuwa vimeimarika.
Ndiyo maana leo hii Lowassa amerejea Chama Cha Mapinduzi (CCM) lakini Chadema bado ipo vilevile kama ambavyo Lowassa aliikuta.
Alichokileta Lowassa Chadema kilikuwa ni umaarufu na ameondoka na umaarufu wake lakini uimara wa chama umebaki pale pale. Wanaodhani kuwa Chadema si chama imara wanajidanganya. Waangalie jinsi CCM na serikali zake wanavyohangaika na chama hicho ndipo watauona uimara wake.