Hivi karibuni Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba ilimhukumu kunyongwa hadi kufa mwalimu mmoja wa Shule ya Msingi Kibeta iliyoko Manispaa ya Bukoba.
Mwalimu huyo alihukumiwa baada ya kupatikana na hatia ya kosa la kumuua kwa makusudi mwanafunzi wake. Mwanafunzi huyo alifariki dunia siku kadhaa baada ya kuadhibiwa na mwalimu wake huyo kwa kupigwa kwa kitu kilichosemekana kuwa ni kuni.
Hukumu hiyo ilipotolewa ilileta hisia mchanganyiko katika jamii kuhusu uhalali wake. Watu walikuwa wakijiuliza, je, mwalimu huyo aliua, alisababisha kifo au kifo kilitokea? Ilikuwa kwa kukusudia au bila kukusudia? Kunyongwa hadi kufa ni adhabu, kafara au mshahara wa kuua au kutenda kosa kubwa kama la kuua?
Kwa kuwa kuishi ni haki ya kila mtu, wanaharakati wengi wa haki za binadamu hupinga adhabu ya kifo. Hata hivyo, kwa kuwa adhabu hiyo hutolewa kwa waliotenda makosa makubwa kama vile kuua, kuna idadi kubwa ya watu wanaotaka adhabu hiyo iendelee kutumika.
Hoja yao kubwa ni kuhusu mtu anayestahili kulindiwa haki yake ya kuishi. Ni haki ya yupi kati ya anayeua na anayeuawa ikiwa haiwezekani kulinda haki za wote wawili kwa pamoja?
Kwa mtazamo wa haraka haraka, haki ya anayeuawa ndiyo inayostahili kulindwa. Anayeua anapaswa kujilinda mwenyewe kwa kuacha kuua. Kwa ujumla haki ya kulindwa huanzia kwa wajibu wa anayelindwa. Kila mtu ana wajibu wa kujizuia si tu kufanya makosa, bali pia kujiingiza kwenye mazingira yanayomsababishia kutuhumiwa kufanya makosa.
Katika mtazamo huo, kuna dhana kuwa adhabu ya kifo kwa wauaji ni njia mojawapo, na pengine ya lazima ya kulinda haki ya wengi ya kuishi kwa kudhibiti wauaji. Lengo ni kuwaogopesha wanaodhamiria kuua na kuondoa uwezekano wa wauaji kurudia vitendo vyao vya kuua.
Aidha, katika jamii kuna makosa yanayoaminika kuwa ni makubwa kiasi cha kustahili adhabu yoyote hata kama ni kubwa kiasi gani mradi iwe na uwezo wa kukomesha makosa hayo. Adhabu kubwa kuliko zote ni kifo, hivyo ikibidi itumike.
Ingawa sababu hizo hushawishi kukubalika kwa adhabu ya kifo, kuna wanaoipinga kwa sababu zifuatazo, ambazo hushawishi pia kutokubalika kwa adhabu hiyo.
Kwanza, hakuna ushahidi wa wazi unaoonyesha kupungua kwa mauaji na makosa makubwa katika nchi zinazotumia adhabu hizo zikilinganishwa na zile zisizotumia.
Pili, kifo cha mtu mwingine hakina manufaa kwa aliyekwishakufa. Hakuna haki inayolindwa kwa mtu aliyekwishakufa. Kuua aliyeua ni kuongeza msiba juu ya msiba. Ni bora kubakia na msiba mmoja wa aliyeuawa kuliko kuwa na misiba miwili kwa kumuua aliyeua.
Tatu, lengo muhimu la adhabu ni kumrekebisha mkosaji, lakini hakuna namna ya kumrekebisha aliyekwishakufa baada ya adhabu ya kifo kutekelezwa dhidi yake.
Nne, kwa kuwa katika hukumu uwezekano wa kumtia hatiani asiye na hatia hauepukiki, kuna umuhimu mkubwa katika kila hukumu kuhakikisha kuwa uwezekano wa kubatilisha, kurekebisha na kufidia hukumu yenye makosa unaendelea kuwapo muda wote baada ya hukumu hiyo kutolewa. Adhabu ya kifo huondoa kabisa uwezekano huo.
Katika mchakato wa kusikiliza kesi hadi hukumu kutolewa, uwezekano wa kutenda kosa moja kati ya mawili hauepukiki hata kama hakimu atakuwa mwangalifu kiasi gani. Bahati mbaya makosa haya hukinzana. Kupunguza uwezekano wa kutenda kosa moja ni kuongeza uwezekano wa kutenda kosa jingine.
Makosa hayo ni kumtia hatiani asiye na hatia, na kutomtia hatiani mwenye hatia. Kadiri hakimu anavyojitahidi kuepuka kumtia hatiani asiye na hatia ndivyo anavyoshindwa kumtia hatiani mwenye hatia. Kadiri anavyojitahidi kumtia hatiani mwenye hatia ndivyo anavyoshindwa kuepuka kumtia hatiani asiye na hatia.
Katika mazingira haya yanayomkabili kila hakimu anapotaka kutoa hukumu, wapenda haki wote hukubaliana kuwa ni bora kutenda kosa la kutomtia hatiani mwenye hatia kuliko kutenda kosa la kumtia hatiani asiye na hatia.
Ili kuepuka kumtia hatiani asiye na hatia, mara zote mshitakiwa anatakiwa achukuliwe na kutendewa kama mtu asiye na hatia hadi itakapothibitishwa kuwa ana hatia.
Aidha, mshtakiwa hatakiwi kubebeshwa mzigo wa kuthibitisha kutokuwa kwake na hatia. Mshitaki ndiye mwenye jukumu la kuthibitisha hatia ya mshitakiwa. Mahakama haihitaji uthibitisho wa mshitakiwa kutokuwa na hatia ili imuachie huru, bali kukosekana kwa uthibitisho wa mshitakiwa kuwa na hatia.
Pamoja na hayo yote, hata ikithibitika bila shaka kuwa mshitakiwa ametenda kosa, hahukumiwi bila kupewa fursa ya kujitetea na kutetewa ili kujua mazingira yaliyomfanya atende kosa.
Umuhimu wa fursa ya kujitetea na kutetewa unatokana na ukweli kwamba hali na mazingira huweza kumfanya mtu afanye jambo au aonekane kufanya jambo ambalo katika mazingira ya kawaida asingelifanya au kuonekana kuwa amelifanya.
Mwindaji mmoja kwa mfano, aliwahi kumchoma mtu mkuki akidhani ni nguruwe kwa sababu tu aliyechomwa mkuki alitokea kuwa mahali na wakati mwindaji alipotarajia nguruwe kuwepo. Kwa mtazamo wa juu juu, mwindaji huyo angeweza kutiwa hatiani kwa kosa la kuua kwa makusudi ingawa katika hali halisi hakukusudia.
Kadiri adhabu inavyokuwa kubwa ndivyo umuhimu wa kuepuka kosa la kumtia hatiani asiye na hatia unavyokuwa mkubwa ukilinganishwa na umuhimu wa kutomtia hatiani mwenye hatia.
Kwa kuwa adhabu ya kifo ndiyo kubwa kuliko zote, mchakato wa kufikia hukumu ya kifo unatakiwa uzingatie kadiri iwezekanavyo umuhimu wa kuepuka kumtia hatiani asiye na hatia.
Hata hivyo, kwa kuwa hakuna umakini unaotosha kuondoa kwa asilimia mia uwezekano wa kumtia hatiani asiye na hatia, wanaharakati wengi wa haki za binadamu wanaona ni bora adhabu hiyo ifutwe kabisa ili, pamoja na sababu nyingine, kuhakikisha kuwa hakuna asiye na hatia anayeweza kunyongwa.
Bahati mbaya baadhi ya watu, au watu wengi, baadhi ya nyakati na mazingira wakiwemo hata mahakimu hushawishika kuepuka kosa la kutomtia hatiani mwenye hatia kuliko la kumtia hatiani asiye na hatia.
Wakati mwingine katika mazingira fulani kunakuwa na shinikizo la kumpata mwenye hatia au hata wa kubebeshwa hatia. Katika mazingira ya kawaida mtu wa kubebeshwa hatia huitwa kafara, lakini katika mazingira ya kisheria hubebeshwa tu hatia na kuitwa mwenye hatia.
Kafara hutolewa kuondoa kile kinachoaminiwa kuwa ni balaa katika jamii au kuleta kile kinachoaminiwa kuwa ni heri. Kafara hutolewa kutokana na umuhimu wake (wa ukweli au wa kufikirika) katika mazingira yanayohitaji kafara hiyo na si kutokana na hatia yake.
Mwalimu aliyehukumiwa kunyongwa hadi kufa huko Bukoba alihukumiwa si kwa kosa la kuua tu, bali kuua kwa makusudi. Je, kuna uthibitisho au ushahidi wa kutosha kuhusu makusudi ya mwalimu huyo kuua, au mazingira yalishinikiza apatikane na hatia? Aliadhibiwa au alitolewa kafara?
Bila shaka yoyote kila mtu atakufa na kila kifo kina sababu ya kutokea kwake. Ingawa ni lazima kifo kitokee, hakuna muda na mazingira ya kukifanya kikubalike. Hakuna wakati ambao kifo huonekana kimekuja kwa wakati unaostahili. Kuja kwake hupingwa kwa njia zote zinazowezekana.
Mara kwa mara kinapotokea huhusishwa na mtu au watu kwa maana ya kutenda jambo lililosababisha kifo au kutotenda jambo ambalo linaaminika lingetendeka kifo kisingetokea. Sababu hizo ni kama vile uzembe, kutowajibika, uchawi, makusudi n.k.
Je, mwalimu huyu alihusika au alihusishwa na kifo cha mwanafunzi wake?
Kabla ya kujibu swali hilo ni muhimu tuzingatie ukweli kwamba kwa kawaida sababu za kifo hutajwa baada ya kifo kutokea. Hakuna mashitaka ya kuua kwa makusudi ikiwa kifo hakikutokea hata kama dhamira ya kuua ilikuwapo na hatua za kukamilisha dhamira hiyo zilichukuliwa. Kwa upande mwingine, kifo kikishatokea ni rahisi kila kitendo kinachoelekea kuchangia kifo hicho kutafsiriwa kuwa kilikusudiwa.
HALIFA SHABANI
0783 705566