Awali ya yote sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya uhai na kutuwezesha – wewe na mimi – kuishi hadi leo. Wengi walitaka wawe hai, lakini haikuwezekana; hivyo ni jukumu letu tunaoishi kumshukuru Mungu bila kikomo kutokana na rehema nyingi anazotujaalia. 

Katika Gazeti la JAMHURI Toleo la Jumanne: Agosti 23–29, 2016 Na.256 kulikuwamo na taarifa kuhusu “Mwongozo uvunaji endelevu, biashara ya mazao ya misitu katika misitu ya asili (i)”. 

Uchapishaji wa sehemu iliyobaki ya Mwongozo huo uliendelezwa katika matoleo ya Gazeti la JAMHURI yaliyofuata (Toleo la Jumanne Agosti 30- Septemba 5, 2016 Na. 257 na kumalizia kupitia Toleo Na 258 Jumanne Septemba 6-12, 2016). 

Taarifa iliyohusu Mwongozo kwa biashara ya mazao ya misitu ilitolewa na Viongozi wa Wakala wa Huduma za Misitu (TFS), Wizara ya Maliasili na Utalii. Naipongeza TFS na Wizara kwa hatua hiyo. 

Kusema kweli, Watanzania hawafurahishwi na baadhi ya wafanyabiashara wa mazao ya misitu kufanya wanavyotaka kwa kutokana na udhaifu uliopo wa Serikali kupitia Wizara husika, na vyombo vingine vya Serikali kushindwa kuisimamia misitu ya asili ili uvunaji uwe endelevu. 

Kimsingi, Mwongozo uliotolewa si kwamba ni mara ya kwanza kuwekwa hadharani. Miongozo kama hiyo imekuwa ikitolewa na Wizara. Changamoto kubwa mbele ya watendaji wakuu pamoja na timu nzima ya TFS ni misitu ya asili kutosimamiwa kisheria. Sheria ya Misitu Sura 323 RE: 2002 inazuia mfanyabiashara wa mazao ya misitu kupewa leseni ya kuvuna au kukata miti katika eneo la msitu wa asili ambao hauna Mpango wa Usimamizi (Forest Management Plan), ulioidhinishwa na mamlaka husika. 

Katika mfumo mzima wa sheria kuna taratibu za kufuata ikiwa ni pamoja na Miongozo; Kanuni na Machapisho ya Kitaaluma (Technical Orders). Kwa mfano, kutokana na utafiti kuweka kiwango cha chini cha kipenyo cha mti (minimum girth) ili kuepuka kuvuna miti michanga. Serikali huweka viwango vya chini kudhibiti kuvunwa miti ikiwa michanga. Sheria inataka pia iwapo msitu hauna mpango wa usimamizi ulioidhinishwa (approved management plan) hakuna kuruhusu uvunaji kufanyika kwenye msitu huo.

Kwa kuwa misitu mingi haina usimamizi, na taratibu za uvunaji hazifuatwi (mathalani, mti kufikia kiwango cha kuruhusiwa kuvunwa; msitu kuwa na mpango wa usimamizi ikiwa ni pamoja na aina ya miti ya kuvunwa kujulikana na ujazo wake (m3) kufahamika na kila mti kuwekewa alama kabla ya kuvunwa): wavunaji wengi wakawa wanaingia na kutoka katika maeneo yenye misitu bila kuwapo wa kuwauliza wanaenda kufanya nini huko kwenye misitu. 

Kwa kuwa ni muda mrefu hali imekuwa hivyo kwa wavunaji wa miti ikawa mazoea, hivyo hawajali kutafuta leseni au hati za kusafirisha mazao ya misitu (Transit pass). 

Isitoshe, ikatokea baadhi yetu tukakosa nidhamu kazini na moyo wa uadilifu hivyo kushindwa kusimamia shughuli za misitu ipasavyo. Kwa mfano, sheria hairuhusu kusafirisha mazao ya misitu usiku (kati ya saa 12 jioni na saa 12 asubuhi). Kwa kufahamu udhaifu uliopo katika kusimamia na kutekeleza Sheria ya Misitu, wafanyabiashara ya mazao ya misitu wasio waaminifu wamekuwa mstari wa mbele kuvunja sheria kwa kusafirisha mazao ya misitu usiku. 

Hata wengine wanaosafirisha mazao ya misitu kwa muda unaotakiwa, wamekuwa wakifanya hivyo kwa kutokuwa na nyaraka sahihi na hata kutumia malori yenye makontena ambayo mazao yakiingizwa ndani (mfano: mbao, mkaa au magogo)huwezi kuyaona kwa macho mpaka uwe na chombo maalumu (scanner); wamekuwa na kiburi cha kutosimama kwenye vizuia vya misitu (kwa mfano, maeneo ya Vigwaza, Kimanzichana na vizuia vinginevyo nchini). 

Serikali ilipoanzisha TFS ilikuwa na nia nzuri ya kuhakikisha misitu yote iliyohifadhiwa kisheria inayomilikiwa na Serikali Kuu inatunzwa na kuendelezwa kwa faida ya Taifa na watu wake. Hii ni pamoja na kuhakikisha shughuli zote zitakazofanywa na binadamu katika misitu hiyo zinatekelezwa kwa kufuata taratibu na Sheria ya Misitu (Sura 323 RE: 2002). 

Vilevile, shughuli za kibinadamu ndani ya misitu zifanyike kiuendelevu (sustainable uses). Hivyo, TFS ilianzishwa chini ya Sheria ya Wakala wa Serikali (Executive Agencies Act-Cap 245) na kupitia Tangazo la Serikali (Government Notice)-GN Na. 269 ya Julai 30, 2010 chini ya Kifungu Na. 3(1) cha Sheria hiyo ili misitu iendelezwe na itumike vizuri. 

Kupitia Tangazo hilo (GN Na. 269), Waziri wa Maliasili na Utalii aliainisha majukumu manne muhimu ya kutekelezwa na TFS pia kuorodhesha misitu ya Serikali Kuu (TT) zaidi ya 500; Hifadhi za Misitu Asilia (Forest Nature Reserves) 11 na mashamba 15 ya miti (kwa sasa yapo 18 baada ya TFS kuanzisha mashamba mapya matatu ya Korogwe (Tanga); Wino (Ruvuma) na Mbizi (Rukwa).

Kimsingi kilichofanywa na viongozi wa TFS kwa kuwakumbusha wafanyabiashara wa mazao ya misitu umuhimu wa kufuata taratibu zilizoainishwa katika mwongozo huo ni jambo zuri. 

Hata kama mwongozo kama huo ulikuwapo, naamini umefanyiwa maboresho, kwa mfano, kwenye kifungu kinachohusu kamati za kusimamia uvunaji miti kwa ngazi za wilaya. Vilevile, zipo juhudi zinazoendelea kufanywa na Wizara ikiwa ni pamoja na kuwapanga watendaji ndani ya TFS ili waongeze ufanisi katika kutekeleza majukumu. Hizi ni jitihada za kupongezwa na inatia moyo unaposikia kuwa Waziri Mkuu anapokuwa jukwaani akasema: “Lazima misitu ya asili isimamiwe kwa kuhudi zote la sivyo mito yote nchini itakauka kwa kukosa maji kutiririka ndani yake”. 

Vilevile, Waziri wa Maliasili na Utalii amekuwa mstari za mbele kukemea uharibifu wa misitu ya asili na ujangili uliokithiri. Waziri amewatangazia wanaopenda kuvuna miti bila wenyewe kupanda miti wasipewe leseni au kibali kuvuna miti. Angalizo hili liwe ni kichocheo cha kupanda miti si tu kwa wale wenye nia ya kuomba kibali cha kuvuna miti katika mashamba ya miti ya Serikali na misitu ya asili, bali watu wote wahimizwe kupanda miti na kuitunza kwa faida yao na vizazi vijavyo.

Pamoja na juhudi zote hizo bado itakuwa vigumu kudhibiti hali ya uvunaji kwenye misitu ya asili. Je, ni kweli juhudi za Serikali ndani ya TFS na Wizara zinalenga kutatua changamoto za uvunaji miti katika misitu ya asili? 

Inawezekana ikawa ndiyo, lakini pia juhudi za ziada zifanyike kwa kulenga zaidi kudhibiti uvunaji huko huko kwenye misitu yenyewe. Hii inamaanisha kwamba TFS ijipange vizuri zaidi isimamie misitu kwa uhalisia wake (i.e. Wataalamu wa misitu badala ya kukimbizana barabarani na waliovuna miti) wasimamie misitu na uvunaji ufanyike chini ya uangalizi mzuri ndani ya misitu yenyewe. 

Kuwa na mwongozo ni jambo jema ili wanaotaka kuvuna wajue nini cha kufanya. Lakini kuishia hapo hakutaleta taswira nzuri ya kudhibiti uvunaji haramu katika misitu ya asili. Sera ya Misitu ya mwaka 1998 ambayo imekuwa ikifanyiwa marekebisho, ipitishwe haraka iwezekanavyo ili iwezeshe pia kufanyika marekebisho katika sheria iliyopo kwa minajili ya kuongeza nguvu za kisheria kudhibiti uvunaji holela. 

Kwa mfano, katika sheria hiyo hakimu amepewa fursa ya kumtoza faini mfanyabiashara aliyepatikana na makosa kwa kumlipisha kati ya shilingi 0 (sifuri) hadi shilingi milioni moja. Hali kama hiyo kisheria inawapa fursa wahalifu kutozwa faini ndogo wakati mhusika amekwenda kinyume cha taratibu na kuvuna miti yenye thamani ya Sh milioni 20, lakini anatozwa faini ya Sh 50,000 tu. Huu ni upungufu makubwa unaofanya wafanyabiashara wa mazao ya misitu wasilazimike kufuata taratibu na mwongozo wa uvunaji kama ilivyotarajiwa, badala yake wanafanya wanavyotaka kwa maslahi binafsi.

Mimi naamini kukiwapo mfumo mzuri wa kiutendaji na TFS kuwa na muundo imara wa kusimamia misitu na rasilimali fedha za kutosha (adequate funding); inawezekana kudhibiti uvunaji holela wa mazao ya misitu. 

Nashauri TFS isimamie misitu yetu ya asili kwa misingi kwamba badala ya kuweka maofisa misitu wilayani na kwenye miji (District Forest Managers) wakisimamia misitu wakiwa mijini na wakifukuzana na waliokwishaiharibu wapangwe kusimamia misitu iliko. Kukiwapo maofisa wa kuisimamia misitu (Forest Managers) pia kukawapo walinzi misitu (Forest Guards) wa kutosha hali ya sasa itabadilika. 

Kusimamia mwongozo wa uvunaji bila ya kuisimamia misitu yenyewe, bado uhalifu utaendelea maana hata mfanyabiashara atakayepata leseni ya kuvuna huku akijua huko anakokwenda kuvuna hakuna msimamizi bado atafanya anavyotaka ikiwamo kukata miti ambayo itakuwa haijafikia umri wa kuvunwa au kuvuna meta za ujazo zaidi ya kiwango cha leseni. Hata kama atakamatwa na kutozwa faini, hiyo miti haitarejeshwa – imekatwa, basi inabaki kilio cha mti wenyewe na kuharibiwa mazingira.

Rai aliyoitoa Waziri wa Maliasili na Utalii hivi karibuni kwamba kusitolewe leseni za mkaa au magogo ya miti kwa mfanyabiashara kama mhusika hajapanda miti ya kutosha (i.e. aoneshe shamba la miti), sina hakika kama suala hili limewekwa kwenye Mwongozo na Kanuni. Iwapo halijawekwa, juhudi zifanyike liingizwe ili kuleta ufanisi katika utekelezaji. Naamini hii ni fursa kwa Watanzania kupanda miti kibiashara pia kuyatunza mazingira asilia ipasavyo. 

Vilevile, iwekwe wazi kwamba hakuna kuruhusu shughuli za kibinadamu zenye kusababisha kuharibika misitu ya asili iliyohifadhiwa kwa ajili ya kutunza vyanzo vya maji na bioanuai (biodiversity). 

Ni vema TFS iangalie upya muundo wake kama kweli unakidhi haja ya kufikia uvunaji endelevu katika misitu ya asili kama ilivyo kwenye mashamba ya miti. Kwa kuwa ipo zaidi ya misitu ya asili 500; chini ya TFS ni vizuri kuanza na misitu michache kulingana na rasilimali zilizopo na kuongeza nguvu kadiri hali ya fedha itakavyoruhusu. Hivyo TFS ianishe misitu muhimu kwa kila wilaya ambayo itaisimamia kwa ukaribu kuliko ilivyo sasa. 

 

Hii ni pamoja na:

(i)  Kuiwekea usimamizi thabiti (Meneja) na Wasaidizi wake (i.e. Walinzi Misitu-Forest Guards); 

(ii) Misitu husika igawanywe katika maeneo ya ulinzi (ranges) kulingana na ukubwa wa msitu. Mfano, msitu wenye ukubwa zaidi ya hekta laki nne (i.e. Mwalye (Kibondo) hekta 401,450 uliohifadhiwa 1957; Ngindo (Ulanga) hekta 557,255 uliohifadhiwa 1960; Mlele Hill (Mpanda) hekta 519,211 uliohifadhiwa 1953; Nyonga (Mpanda) hekta 578,623 uliohifadhiwa 1954; Rungwa  (Manyoni) hekta 785,840 uliohifadhiwa 1961 na Mpanda Line (Urambo) hekta 427,363 uliohifadhiwa 1955). Hii ni mifano michache tu ambako naamini uvunaji unafanyika bila ya kusimamiwa ipasavyo;

(iii) Kujengwe ofisi ya Meneja na vituo vya Walinzi misitu (Rangers’ posts). Mathalani, kila hekta 100,000 kuwekwe kituo na Walinzi Msitu kama watatu au zaidi hali ikiruhusu. Kila kituo kiwezeshwe vitendea kazi kama pikipiki, vifaa vya mawasiliano – simu au ‘simu za upepo (radio calls). Kila kituo kiainishe vijiji vinavyopakana na msitu ili kuhakikisha vinashirikishwa kikamilifu katika kuulinda msitu. Kwa utaratibu mzuri hata meneja mmoja anaweza kusimamia misitu mitatu au zaidi kulingana na mahali ilipo ilimradi kumewekwa walinzi misitu ambao watawajibika kwake. Isitoshe, hata utoaji wa leseni za kuvuna unaweza kufanywa na kusimamiwa na meneja ambaye anawajibika kwa kanda husika. 

Naamini TFS wakijipanga vizuri, kukawapo motisha na ufuatiliaji mzuri kutoka makao makuu na kanda; uharibifu wa misitu ya asili utapungua kwa kiasi kikubwa.

Vilevile, inawezekana iwapo kila mtaalamu wa misitu akitimiza wajibu wake bila shuruti, pia kukawapo mawasiliano na uhusiano mzuri kati ya TFS na Halmashauri za Wilaya, Serikali za Vijiji, NGOs na wanajamii kwa ujumla.