Kukosekana kwa sheria ya kusimamia, kuratibu na kuendeleza sekta ndogo ya fedha kwa muda mrefu nchini kumesababisha huduma kutolewa kiholela huku watumiaji na watoa huduma wakiathirika.
Kwa mujibu wa Naibu Kamishna wa Idara ya Maendeleo ya Huduma Ndogo za Fedha wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dionisia Mjema, takriban asilimia 80 ya Watanzania wanatumia huduma hizo.
Kutokuwapo kwa sheria hiyo tangu nchi ipate Uhuru, huduma zimekuwa zikitolewa kiholela, huku watumiaji wa huduma hizo wakijikuta wanatapeliwa.
Baada ya kubaini kasoro zote zilizokuwa zikiathiri sekta hiyo na kushindwa kuboreka na kuwa endelevu, serikali imechukua hatua stahiki kwa ajili ya kuziba mapungufu ambayo yamekuwa yakisumbua kwenye sekta ndogo ya fedha.
Mchakato wa kuanzisha sheria ya sekta ndogo ya fedha ulianza rasmi mwaka 2012 kwa utafiti na kukamilika mwaka 2018 ilipotungwa rasmi sheria hiyo kisha kufuatiwa na utungwaji wa kanuni zake mwaka 2019.
Kanuni ambazo zimetungwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), zimejikita katika maeneo mengi kwa kuweka masharti kuanzia usajili, utoaji leseni kwa madaraja yanayojihusisha na utoaji wa huduma ndogo za fedha.
Kanuni zinaweka mazingira ya kuhakikisha kwamba watoa huduma wanatambulika, wanavyoendesha shughuli zao pamoja na kuwa na utaratibu wa kuwa na taarifa za wateja wanaowahudumia.
Sekta ndogo ya huduma za fedha inajumuisha watoa huduma katika madaraja manne. Daraja la kwanza linahusisha taasisi zinazopokea amana wakiwamo wakopeshaji binafsi wakati daraja la pili linahusisha taasisi za huduma ndogo za kifedha zisizopokea amana wakiwamo wakopeshaji binafsi, watoa huduma kwa njia za kielektroniki na kampuni za mikopo.
Madaraja haya mawili kwa mujibu Mwanasheria ambaye pia ni mjumbe wa kikosi kazi cha utoaji elimu kwa umma kuhusu sheria hiyo, Shanii Mayosa, anasema sheria hiyo inaelekeza kwamba muda wa mwisho kwa watoa huduma kujisajili au kuwa na leseni ni Oktoba 31, mwaka huu.
Daraja la tatu ni vyama vya ushirika wa akiba na mikopo (Saccos). Makundi haya matatu sheria hii inataka kukata leseni kwanza kabla ya kuanza kutoa huduma, wakati daraja la nne linalojumuisha vikundi vya kijamii vya huduma ndogo za fedha kama Vikoba halibanwi kuwa na leseni bali kujisajili tu.
Katika usimamizi na uratibu wa daraja la tatu na nne, Benki Kuu ya Tanzania imekasimisha madaraka kwa Tume ya Maendeleo ya Ushirika kwa ajili ya Saccos na Mamlaka ya Serikali za Mitaa kwa ajili ya Vikoba.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dotto James, anasema changamoto zilizoathiri usimamizi, udhibiti na ustawi wa sekta ndogo ya fedha ni taasisi za huduma ndogo za fedha kutoa mikopo kwa wananchi kwa vigezo na masharti magumu, hivyo kusababisha madhara kwa wananchi, ikiwamo viwango vikubwa vya riba na tozo, kukosekana kwa uwazi wa masharti ya mikataba na mikopo.
Katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Kamishna wa Idara ya Maendeleo ya Sekta ya Fedha nchini, Dk. Charles Mwamwaja, alitaja changamoto nyingine ni utoaji holela wa mikopo uliosababisha limbikizo la madeni kwa wateja.
Pamoja na utaratibu usiofaa wa ukusanyaji wa madeni unaosababisha wananchi kupoteza mali na kujitokeza kwa baadhi ya wananchi wasio waaminifu na wanaotumia mwanya wa kutokuwapo kwa sheria mahsusi kutoa huduma ndogo za fedha.
Katibu Mkuu, Dotto James, anasema mambo mengine yaliyoathiri ni kuwapo kwa baadhi ya taasisi za huduma ndogo za fedha zisizotoa gawio au faida kwa wanachama au wateja wanaoweka fedha kati ya asilimia 25 hadi 30 kama dhamana ya mikopo na ukosefu wa takwimu au taarifa sahihi za uendeshaji wa taasisi za watoa huduma ndogo za fedha.
Pia kukosekana takwimu na taarifa tajwa na kusababisha serikali kutojua mchango wa sekta ndogo ya fedha katika uchumi wa taifa.
“Tatizo jingine lililobainika ni ukosefu wa utaratibu wa kuwalinda watumiaji wa huduma ndogo za fedha na kuwapo kwa mianya ya utakatishaji wa fedha haramu kutokana na taasisi za huduma ndogo za fedha kutokuwa na utaratibu wa kisheria unaozitaka kutekeleza matakwa ya sheria ya udhibiti wa utakatishaji wa fedha haramu,” anasema.
Kwa upande wake, Dk. Mwamwaja, anasema lengo la serikali ni kuweka mazingira wezeshi kwa wananchi kunufaika na rasilimali nyingi zilizopo nchini kupitia fursa za kiuchumi na kwamba hilo litawezekana kwa kutumia sekta ndogo ya huduma za fedha.
Dk. Mwamwaja anasema kuna umuhimu mkubwa wa kuwakumbusha wananchi kuzitumia huduma ndogo za fedha kufanya uwekezaji na kwamba fedha hazina thamani bila kuziwekeza.
“Halmashauri zina wataalamu ambao wanaweza kuwasaidia kuwaendeleza na kwa kuzitumia fursa hizi zitawasaidia kuongeza kipato kuondokana na umaskini kwenye halmashauri zetu 185 nchini,” anasema Dk. Mwamwaja.
“Sekta hii ni pana, lakini pia zipo fursa nyingi zinazotolewa kupitia mabenki, bima, hisa na mifuko ya kijamii, ni lazima wananchi washiriki kwa kuwapa elimu kuwa wakishiriki wanaweza kunufaika kiuchunmi na kuondokana na umaskini,” anasema Dk. Mwamwaja.
Sheria inayosimamia sekta ndogo ya fedha inaipatia Benki Kuu ya Tanzania mamlaka ya usimamizi pamoja na kumpa waziri mwenye dhamana ya Fedha na Mipango mamlaka ya uhamasishaji, utelekezaji wa sheria na kanuni zake utaweza kuitambua, kuiboresha, kuiendeleza na kuiwezesha sekta ndogo ya huduma za fedha baada ya utekelezaji wake kuanza Novemba 1, mwaka jana.
Alifafanua kuwa, kwa mujibu wa utafiti wa Finscope wa mwaka 2017, asilimia 55.3 ya nguvukazi ya taifa wanapata huduma za fedha kutoka taasisi za huduma ndogo za fedha.
Kutokana na umuhimu wa sekta hiyo, serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango ilifanya mapitio ya Sera ya Taifa ya Huduma Ndogo za Fedha ya Mwaka 2000 na kutunga Sera ya Taifa ya Huduma Ndogo za Fedha ya Mwaka 2017.
Sera hiyo pamoja na mambo mengine, imeelekeza kutungwa kwa sheria mahsusi ya kusimamia na kuendeleza sekta ya huduma ndogo ya fedha ili kuondoa changamoto za kisheria zilizokuwepo ambazo ziliathiri usimamizi, udhibiti na ustawi wa sekta hiyo.
Josephat Kasamalala, mjumbe wa kikosi kazi cha kuhamasisha sheria hiyo kutoka Tume ya Maendeleo ya Ushirika, anataja baadhi ya mambo yaliyomo kwenya kanuni hizo kuwa ni kuzitaka Saccos kutoa gawio kwa wanahisa wake, kitu ambacho hakikuwapo katika vyama vingi.
Kwa mujibu wa sheria hiyo, Saccos zitatakiwa kuongeza mtaji pale itakapotokea chama husika mtaji wake kuanza kupungua. Vilevile inaweka muda kwa vyama hivyo kuwa na mkaguzi wa hesabu kwa kipindi kisichozidi miaka mitatu.
Vikoba navyo vimewekewa kanuni za kuhakikisha kuwa vinakuwa endelevu na vinatoa huduma katika mazingira ya uwazi, tofauti na kabla ya kuwepo kwa sheria mpya.
Zahara Msangi, mjumbe wa kikosi kazi cha uhamasishaji wa sheria mpya kutoka Tamisemi, ambayo imekasimiwa mamlaka na Benki Kuu ya Tanzania kusimamia vyama hivyo, anaeleza kuwa kanuni ya 18 inaziruhusu Mamlaka za Serikali za Mitaa kukifutia usajili chama chochote kilichosajiliwa na kukaa muda mrefu bila kutekeleza majukumu.
Kanuni pia zinavikataza vikundi hivyo kuwa na matawi, haviruhusiwi kupokea amana na vinatakiwa kufungua akaunti benki kwa ajili ya kumbukumbu, tofauti na sasa ambapo fedha za wanachama zinatunzwa katika akaunti binafsi au kwenye vibubu.
Msangi anafafanua zaidi kuwa chini ya sheria hii, Vikoba vinatakiwa kuwasilisha taarifa serikalini kila robo mwaka, kutakiwa kufanya uchaguzi wa viongozi, kitu ambacho hakifanyiki sasa, hivyo kusababisha baadhi ya wanakikundi kuwa viongozi wakati wote, na matokeo yake kukosekana uwajibikaji na vikundi kufa.
Kanuni pia zinaitaka mamlaka ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kufuatilia vikundi kwa kuangalia changamoto na kujiridhisha na uendeshaji wa shughuli zao.
Kuna adhabu kadhaa zilizoainishwa kwa wale ambao watakwenda kinyume cha sheria hii. Kwa mfano, upande wa Saccos ni faini ambayo si chini ya Sh milioni 10 na si zaidi ya Sh milioni 50 au kifungo kisichozidi miaka miwili na isiyozidi mitano. Upande wa Vikoba faini si chini ya Sh milioni moja au isiyozidi Sh milioni 10.
Sekta ndogo ya fedha ni nini?
Ni huduma za fedha zitolewazo kwa wananchi wa kipato cha chini (mtu binafsi, kaya au kikundi cha ujasiriamali) zikiwemo huduma ndogo za mikopo ya fedha, mikopo ya karadha (mikopo ya vitu na vifaa mbalimbali), mikopo ya nyumba, huduma ya akiba, elimu ya fedha na ujasiriamali, huduma za bima (bima ya afya, bima za mali).
Watoa huduma ndogo za fedha ni nani?
Ni benki, taasisi za huduma ndogo za fedha, wakopeshaji binafsi, watoa huduma ndogo za fedha kwa njia za kidijitali, vyama vya ushirika wa akiba na mikopo (SACCOS) na vikundi vya kijamii vya huduma ndogo za fedha (mfano VSLA, SILC, VICOBA, Upatu n.k).
Umuhimu wa huduma ndogo za fedha
Huduma ndogo za fedha zinawawezesha wananchi kujiwekea akiba na kupata mikopo nafuu kwa ajili ya kuendesha shughuli mbalimbali za kiuchumi ili kujiongezea kipato na kujikwamua na umaskini. Pia zinawezesha wananchi kukidhi mahitaji muhimu kama vile chakula, elimu, matibabu, dharura, ajira n.k.
Umuhimu wa sera na sheria ya huduma ndogo za fedha
Sera na sheria ya huduma ndogo za fedha ni muhimu kwa kuwa zinaweka miongozo ya usimamizi na utaratibu wa kumlinda mtumiaji wa huduma ndogo za fedha.
Sera ya Taifa ya Huduma Ndogo za Fedha ya Mwaka 2017 imezingatia masuala mbalimbali ili kutatua changamoto zinazoikabili sekta ndogo ya fedha kwa kuweka miongozo ambayo serikali na wadau wengine watapaswa kuyatekeleza.
Masuala na miongozo hiyo ni pamoja na:
Kuongeza upatikanaji wa huduma za fedha, kuhakikisha uendelevu wa watoa huduma ndogo za fedha, kuimarisha usimamizi wa utoaji wa huduma ndogo za fedha.
Kuhamasisha shughuli za ubunifu na uendelezaji wa huduma ndogo za fedha, kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa.
Kuimarisha utawala bora katika sekta ndogo ya fedha pamoja na kuweka mazingira wezeshi kwa makundi yenye mahitaji maalumu, jinsia na vijana.