* DCC yataka zitangazwe kuwa adui namba moja
* Serikali yataka sheria mpya, mahakama maalum
Mapambano dhidi ya dawa za kulevya bado yana safari ndefu hapa Tanzania kutokana na kusongwa na vikwazo lukuki vikiwamo vya sheria dhaifu, ukosefu wa sera ya Taifa ya udhibiti na kuendekezwa kwa vitendo vya rushwa katika vyombo vya dola.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inakiri kuwa tatizo la dawa za kulevya hapa nchini ni kubwa, linalohitaji nguvu kubwa ya mataifa yote duniani.
“Mapambano dhidi ya dawa za kulevya hayatafanikishwa na nchi moja bali nchi zote duniani,” amesema Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, wakati akiliahirisha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mjini Dodoma, Septemba 6, mwaka huu.
Kutokana na ukubwa wa tatizo hilo, Pinda anasema Serikali inafikiria kuanzisha mahakama maalumu ili kuharakisha mashauri ya dawa za kulevya.
“Nina imani tukijipanga vizuri inawezekana… tutafika mahala tufikirie mahakama maalumu ya dawa za kulevya ambayo itakuwa na kazi moja tu ya kusimamia mashauri yanayohusu dawa za kulevya,” anasema.
Kadhalika, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi, anasema Serikali inaandaa mapendekezo ya kufuta Sheria ya Dawa za Kulevya na kutungwa mpya itakayokidhi mahitaji ya kushughulikia ipasavyo makosa ya dawa za kulevya.
Wakati Serikali ikitangaza msimamo wake huo, meli iliyosajiliwa Tanzania (upande wa Zanzibar) iliripotiwa kukamatwa nchini Italia ikiwa imesheheni tani 30 za dawa za kulevya zenye thamani ya paundi milioni 50, sawa na Sh bilioni 123 za Tanzania.
Kutokana na mazingira hayo, Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya nchini (DCC) kwa upande wake, inaona pia kuna haja ya Serikali kutangaza dawa za kulevya kuwa adui namba moja kama hatua mojawapo ya kuonesha ukubwa wa tatizo hilo hapa nchini.
“Serikali itangaze dawa za kulevya kuwa adui namba moja wa jamii yetu na kuwa ni janga la Taifa,” anasema Ofisa Tawala Mkuu wa DCC, Aida Tesha, katika mahojiano maalum naJAMHURI Dar es Salaam, hivi karibuni.
Kwa upande mwingine, DCC inaeleza kutoridhishwa kwake na sheria ya kuzuia biashara ya dawa za kulevya iliyotungwa bila kuwekewa sera inayoainisha mwongozo na dira katika kudhibiti biashara hiyo haramu.
Majukumu, kazi za DCC
Majukumu ya tume hii ni kuainisha, kutangaza na kuratibu utekelezaji wa Sheria ya Serikali ya kudhibiti matumizi na biashara ya dawa za kulevya.
“Kazi za Tume kama zilivyofafanuliwa katika kifungu cha 5 cha sheria ni pamoja na kuandaa na kutekeleza Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Dawa za Kulevya,” anasema Aida.
Anataja shughuli nyingine za DCC kuwa ni kutekeleza mikataba ya kimataifa inayohusu dawa za kulevya na kuhakikisha matakwa ya mikataba hiyo yanatekelezwa kikamilifu na Serikali.
Kadhalika, DCC huzipitia sheria na kanuni za udhibiti wa dawa za kulevya na kupendekeza marekebisho ya kuziwezesha kuendana na wakati. Pia inaendeleza jitihada za utoaji taarifa kwa umma na kuzuia matumizi ya dawa hizo.
Shughuli nyingine za tume hii ni kuweka mfumo unaotekelezeka wa ukusanyaji na uchambuzi wa takwimu za matumizi na biashara ya dawa za kulevya kitaifa, kufanya tafiti juu ya uratibu wa dawa za kulevya na kuanzisha programu za kutibu na kurekebisha waathirika wa dawa hizo.
Aida anaongeza kuwa DCC pia inaendesha mafunzo kwa watendaji wanaojihusisha na udhibiti wa matumizi na biashara ya dawa za kulevya na fedha haramu. Inaendeleza na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika udhibiti wa dawa za kulevya. Inaratibu na kusaidia shughuli za asasi na vikundi vya kijamii vinavyoshiriki katika udhibiti wa matumizi ya dawa za kulevya.
Mafanikio ya DCC
Kwa mujibu wa Aida, baadhi ya mafanikio ambayo tume hii inaweza kujivunia hadi sasa ni pamoja na kuongezeka kwa uelewa miongoni mwa jamii juu ya tatizo la dawa za kulevya.
“Tumekuwa tukitoa elimu hiyo kupitia vyombo mbalimbali vya habari na matukio ya kitaifa kama vile Maonesho ya Nanenane, Kilele cha Mbio za Mwenge, Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani, Siku ya Ukimwi Duniani na Siku ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya Duniani,” anafafanua.
Hatua ya kuongezeka kwa ushirikiano miongoni mwa vyombo vya dola kupitia Kikosi Kazi(Task Force) nayo inatajwa kuwa ni mojawapo ya mafanikio ya DCC, kwani imesaidia kuimarisha udhibiti kwa kufanya operesheni mara kwa mara.
Aida anataja mafanikio mengine yaliyopatikana kutokana na msaada wa DCC kuwa ni ongezeko la ukamataji wa wafanyabiashara wa dawa za kulevya, ambapo takwimu za ukamataji wa dawa za kulevya kati ya Januari na Agosti, mwaka huu zinaonesha kuwa watuhumiwa 2,202 walikamatwa.
Watuhumiwa hao, kwa mujibu wa Ofisa Tawala Mkuu huyo wa DCC, walinaswa na vyombo vya dola kwa nyakati tofauti katika sehemu mbalimbali hapa nchini wakiwa na dawa za kulevya aina ya heroin, cocaine, bangi, mirungi na ephedrine zenye uzito wa kilo 97,535.
Kadhalika, tume hiyo imeweza kushirikiana na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kuratibu uanzishwaji wa kituo cha tiba ya methadone kwa waathirika wa heroin katika Hospitali ya Mwananyamala, jijini Dar es Salaam.
“Pia tume imewezesha ukarabati wa jengo litalakotumika kutoa tiba ya methadone katika Hospitali ya Temeke (pia iliyopo jijini Dar es Salaam),” anaongeza Aida.
DCC imefanikiwa pia kukamilisha Rasimu ya Sera ya Taifa ya Udhibiti wa Dawa za Kulevya nchini.
Heroin na madhara yake
Heroin ni aina ya dawa ya kulevya ya unga inayopumbaza mfumo wa fahamu. Dawa hiyo inatokana na mmea uitwao ‘opium poppy’. Imekuwa ikiingizwa hapa Tanzania ikitokea nchi za Mashariki ya mbali.
Mitaani heroin huitwa majina mengi kama vile unga, brown shugar, ngoma, ubuyu, mondo, ponda, dume, farasi, n.k.
Mfamasia wa DCC, Amani Msami, anataja madhara ya heroin kuwa ni pamoja na kumfanya mtu kukosa umakini, kuzubaa na kupungua uwezo wa kufanya kazi, kuharibika kwa mfumo wa ubongo na fahamu, kupata magonjwa yakiwamo ya moyo, ini, kifua na mapafu.
“Madhara mengine ni kuupata kizunguzungu, kichefuchefu, kutapika na kufunga choo, mabadiliko ya hedhi kwa wanawake, kushuka kwa mapigo ya moyo na dozi kubwa humsababishia mtu kifo,” anaongeza Msami.
Anasema mwanamke mjamzito anapotumia heroin hujiweka katika hatari ya kupungukiwa damu, mimba kuharibika na kuzaa watoto njiti. Pia watoto wanaozaliwa hupata matatizo ya kiafya kama vile kuchelewa kukua kiakili na kimwili.
Kwa mujibu wa utafiti wa kifamasia, mchanganyiko wa heroin na pombe huleta madhara makubwa zaidi ikiwa ni pamoja na kifo.
Msami anasema watumiaji wa heroin kwa njia ya kujidunga sindano huweza kuambukizana virusi vya Ukimwi na magonjwa mengine ya damu.
“Madhara ya heroin huongezeka zaidi kutokana na kuchanganywa na sukari, kahawa, aspirin, panadol na unga,” anasema mfamasia huyo wa DCC.
Anataja madhara ya kijamii yanayosababishwa na matumizi ya heroin kuwa ni pamoja na kutoweka kwa mawasiliano na amani, kuvunjika kwa ndoa na uhusiano, kuongezeka kwa fujo, vurugu na uhalifu, ukosefu wa adabu kwa watoto mbele ya wazazi, walezi na jamii kwa jumla.
Cocaine na madhara yake
Mfamasia Amani anasema cocaine ni dawa ya kulevya inayotengenezwa kutokana na mmea wa coca ambao hustawi zaidi katika nchi za Amerika ya Kusini. Kitaalamu mmea huo hujulikana kwa jina la erythroxylon coca.
Cocaine, kwa mujibu wa Amani, huwa katika unga mweupe au katika hali ya mawe madogo madogo. Inajulikana kwa majina mengi kama vile snow, star dust, keki, unga, big c, bazooka, white sugar na unga mweupe.
Hapa Tanzania cocaine hupatikana kwa wingi mitaani ikilinganishwa na dawa nyingine kama vile heroin na bangi. Hutumiwa kwa njia za kumeza, kunywa, kunusa, kuvuta kama sigara na kujidunga.
“Cocaine huchanganywa na heroin, mchanganyiko ambao hujulikana kwa jila la speedball ambao ni wa hatari sana, na mara kwa mara husababisha vifo [vya watu],” anasema Msami.
Anataja madhara ya cocaine kuwa ni kuathiri mfumo wa fahamu wa binadamu, kutokwa na damu puani, kuwa na mafua makali yasiyopona, kukosa hamu ya chakula, kupanuka kwa mboni za macho, mchafuko wa damu na kupata majipu, kuongezeka kwa mapigo ya moyo na shinikizo la damu.
Madhara mengine ya cocaine ni mtu kuchanganyikiwa, kukosa ufanisi kazini, kuwa na hisia za kuwapo kwa vijidudu mwilini, magonjwa ya ini, kuharibika kwa mishipa ya fahamu, kuharibika kwa moyo, figo na mapafu, kikohozi cha muda mrefu, kupasuka kwa mishipa ya damu kichwani kunakoweza kusababisha kiharusi au kifo na kumweka mtu katika hatari ya kuambukizwa virusi vya Ukimwi.
Hata hivyo, mfamasia huyo wa DCC anasema soda aina ya coca cola haina cocaine kama inavyodhaniwa baadhi ya watu.
Vikwazo vikuu
“Kukosekana kwa Sera ya Taifa ya Udhibiti wa Dawa za Kulevya kunakwamisha jitihada za udhibiti,” anasisitiza Aida na kudokeza kuwa tayari tume hiyo imekamilisha rasimu ya Sera ya Taifa ya Udhibiti wa Dawa za Kulevya.
Kwa upande wake, Waziri Lukuvi anasema sheria iliyopo ina upungufu mwingi unaokwamisha jitihada za udhibiti kiasi cha kusababisha uamuzi katika baadhi ya kesi za dawa za kulevya kuacha hisia mbaya na kuleta utata katika jamii.
“Baadhi ya vifungu katika sheria hii vinatoa adhabu isiyoendana na ukubwa wa makosa husika, jambo ambalo linachochea kuendelea kushamiri kwa biashara hii haramu,” anasisitiza waziri huyo.
Kwa mujibu wa Aida, DCC pia haina nguvu ya kisheria ya kuchunguza, kukamata na kupekua wahalifu wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya, hali ambayo inachangia kukwaza jitihada zake katika kushughulikia tatizo hilo.
Mamlaka za kuchunguza, kukamata na kupekuwa watu wanaotuhumiwa kujihusisha na biashara, usafirishaji na matumizi ya dawa za kulevya ni Jeshi la Polisi, Usalama wa Taifa, idara za Uhamiaji, Ushuru na Forodha.
Anaeleza kwamba ingawa udhibiti wa dawa za kulevya ni suala mtambuka linalohitaji ushirikiano, bado taasisi nyingi hapa nchini hazijaonesha nia thabiti ya kusaidia mapambano hayo.
Pia kuwapo kwa watendaji wanaojihusisha na vitendo vya rushwa katika mfumo wa udhibiti wa dawa za kulevya, ni miongoni mwa mambo yanayotajwa kudhoofisha juhudi za kukabili tatizo hilo.
“Kwa mfano, mwaka 2006 vielelezo vya dawa za kulevya vilivyokuwa vimehifadhiwa katika ofisi ya Kitengo cha Polisi cha Kupambana na Dawa za Kulevya viliibwa na baadhi ya askari polisi, hivyo kusababisha kufutwa kwa kesi iliyokuwa mahakamani kwa kukosa ushahidi. Hata hivyo, Serikali iliwachukulia hatua za kinidhamu watendaji hao,” anasema Aida.
Kwa upande mwingine, Aida anasema mipaka mingi ya nchi yetu isiyo rasmi, hasa ya nchi kavu na majini ni rahisi kupenyeka. “Hali hii inasababisha udhibiti kuwa mgumu na hivyo wafanyabiashara wa dawa za kulevya kuingiza au kutoa kirahisi dawa hizo,” anaeleza.
Pia jitihada za udhibiti wa dawa za kulevya hapa nchini kwa muda mrefu sasa zimekuwa zikizoroteshwa na upungufu wa rasilimali fedha, watendaji wa vyombo husika na vitendea kazi vya kisasa.
Kiongozi huyo wa DCC anaongeza kuwa uduni wa matibabu kwa waathirika wa dawa za kulevya nao unachangia kuzorotesha mapambano dhidi ya dawa hizo, kwani hutoa mwanya kwa baadhi ya wananchi kuendelea kuzitumia baada ya kukata tamaa ya kupona.
Vyombo vya habari navyo vinatajwa kuchangia kukwaza jitihada za kupiga vita dawa za kulevya, kutokana na kupandisha gharama za matangazo na uendeshaji wa vipindi vinavyoelezea madhara ya dawa hizo kwa binadamu.
Kumekuwapo pia na kikwazo cha wananchi wengi kutoshiriki kikamilifu kupiga vita dawa za kulevya, kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo hofu ya kudhuriwa na wafanyabiashara wa dawa hizo.
Lakini pia baadhi ya wananchi wamekuwa wakijihusisha na biashara ya dawa za kulevya kwa matarajio hasi kwamba ndiyo itakayowawezesha kumiliki utajiri wa haraka bila kujali madhara yake na kujiweka katika hatari ya kukumbwa na adhabu kubwa kisheria.
“Kwa mtazamo potofu huo huo, wafanyabiashara wa dawa za kulevya wanaonekana kuwa na mafanikio kimaisha na hivyo kuwavutia wananchi wengine wenye tamaa ya utajiri wa haraka haraka, kujiingiza katika biashara hiyo bila kujali athari zake katika jamii,” anasema Aida na kuongeza:
“Vile vile, baadhi ya wananchi huwanyanyapaa na kuwatenga waathirika wa dawa za kulevya na kuwaona kama vile wamejitakia na hawastahili msaada. Mitazamo kama hiyo inakwamisha jitihada za Serikali katika udhibiti wa biashara na matumizi ya dawa za kulevya.”
Ugumu wa udhibiti wa dawa za kulevya unasababishwa pia na kubadilika mara kwa mara kwa mbinu za ufichaji, usafirishaji na uendeshaji wa biashara hiyo zinazobuniwa na wafanyabiashara husika ili kukwepa mkono wa dola.
Mipango ya baadaye DCC
Msisitizo mkubwa wa DCC ni kwamba bado juhudi zaidi zinahitajika kupiga vita biashara na matumizi ya dawa za kulevya hapa Tanzania. Kwa mantiki hiyo, pamoja na mambo mengine, ina mpango mkakati wa kuendeleza jitihada za utoaji tiba kwa kuongeza vituo vya tiba kwa waathirika wa dawa za kulevya.
“Mipango mingine ya tume ni kuendelea kuuelimisha umma juu ya madhara ya matumizi na biashara ya dawa za kulevya, kuandaa mfumo wa ufuatiliaji na tathmini wa huduma kwa watumiaji wa dawa za kulevya na kuongeza uwezo wa kiutendaji kwa kuwapatia mafunzo wataalamu wanaohudumia waathirika wa dawa hizo,” anaongeza.
Wito kwa umma, Serikali
“Nawaasa wanaojihusisha na biashara hii haramu [ya dawa za kulevya] waache tabia hiyo kwa kuwa ni hatari kwa jamii nzima,” anasema Aida.
Anaikumbusha jamii kutambua kuwa madhara ya dawa za kulevya yanawagusa watu wote na kukwaza maendeleo ya kiafya, kiuchumi, kijamii na kimazingira.
Kwa upande mwingine, Aida anawahimiza wananchi wote kushiriki, hasa kwa kuwafichua wafanyabiashara wa dawa za kulevya kwa vyombo vya dola ili waadhibiwe kisheria.
“Nawaomba wananchi wote tushiriki kuwafichua wafanyabiashara hao kwa kuwa wanaishi mitaani mwetu na wengine tunawafahamu, tusiache waendelee kuharibu watoto wetu, ndugu, jamaa na rafiki zetu,” anasisitiza.
Mbali ya kuiomba Serikali iangalie uwezekano wa kutangaza dawa za kulevya kuwa adui namba moja katika jamii yetu na janga la Taifa, kiongozi huyo wa DCC anaiomba idhamirie kuongeza nguvu katika mapambano dhidi ya tatizo hilo.
“Mapambano haya yanahitaji nguvu zaidi, Serikali iongeze rasilimali watu, fedha na vitendea kazi vya kisasa katika maeneo muhimu kama viwanja vya ndege na mipakani,” anaongeza Aida.
Hata hivyo, Ofisa Tawala Mkuu huyo wa DCC hakuwa tayari kujibu baadhi ya maswali aliyoulizwa na JAMHURI katika mahojiano haya.
Maswali hayo ni pamoja na yaliyomtaka kueleza iwapo tume hiyo inaridhika na adhabu zilizopo dhidi ya watu wanaopatikana na makosa ya dawa za kulevya, na iwapo anadhani adhabu ya kifo inafaa kwa wanaopatikana na makosa hayo hapa Tanzania kama inavyofanyika katika nchi ya China.
Swali jingine lilimtaka atoe maoni yake kuhusu mamlaka ya kisheria aliyo nayo Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), ambayo wakati mwingine humwezesha kuagiza Mahakama ifute kesi na kuwaachia huru washtakiwa wa makosa ya jinai yakiwamo ya dawa za kulevya.
“Maswali niliyokujibu mwanzo yamejibiwa kwa kirefu kabisa, naomba yanayohusu ofisi nyingine waulize wao kwa sababu wote ni Serikali moja na tunafanya kazi kwa ajili ya wananchi.
“Si vema kutafuta mchawi kwa kuangalia utendaji wa ofisi nyingine, ninaamini kufanya tathmini ya kazi unayoisimamia ni vizuri zaidi ili kurekebisha pale unapokosea.
“Wataalamu kwa DPP, au mahakamani, au ofisi nyingine ambayo si tume [DCC] wasemaji ni wao wenyewe,” ni maelezo ya Aida kwa mwandishi wa makala haya.
Sheria ya DCC
Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya Tanzania ilianzishwa kwa Sheria ya Kuzuia Biashara ya Dawa za Kulevya, Na. 9 ya mwaka 1995 (The Drugs and Prevention of Illicit Traffic in Drugs Act, No. 9 of 1995) Sura ya 95.
Sheria hii inaharamisha/kukataza uzalishaji (kilimo na utengenezaji), usafirishaji, uuzaji, uhifadhi, usambazaji, utumiaji na ufadhili au kusaidia shughuli yoyote inayowezesha upatikanaji wa dawa za kulevya nchini pamoja na kutoa adhabu kwa makosa hayo.
Kadhalika, sheria hii imeweka utaratibu wa kuzuia uchepushwaji wa dawa za tiba zenye madhara ya kulevya ili zitumike kwa ajili ya tiba pekee.