Nape NnauyeWiki iliyopita hatimaye Serikali imehitimisha safari ya miaka 23 ya mchakato wa kutunga Sheria ya Huduma za Habari (MSB). Sheria hii inajihuisha zaidi na utendaji wa vyombo vya habari na wanahabari. Mchakato huu ulianza rasmi mwaka 1993 na umehitimishwa mwaka 2016. Waliouanzisha mchakato huu baadhi wamefariki dunia kabla ya kuona hitimisho lake, akiwamo Dk. William Shija aliyefariki mwaka 2014.

Niseme mapema, kuwa sitajikita katika kuchambua kifungu kwa kifungu, bali nitagusia baadhi ya maeneo ya sheria hii, na utaratibu uliotumika kuitunga. Najizuia kuingia katika vifungu kwa undani, kwani wadau tunapaswa kukaa tukajadili kwa pamoja sheria hii kuangalia maeneo na kubaini nini kimeingizwa au kuondolewa kwa kulinganisha na sheria iliyotangulia.

Sitanii, niseme mchakato huu uligubikwa na upotoshaji wa hali ya juu. Kwa upande wa Serikali, zimesambazwa taarifa potofo kuwa wadau wamehongwa na mmoja wa wamiliki wa vyombo vya habari kukataa muswada. Taarifa hizi zimesambazwa hadi ngazi za juu, wakati uhalisia mtu huyo anayetajwa alikuwa akivisihi vyombo vya habari muda wote vitumie majadiliano badala ya mapambano na Serikali.

Hoja hii ilitokana na wazo la wadau kutaka kushirikisha wanahabari kutoka nchi nzima katika mchakato huu wa kutunga sheria. Walitaka wanahabari waliopo mikoani kupata fursa ya kutoa mawazo yao kueleza nini kilichomo katika muswada huu, ila kwa bahati mbaya hili likatafsiriwa kuwa ni nia ya kuzuia mchakato wa kutunga sheria.

Kwa muda wote, wadau wamekuwa wakisema kuwa hawapingi ujio wa sheria hii kwani wao ndiyo walioomba ujio wa sheria hii, ila baadala ya dhana ya msingi kueleweka kuwa wanalenga kupanua wigo wa ushirikishaji, wakaishia kushushiwa tuhuma za rushwa.

Sitanii, kama yupo mtu aliyevuruga mchakato wa kutunga sheria hii, basi ni Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CCM), Peter Serukamba. Kimsingi Serukamba amejipendekeza kwa serikali kupita kiasi. Alisahau wajibu wake wa kuwa Mwenyekiti wa Kamati akageuka kuwa msemaji wa Serikali.

Tofauti na miswada mingine, ambayo wadau hualikwa kwenye Kamati kutoa maoni kwa uhuru, Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii ya Bunge inapaswa kujitathmini. Oktoba 19, 2016 wadau walipofika mbele ya Kamati kutoa maoni, walidhalilishwa. Wadau walipangiwa viti vya nyumba kama si washiriki wa shughuli hiyo.

Si hilo tu, kadri walivyoingia maafisa wa Serikali na maafisa usalama, wadau walisongwa na kusogezwa karibu na nje ya ukumbi. Nilimuuliza Serukamba iweje Kamati yake ishindwe kuwapatia wadau angalau meza ya kuwasilishia maoni, akasema kwa hasira nisiyojua ilitokana na nini, “mtapewa meza.” Hadi tunaondoka mbele ya Kamati iliyokuwa inavutana kwa kiwango cha kutisha hatukupewa meza.

Sitanii, wapo wanaosema kuwa Serukamba katika mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, alikuwa mfuasi wa karibu wa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa. Wanasema Serukamba anatumia nguvu kubwa kumwaminisha Rais John Pombe Magufuli kuwa yeye si mmoja wa ‘waliokatwa mkia’. Nasema hata kama anatafuta cheo, basi apime kiwango cha kujipendekeza! Sitamzungumzia Dk. Harrison Mwakyembe maana huyo aliishachagua kuwa adui wa vyombo vya habari!

Kuhusu muswada, bado kuna tatizo la kifungu kinachoipa Serikali mamlaka ya kuelekeza vyombo vya habari binafsi cha kuandika. Kifungu hiki kimefikisha uhuru wa uhariri. Kikitumiwa vibaya, basi nchi hii itajikuta Waziri mwenye dhamana na masuala ya habari akigeuka Mhariri wa vyombo vya habari vyote. Napata tabu kuujadili kwa kina muswada huu, kwani hotuba aliyotoa waziri bungeni na mahudhui ya muswada vinatofautiana.

Kuna eneo ambalo sioni aibu kulizungumzia kwamba ni jambo zuri katika muswada huu. Hili si jingine bali ni kuanzishwa kwa Baraza la Huru la Habari. Baraza hili litashughulikia maadili na mienendo ya wanahabari, hali itakayosaidia kudhibiti viwango vya wanahabari na hatimaye kuboresha ubora wa huduma ya habari kwa jamii yetu. Wiki hii wadau tutajadiliana kuona muswada umebeba au kuacha nini, ila nasema sasa inatupasa kuelekeza nguvu katika mchakato wa kutunga Kanuni.