Aprili 7 ni siku ya kumkumbuka mwasisi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume. Mzee Karume aliuawa nikiwa na umri mdogo; kwa maana hiyo sikumwona.
Nimemjua kiongozi huyu shupavu kupitia hotuba zake na maandishi yanayomhusu. Ni miongoni mwa viongozi wa awali wa Afrika waliokuwa na maono makubwa.
Ukiacha ukweli kwamba elimu yake haikuwa kubwa kama waliyonayo viongozi wengi wa leo wa Zanzibar na Tanzania kwa jumla, Mzee Karume kawapiku.
Mara ya kwanza nilipofika Unguja nikiwa na uelewa, sikupata shida ya ‘kumuona’ Mzee Karume. Kadhalika, nilipozuru Pemba ‘nilimuona’ Mzee Karume. Kwa Zanzibar, Mzee Karume yupo kila mahali!
Karume niliyemwona yupo katika alama alizoiachia Zanzibar. Ukifika Michenzani, ukifika Wete na kwingineko kote Visiwani, utayaona matunda ya kazi kubwa na iliyotukuka iliyoachwa na Mzee Karume. Laiti kama majahili wasingemtoa roho mapema, pengine Zanzibar ingekuwa tofauti kabisa na ile aliyoiacha.
Viongozi wetu hawakosi maneno mengi ya kisiasa, likiwamo lile maarufu la ‘kuwaenzi waasisi’. Sijui ni kwa namna gani viongozi wetu – wa Visiwani na Bara – wanafuata nyayo za shujaa huyu na kuwaenzi kwa vitendo.
Mzee Karume ni mfano wa aina ya viongozi tunaowahitaji katika nchi yetu. Tunahitaji viongozi wenye maneno machache, lakini wenye wingi wa vitendo vyenye manufaa kwa nchi yetu.
Mwaka huu tunaelekea kwenye Uchaguzi Mkuu. Tutawapata viongozi mbalimbali.
Kwa bahati mbaya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na vyama vingine vya siasa wanaufanya uongozi, hasa urais, kama ni jambo la siri mithili ya jando na unyago. Hadi leo, tukiwa tumesaliwa na miezi takribani mitano, hatujajua nani atakuwa nani katika nchi yetu.
Binafsi, nadhani hili la watu kutotangaza mapema nia na kuchukua fomu za kuwania nafasi kubwa kama ya urais, ni kosa. Ni vema wakajitokeza mapema ili wananchi waweze kuwajua kina ‘Karume’ watakaowafaa katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya Taifa letu.
Tunahitaji kuwapata viongozi makini ambao watatumia muda mrefu kuwatumikia wananchi mijini na vijijini badala ya kuwa mabingwa wa kusafiri kila kona ya dunia. Tunahitaji kuwapata viongozi ambao wanaweza kukataa kwenda safari fulani kwa sababu watu wao wanaowaongoza wanakabiliwa na mambo mazito — iwe ni katika kata, jimbo la uchaguzi au urais.
Tunapaswa kuwapata viongozi watakaokuwa na vipaumbele vichache watakavyosimamia ili kuhakikisha wanavitekeleza.
Viongozi wa aina ya Mzee Karume kwa sasa ni adimu mno. Ni wachache wanaokosa usingizi kwa kuhangaishwa na matatizo ya wananchi. Ni wachache wanaotaka waking’atuka, au siku Mola akiwaita, wawaache wananchi wakiwambuka kwa mazuri waliyowatendea.
Viongozi wengi wa sasa si wa kuyaangalia na kuyapatia ufumbuzi matatizo ya wananchi. Ni viongozi waliopo madarakani kwa ajili ya matumbo na familia zao. Haishangazi leo kuziona familia na walio karibu na viongozi wakinona ghafla kwa ukwasi mkubwa wa kutisha.
Tumeona viongozi wakiingia madarakani wakiwa masikini kama walivyo Watanzania wengi, lakini miezi au miaka michache madarakani, wao, familia zao na pengine lile kundi linalojipendekeza kwao wamekuwa na ukwasi mkubwa.
Tunaona na kusikia kila siku namna viongozi wanavyojitwalia ardhi kubwa. Wanataka wamiliki kila wanapotaka. Mzee Karume alikuwa tofauti.
Aliposhika madaraka alihakikisha kila Mzanzibari anapata ardhi. Alifanya hivyo kwa kuamini kuwa ardhi ndiyo baba na mama wa maendeleo yote.
Mzee Karume hakuwa na tamaa ya kujenga nyumba za kifahari kwa ajili yake na familia yake, ndiyo maana hakuona uvivu kuhakikisha kila Mzanzibari anapata sehemu nzuri ya kuishi. Kuhakikisha hilo linawezekana, ndiyo akafanya kile tunachokiona Michenzani na kwingineko.
Hakuwa kiongozi wa ‘upembuzi’, ‘upembuzi yakinifu’, ‘usanifu’ wala ‘mikakati’. Alikuwa kiongozi wa vitendo. Kuna hadithi inazungumzwa juu ya alivyoamua kufanyika kwa ujenzi wa Hoteli ya Bwawani. Tunaambiwa kwamba wapo ‘wasomi’ mainjinia waliopinga wazo lake la kujengwa hoteli katika eneo hilo. Hoja yao kuu ilikuwa kwamba eneo hilo halifai kujengwa nyumba aliyokusudia ijengwe. Waling’ang’ania hoja ya kwamba eneo hilo kuna maji mengi.
Tunahadithiwa kuwa Mzee Karume alipinga madai hayo, na akiwa kiongozi mkuu mwenye sauti ya utawala akaamuru ujenzi ufanywe. Matokeo yake hadi leo Hoteli ya Bwawani ipo.
Leo tuna wasomi wengi ambao ni kama wapiga ramli tu. Tuna wasomi wanaohitimu masomo ya kuwawezesha kuipanga miji yetu vizuri. Maelfu kwa maelfu ya vijana wanahitimu masomo hayo kila mwaka. Hebu tuitazame miji yetu tuone kama kweli ni miji ya nchi inayotoa wasomi wengi wa taaluma ya mipango miji.
Viongozi wetu wa sasa wameshindwa kulifanya lile lililofanywa na Mzee Karume aliyetambua kuwa watu wanaongezeka, lakini ardhi haiongezeki. Kwa kulijua hilo, Mzee Karume akaona ujenzi wa maana ni ule wa ghorofa. Hebu tujiulize, wale watu wanaoishi kama wanyama kule Manzese na katika miji mingine nchini, ni kwa namna gani siku moja wataishi vizuri kwenye nyumba kama zile zilizojengwa na Mzee Karume?
Leo tunapomkumbuka Mzee Karume, viongozi wetu hawana budi kujitafakari kama kweli wapo kwa ajili ya kuifanya Zanzibar na Tanzania yote kuwa mahali salama pa kumwezesha mwananchi kuishi kwa raha.
Viongozi wetu wajiulize kama kweli wana nia ya dhati ya kushika madaraka na kuwatumikia wananchi ili siku wakiondoka madarakani, basi kuwe na mambo mazuri au vitu vya kuwafanya wakumbukwe.
Kila anayetaka kuwania uongozi katika ngazi yoyote ajiulize ni mambo gani aliyokusudia kuyafanya ili yamfanye aingizwe kwenye vitabu vya rekodi bora za utumishi kama alivyokuwa Mzee Karume.
Ukisikiliza hotuba za Mzee Karume, unajua alikuwa kiongozi wa aina yake. Sauti yake nzito ilisisitiza juu ya umuhimu wa watumishi wa umma kuwatumikia wananchi kwa lengo la kuwaletea maendeleo.
Mzee Karume alikuwa kiongozi mkweli aliyetenda kile alichoamini kina manufaa kwa wananchi wake. Aliamini katika umoja. Hilo alilithibitisha pale alipokubali, bila shuruti, kuifanya Zanzibar kuwa sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mzee Karume alipinga aina zote za ubaguzi na uonevu. Kadhalika, hakuna mahali ambako Mzee Karume alisikika akihimiza ubaguzi miongoni mwa wananchi. Lililo dhahiri ni kuwa alichukia mno Mwafrika kunyanyaswa. Viongozi wetu wa leo hawana budi kuyatafakari hayo na kuona kama wanachokifanya kinalenga kuiona Zanzibar ikiwa moja, na pia Tanzania ikiendelea kudumu katika umoja na mshikamano.
Mwaka huu wa uchaguzi ni mwaka mwingine kwa wananchi wa Tanzania kuonesha kwa vitendo namna njema ya kumuenzi Mzee Karume. Kwa wanaotaka uongozi, ni sharti wajipime kama wana vigezo vya kiuongozi kama alivyokuwa mwasisi huyo. Kwa wapigakura, ni wajibu wao kuhakikisha wanachagua watu wenye dhamira ya kweli ya kuwatumikia na kuacha alama chanya za maendeleo kwa Taifa letu.
Kwangu mimi, Mzee Karume anabaki kuwa miongoni kwa viongozi mahiri kabisa kuwahi kutokea katika Taifa letu. Alama za maendeleo alizoziacha Zanzibar zitaendelea kudumu na kumtofautisha na viongozi wengine wengi, si kwa Zanzibar pekee, bali pia kwa Tanzania nzima. Sheikh Karume hajafa na hatakufa maana ukifika Zanzibar ‘utamwona’ kupitia kazi zake njema zilizotukuka.