Zanzibar

Na Mwandishi Wetu

Wakati taifa likijiandaa kwa kumbukumbu ya miaka 50 ya kifo cha Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Mzee  Abeid Amani Karume, mwanasiasa mkongwe, Baraka Mohamed Shamte, amesema waliopanga njama za mauaji ni vigogo wa Umma Party.

Anasema vigogo wa chama hicho ndio wahusika wakuu wa mpango batili uliokatisha maisha ya kiongozi ambaye utawala wake wa muda mfupi ulileta maendeleo ya kupigiwa mfano barani Afrika.

Mzee Karume aliuawa kwa risasi Aprili 7, 1972 kwenye ofisi za makao makuu ya chama Kisiwandui.

Akizungumza na JAMHURI nyumbani kwake Mkunazini, Mji Mkongwe kisiwani Unguja wiki iliyopita, Mzee Shamte amesema kifo cha Mzee Karume kilisimamisha na kurudisha nyuma kwa zaidi ya miaka 20 maendeleo ya Zanzibar.

“Baada ya kuzuka mtafaruku ndani ya Zanzibar Nationalist Party (Hizbu), chama kilichoongozwa na Ali Mohsin, baadhi ya wanasiasa wake wakajitoa na kuunda kundi la Umma wakiongozwa na Abdulrahman Babu. Wakataka kujiunga na ASP lakini Mzee Karume akawakatalia,” anasema Mzee Shamte.

Mzee Shamte aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Kwanza wa ASP Youth League (Umoja wa Vijana wa ASP), anasema baada ya kujiondoa rasmi Hizbu, viongozi (wa Umma) walikwenda moja kwa moja nyumbani kwa Mzee Karume, Mtaa wa Kisima Majongoo kumuelezea nia yao ya kujiunga ASP, lakini akawakwepa na kuwataka waunde chama chao.

Tukio hilo, kwa mujibu wa Mzee Shamte, lilitokea kabla hata ya kupatikana kwa jina la Umma Party.

“Siasa na sera za ASP chini ya uongozi wa Mzee Karume zilikubaliwa na Wazanzibari wote. Vigogo wa Umma Party walipoona hivyo wakataka kujiingiza ASP ili wapate ngome. Mzee Karume hakuwaamini kama kweli walikuwa na nia njema,” anasema.

Mwanasiasa huyo mkongwe anasema vigogo wengi wa Umma Party waliojiondoa Hizbu walikuwa na  elimu, hivyo walikusudia kufanya mapinduzi ya kisiasa ndani ya ASP baada ya kujiunga, wakidhamiria kuiteka na kuimiliki. 

“Mpango huo ulipokwama ndipo Babu na wenzake wakaunda Umma Party. Idadi kubwa ya wanachama na viongozi wake walikuwa na asili ya Kiarabu. Hata aliyempiga risasi Mzee Karume mwaka 1972 ni kijana wa Kiarabu, Luteni Houmuod Mohamed Houmuod,” anasema.

Anasema baada ya Mapinduzi ya mwaka 1964 viongozi wa Umma Party, ZPPP, Hizbu na mshirika wao, Sultani, hawakutegemea kuiona serikali ya Mzee Karume ikiongoza nchi na kupata mafanikio makubwa kiuchumi, kisiasa na kijamii kwa haraka kiasi kile. 

“Waliompinga Mzee Karume walivunjika nguvu  baada ya kusikia Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) ikitangaza kuwa kusingefanyika uchaguzi mpaka baada ya kupita miaka 50.

“Wazanzibari waliona vyama vingi na uchaguzi ni fitina, faraka na upasi. Wazanzibari walijifunza mengi kutoka uchaguzi wa kwanza mwaka 1957 hadi 1963,” anasema mzee huyo.

Kufuatia tangazo hilo la SMZ, anasema Zanzibar ilitulia, wananchi waliishi kwa umoja, amani, mafahamiano na maelewano huku kila mmoja akijituma kwa bidii, kujitolea na kuongoza kwa ari ya uzalendo, utaifa na kusimamia maendeleo.