Mashindano ya magongo kwa mataifa ya Afrika yaliyopangwa kuanza Alhamisi wiki hii mjini Nairobi, huenda yakaahirishwa kutokana na mkasa wa shambulio la jengo la kitegauchumi la Westgate lililovamiwa na magaidi wa Al Shabaab.
Mwenyekiti wa Chama cha Mchezo wa Magongo cha Kenya, Nashon Randiak, amesema mjini Nairobi kuwa shirikisho la kimataifa la mchezo huo lina wasiwasi kuhusu usalama wa wachezaji mjini Nairobi, baada ya magaidi wa Al Shabaab kulivamia jengo hilo la kibiashara, hivi karibuni.
Licha ya Randiak kuwaeleza kwamba hali sasa ni shwari baada ya magaidi kudhibitiwa na wanajeshi wa Kenya, shirikisho hilo limesema linataka Mkuu wa Polisi nchini Kenya kuwahakikishia usalama wa wachezaji.
Randiak ameshangazwa na msimamo huo akisema mashambulizi ya magaidi hutokea kote duniani, hivyo anashangaa ni kwanini hili la Kenya linachukuliwa kama la kipekee.
Mataifa yanayotarajiwa kushiriki mashindano hayo kwa upande wa wanaume ni Kenya, Ghana na Afrika Kusini. Kwa upande wa wanawake ni Kenya, Tanzania, Ghana na Afrika Kusini.
Timu ya Tanzania ikiongozwa na Katibu wa Chama cha Magongo Mkoa wa Dar es Salaam, Mnonda Magani, tayari imeshawasili mjini Nairobi. Timu ambazo zimejiondoa kwa sababu mbalimbali na si hiyo ya shambulio la Westgate ni Nigeria, Namibia, Misri na Ushelisheli.